Thursday 4 July 2013

Mandla: Mjukuu anayeinyima usingizi familia ya Mandela

Mandla Zwelivelile Mandela

Johannesburg. Mjukuu wa Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, Mandla Zwelivelile Mandela ambaye ameibua mgogoro mkubwa katika familia ya shujaa huyo wa Afrika katika mzozo wa makaburi amekuwa na mlolongo wa visa katika maisha yake.
Visa hivyo kwa sehemu kubwa vinahusu maisha yake ya ndoa kwani ameoa na kuacha mara tatu huku akikabiliwa na kisa kingine cha kudaiwa kuuza haki za televisheni za kuonyesha mazishi ya Mzee Mandela.

Mandla ambaye jana aliamriwa na Mahakama kurejesha mabaki ya miili ya watoto watatu wa Mandela, alizaliwa mwaka 1974 na kwa sasa ni Chifu wa eneo la Mvezo. Ni msomi mwenye shahada ya kwanza ya siasa aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Rhodes mwaka 2007.
Chifu huyo wa Kabila la Xhosa amekuwa na vituko vingi katika maisha yake. Mwaka 2009 alizua utata baada ya kuuza haki ya kutangaza mazishi ya Mandela atakapokufa kwenye kituo cha televisheni cha SABC kwa Rand 3 milioni (Sh481 milioni).
Hata hivyo, suala hilo lilifikishwa katika Mahakama Kuu ya Mthatha ambako hukumu ilitoka na alipewa siku 15 kutangaza kama kweli ameuza haki ya matangazo ya mazishi ya Mandela au akanushe taarifa hizo.
Taarifa zilisema kuwa kutokana na shinikizo la baadhi ya wanafamilia na mkazo wa hukumu ya Mahakama, Mandla alilazimika kukanusha kuuza haki ya matangazo ya mazishi ya Mandela kwa kituo kimoja cha televisheni.
Mandla ambaye ni mtoto wa Makgatho Mandela aliyefariki dunia mwaka 2005 baada ya kuugua maradhi yanayofanana na ya Ukimwi, alipata hadhi ya uchifu baada ya kifo cha baba yake mwaka 2007.
Mandela ambaye alikabidhiwa uchifu wa uongozi wa watu wa Kabila la Xhosa takriban miaka 70, ndiye aliyempendekeza Mandla kuchukua wadhifa huo. Alikabidhiwa wadhifa huo mwaka 2007 wakati huo akiwa na umri wa miaka 32. Majukumu yake yalikuwa kuongoza sherehe za kimila, kutatua matatizo ya ndani ya ukoo wao na kuwakilisha Kabila la Xhosa katika masuala ya kisiasa.
Kutokana na majukumu hayo, Mandla alichaguliwa kuwa mbunge mwaka 2009 kupitia Chama cha African National Congress (ANC). Mke wake wa kwanza ni Tando Mabuna-Mandela aliyemuoa mwaka 2004. Hata hivyo, mwaka 2009, mwanamke huyo aliomba talaka mahakamani akidai kuwa mumewe huyo ni mgumba.
Mke wa pili wa Mandla ni Anais Grimaud aliyezaliwa mwaka 1990 huko Reunion ambaye alibadili jina lake na kuitwa Nkosikazi Nobubele. Walioana Machi 2010 katika ndoa ya kimila.
Septemba 2011 alipata mtoto aliyepewa jina la Qheya II Zanethemba Mandela na alikaribishwa kwa Mandela kijijini Qunu kwa taratibu za kimila. Hata hivyo, Agosti mwaka 2012, Mandla alimkataa mtoto huyo akidai mkewe alikuwa ana uhusiano na kaka yake, kesi ilifika mahakamani na waliachana kutokana na sababu hiyo.
Mkewe wa tatu ni Nodiyala Mbali Makhathini ambaye walioana Desemba 24, 2011, lakini tayari amefungua kesi ya kudai talaka.
Huyo ndiye Mandla ambaye jana alishindwa kesi ya kuhamisha makaburi na kutakiwa na Mahakama Kuu ya Eastern Cape katika Mji wa Mthatha kurudisha mabaki hayo kwenye makaburi yake ya awali katika Kijiji cha Qunu.
Amri hiyo ya mahakama imetolewa baada ya wanafamilia 16 ya Mandela kufungua kesi ya kumshtaki kwa kuyafukua.
Kuibuka kwa mgogoro huo kumetokana na utata wa sehemu gani Mandela azikwe, wanafamilia wanasema akifa azikwe Qunu jirani na walikozikwa watoto wake, lakini Mandla alikuwa akilazimisha babu yake azikwe Mvezo ambako alikuwa amehamishia makaburi hayo kwa siri.
Jaji Pakade alitoa muda wa chini ya saa 24 mabaki hayo yawe yamefukuliwa na kurejeshwa kwenye ‘makazi’ yake ya awali. Aliambiwa kazi ya ufukuaji isizidi saa 9.00 alasiri ya jana mchana. Hukumu hiyo ilishuhudiwa na binti wa Mandela, Makaziwe Mandela, shangazi wa Makaziwe, Ndaba na mjomba wake Ndileka.
Wanafamilia walimtuhumu Mandla kwamba alidhamiria kulifanya eneo la Mvezo kuwa eneo la utalii kwa wageni kwenda kutembelea kaburi la Mandela kwa kuwa amejenga hoteli huko na kwamba makaburi hayo yangesaidia hoteli yake kupata wageni wengi wa mara kwa mara.
Kwa mujibu wa wanafamilia, Mandla amejenga hoteli yenye thamani ya Pauni za Uingereza 4 milioni.
CHANZO: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...