Sunday 26 January 2014

Wizara yakemea ukatili na mauaji ya wanawake Butiama, Mara

 JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA 

WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII  JINSIA NA WATOTO
Picture
Hivi karibuni kumekuwa na taarifa za kutisha katika Wilaya ya Butiama mkoa wa Mara ambapo imearifiwa baadhi ya wanawake kuuawa kikatili kwa kukatwa vichwa.

Sababu ambazo hazijathibitishwa zinaeleza kuwa chanzo cha mauaji hayo ni pamoja na imani za kishirikina, uchu wa kumiliki mali, kulipiza visasi na kuendekeza hulka ya ukatili kwa kudhani kuwa mhusika anapata heshima yoyote katika jamii.

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kuwepo kwa mauaji hayo ya 
kikatili na inawataka wananchi kutoa ushirikiano thabiti ili kuhakikisha kuwa matukio hayo ya  udhalimu YANAKOMA MARA MOJA.


Wizara inalaani vikali mauaji ya wanawake waliokatishwa maisha yao kutokana na kuuawa na watu wenye fikra potofu dhidi ya wanawake. Wizara inasisitiza kwamba  wanawake wanayo haki ya kuishi kama inavyosisitizwa katika Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977  inayotamka kuwa ‘Kila mtu anayo Haki ya Kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake kwa Mujibu wa Sheria.’

Wakati mwingine wanawake wamekuwa wakikandamizwa katika jamii kutokana na tofauti za kimaumbile na hivyo kusababisha ukatili au mauaji. Wizara inaitaka jamii itambue kuwa wanawake wana haki ya kuthaminiwa utu wao na kushiriki haki zote za msingi bila ubaguzi wowote ambao unaweza kuhatarisha haki zao ikiwemo haki ya kuishi ambayo ndio haki kuu kuliko haki zote.

Vitendo vya mauaji ya kikatili wanavyofanyiwa wanawake wa wilaya ya Butiama ni jambo ambalo linasababisha hofu kubwa miongoni mwa wanawake. Mauaji hayo yana wakosesha amani na utulivu na hivyo kuzorotesha ari yao katika shughuli za uzalishaji mali kwa wanawake wa  wilaya ya Butiama na Taifa kwa ujumla.  Mwananchi ambaye anawindwa kama mnyama kamwe hawezi akashiriki kikamilifu katika kujiletea maendeleo ya kiuchumi kwa kuogopa kuwa,  maisha yake yako hatarini.

Kwa kutambua hili Wizara inaagiza wadau wote kuiunga mkono Serikali katika kuhakikisha kwamba uhai wa wanawake wa Butiama na  kote nchini  unalindwa. Wananchi watambue kuwa tukio la mauaji dhidi ya mtu yeyote ni kinyume na haki za binadamu na ni kosa la jinai.

 Katika kipindi hiki cha majonzi, Wizara inatoa pole kwa familia ambazo zimeguswa na mauaji ya ndugu zao waliopoteza maisha,  Wizara inahimiza wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha watuhumiwa wa mauaji wanafichuliwa na kuchukuliwa hatua ili kukomesha tabia hiyo.

Mwisho, Wizara  inapenda kuikumbusha jamii kuwa, mauaji ya kikatili dhidi ya wanawake yanapingana na jitihada kubwa za Taifa katika kutekeleza  sheria za nchi na Mikataba ya Kimataifa na Kikanda kuhusu haki na usawa wa kijinsia,Aidha ni wajibu wetu sote kuhakikisha kuwa wananchi wote wa Tanzania wanaishi katika hali ya usalama, amani na utulivu.


Sophia M. Simba (Mb)
Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto
23 Januari, 2014


No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...