Saturday, 31 August 2013

IGP aibiwa upanga wa dhahabu


Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi Said Mwema 
Jeshi la Polisi limeingia katika kashfa nzito baada ya mkuu wake, Inspekta Jenerali Said Mwema, kuibiwa upanga wa dhahabu ambao ni mali ya Shirikisho la Wakuu wa Majeshi ya Polisi wa nchi za Kusini mwa Afrika (SARPCCO).
Upanga huo wenye uzito wa takriban kilo tatu na wenye thamani ya zaidi ya fedha za Tanzania Sh600 milioni, ni kielelezo kwa nchi inayokabidhiwa uongozi wa SARPCCO.
Mwaka jana Tanzania ilikuwa mwenyekiti wa SARPCCO, ambapo upanga huo ulikabidhiwa kwa IGP Mwema na Jenerali Magwashi Victoria ‘Riah’ Phiyega, ambaye ni Kamishna wa Taifa wa Polisi wa Afrika Kusini aliyekuwa amemaliza muda wake kwa wakati huo.
Hilo ni tukio la pili la wizi la mali zinazohusu ofisi ya IGP, ambapo mwaka jana ndani ya ofisi hiyo kuliibwa kompyuta ndogo (laptop), ikiwa na taarifa muhimu za kipolisi. Hadi sasa hakuna taarifa za kupatikana kwa kompyuta hiyo.

IGP Mwema alikabidhiwa upanga huo Septemba 5, 2012, katika mkutano saba wa SARPCCO uliofanyika Zanzibar na kuhudhuriwa na wakuu wa majeshi ya Polisi kutoka nchi 13, pamoja na mashirika ya kimataifa.
Upanga huo ambao unakwenda sambamba na bendera ya SARPCCO, ni moja ya vielelezo vya nchi iliyochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa shirikisho hilo, ambaye moja kwa moja anakuwa ni Mkuu wa Jeshi la Polisi katika nchi husika.
Kwa mujibu wa taratibu za SARPCCO, vielelezo hivyo hutakiwa kuwekwa ofisini kwa kiongozi husika, ikiwa ni alama ya kila mgeni atakayeingia ofisini hapo kutambua uwepo wa wadhifa huo wa kimataifa.
Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa IGP aligundua kutoweka kwa upanga huo wiki iliyopita, wakati akijiandaa kwenda kuukabidhi kwa mwenyekiti mpya wa SARPCCO, ambaye ni IGP wa Namibia.
Taarifa za ndani ya jeshi hilo zilibaini kuwa, IGP alilazimika kuondoka bila upanga huo alipokwenda Namibia wiki iliyopita kuhudhuria mkutano wa nane wa SARPCCO, uliofanyika Jumapili iliyopita mjini Windhoek.
Kwa mujibu wa uchunguzi, IGP Mwema alikabidhi upanga unaofanana na huo ambao siyo wa dhahabu, alioazimwa kutoka kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi la Namibia, Inspekta Jenerali, Luteni Jenerali Sebastian Ndeitunga, na kukabidhiwa kama ishara ya kukabidhiwa uenyekiti wa SARPCCO kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Uchunguzi ulibaini kuwa IGP Mwema alitoa ahadi ya kurejesha upanga halisi ndani ya kipindi cha mwezi mmoja, au Serikali ya Tanzania italazimika kutengeneza mwingine kulipa uliopotea.
Uchunguzi wa gazeti hili unaonyesha kuwa kashfa hiyo ametupiwa Mkuu wa Polisi Zanzibar, Kamishna Mussa Ali Mussa pamoja na dereva wake, ikidaiwa kuwa upanga huo baada ya kupokewa na IGP Mwema, Septemba mwaka jana uliwekwa kwenye gari la kamishna huyo.
Kamishna Mussa ndiye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano wa Saba, na pia ofisa mwenyeji kwa wajumbe wa mkutano huo uliofanyika Zanzibar.
Hata hivyo, taarifa zingine zilidai kuwa IGP Mwema naye analaumiwa kwa kutofuatilia kwa karibu zana za kazi, kwani baada ya kuupokea alitakiwa kuhakikisha unakuwepo ofisini kwake kama alama ya uenyekiti wake.
Gazeti hili lilipowasiliana kwa njia ya simu na Mkuu wa Polisi Zanzibar, Kamishna Mussa Ali Mussa kuhusu madai hayo alisema, kitara (upanga) hicho ni kweli kimepotea, lakini yeye hahusiki kwa kuwa kila kitu kina utaratibu wake.
“Ni kweli kitara kilikabidhiwa kwa afande IGP na mimi nilishuhudia kikikabidhiwa, na ni kweli kitara hakijulikani kiliko, lakini mimi sihusiki na kupotea kwake. Ni kweli mimi nilikuwa ofisa mwenyeji wa mkutano huo, lakini siku hiyo zilitolewa zawadi nyingi, watu walipewa mikoba, kwa hiyo mtu akipoteza mkoba wake niulizwe mimi?” alihoji Kamishna Mussa.
Alisema kila kitu kina utaratibu wake na kwamba taarifa kwamba yeye amehojiwa kutokana na upotevu wa kitara hicho au kuna kamati imeundwa, hazina ukweli.
“Sijawahi kuona kamati hiyo. Kamati hiyo kwanza imeundwa na nani na inatoka wapi? Hayo maneno yanatengenezwa na watu wa nje,” alisema Kamishna Mussa.
Alisema kinachofanyika hivi sasa ni kukitafuta ili kiweze kurejeshwa kunakohusika.
Taarifa zingine zilidai hata bendera ya mezani ya mwenyekiti wa SARPCCO, aliyokabidhiwa sambamba na upanga huo nayo kuna hatihati ilipotea.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso alipotakiwa kuzungumzia suala hilo alisema aulizwe kamishina wa polisi Zanzibar.
“Suala hilo muulize Kamishina wa Zanzibar ndiye anayejua,” alisema Senso.
Uchunguzi unaonyesha kuwa maofisa katika ofisi ya IGP na ile ya Kamishna wa Polisi Zanzibar, wamehojiwa akiwamo Kamishna Mussa, na kwamba upelelezi mkubwa umekuwa ukiendelea ndani ya jeshi hilo.
Hata hivyo, juhudi za gazeti hili za kutaka kufahamu uamuzi wa SARPCCO katika ofisi yake ya uratibu iliyopo kwenye ofisi za Makao Makuu ya Kanda ya Polisi wa Kimataifa (INTERPOL), Harare, Zimbabwe, hazikuzaa matunda baada ya baruapepe iliyotumwa kwa ofisa mratibu wa SARPCCO ambaye pia ni mkuu wa ofisi ya Kanda ya INTERPOL, C. Simfukwe kutopata majibu.
SARPCCO ilianzishwa mwaka 1995, Victoria Falls, Zimbabwe, lakini kisheria ilitambulika rasmi mwaka 2006 na lengo lake kuu ni kupambana na uhalifu wa kuvuka mipaka.
Uenyekiti wake ni mwaka mmoja, ambapo kwa sasa mwenyekiti ni Mkuu wa Jeshi la Polisi la Namibia Inspekta Jenerali, Luteni Jenerali Sebastian Ndeitunga, aliyepokea wadhifa huo kutoka kwa IGP Mwema.
CHANZO:MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...