Wednesday 18 September 2013

WAUNGANA KUMSHINIKIZA RAIS KUTOKUSAINI MSWADA

Mwenyekiti wa jukwaa hilo, Deus Kibamba 

Dar es Salaam. Jukwaa la Katiba Tanzania, limesema limeungana na vyama vikuu vya upinzani nchini ili kutoa elimu ya mchakato wa Katiba kwa Watanzania kupitia asasi za kiraia.
Pia, jukwaa hilo limeungana na vyama hivyo kumshinikiza Rais Kikwete asisaini Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Mpya uliopitishwa bungeni Septemba 6, mwaka huu.
Kauli ya kuungana na vyama hivyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa jukwaa hilo, Deus Kibamba baada ya kukutana na wenyeviti wa vyama hivyo vikuu vya upinzani ngazi ya taifa.
Tamko hilo lilitolewa jana muda mfupi baada ya kukamilika kwa kikao cha ndani kilichofanyika kati ya uongozi wa jukwaa na wenyeviti wa vyama hivyo.
Vyama vilivyofika kwenye kikao hicho kilichofanyika kwenye ofisi za Jukwaa la Katiba ni pamoja na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho kiliwakilishwa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, Chama cha Wananchi (Cuf), Profesa Ibrahim Lipumba na Chama cha NCCR- Mageuzi, James Mbatia.
Mkutano huo ambao unaelezwa kuwa ni wa kawaida wenye lengo la kushirikisha asasi za kiraia, ulifanyika kwa muda wa saa tano huku waandishi wa habari wakitakiwa kusubiri nje ya ofisi hizo ili kupewa taarifa ya mambo yaliyodaiwa yanaweza kusababisha kutengeneza Katiba ya upande mmoja.
Mkutano huo ambao ulianza saa 3 asubuhi, ulimalizika saa 8 mchana ambapo viongozi wa vyama vya upinzani na Jukwaa la Katiba walitoka kwa pamoja na kutoa matamko yao.
Akizungumza baada ya kutoka kwenye mkutano huo Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deus Kibamba alisema, lengo la kukutana na viongozi wa vyama hivyo ni kuhakikisha mchakato wa Katiba unafanyika kwa haki na Katiba itakayopatikana iwe ya Watanzania wote na siyo ya upande mmoja.
Naye msemaji wa viongozi hao,Profesa Ibrahim Lipumba alisema, ushirikiano huo umetokana na Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Mpya kupitishwa bungeni Septemba 6, mwaka huu, kwa nguvu na wabunge wa CCM.
Lipumba alibainisha kwamba kuanzia sasa watafanya mikutano na asasi za kiraia ili kuungana pamoja kutoa elimu na kushinikiza Rais Kikwete asisaini muswada huo.
Leo wanatarajia kukutana na wawakilishi wa vyama vya walemavu.
CHANZO: MWANACHI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...