Wednesday, 19 June 2013

Kupuuzwa elimu ya watu wazima kwachangia ongezeko la mbumbumbu



Sanjito Msafiri, Mwananchi

Sababu zinazochangia hali hiyo ni nyingi, ikiwamo ya chombo kinachohusika na Elimu ya Watu Wazima kukosa fedha.
Kwa hakika hali siyo nzuri, kwani katika siku za karibuni tumeshuhudia pia maelfu ya wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi, nao wakitajwa kuwa miongoni mwa wananchi wasiojua kusoma na kuandika.
Ndiyo tunaweza kusema miaka saba au zaidi ya kuwa shule imeshindwa kuwasaidia kupata stadi hizo muhimu kwa maisha ya mwanadamu.
Elimu ya Watu Wazima
Utafiti uliofanywa na Shirika la Elimu Kibaha (KEC) katika wilaya mbalimbali za Mkoa wa Pwani, unaonyesha licha ya kuwapo kwa vituo vya elimu ya watu wazima, shughuli katika vituo hivyo zimedorora, tofauti na ilivyokuwa miaka ya 1970 ambapo vituo hivyo vilikuwa chachu ya kuwasaidia wananchi kuondokana na umbumbumbu.

“Tumeweza kutafiti kwa kina juu ya suala la elimu ya watu wazima wilayani Kibaha. Ukweli ni kwamba hali ni mbaya sana, kwani tumebaini kuwa kati ya watu wazima kumi hasa wa vijijini watatu hawajui kusoma na kuandika,’’ anasema Msaidizi wa Mkuu wa Idara ya Utafiti wa shirika hilo, Anne Kuoko.
Anaongeza kuwa pamoja na kuwepo kwa hali hiyo inayowakumba watu wazima na hata wahitimu wa shule za msingi, inasikitisha kuwa hakuna mikakati ya kuwasaidia watu hao na hata kuzuia hali hiyo kwa vizazi vipya.
Kwa mujibu wa utafiti, mpaka sasa hakujawa na bajeti maalumu kugharimia mafunzo ya elimu kwa watu wazima. Walimu nao wanalalamika kutopewa stahili zao mbalimbali kwa miaka sasa.
”Tumeweza kuona kuwa wapo walimu waliojitolea kwa kipindi kirefu bila kulipwa. Taarifa tulizonazo walitakiwa walipwe kiasi cha Sh20, 000 kwa mwezi, lakini hata hicho kidogo hawakulipwa, hivyo wakaacha kufundisha, jambo linalozorotesha vituo vya elimu ya watu wazima.
Kauli ya Kuoko inathibitishwa na Zawadi Rashid, mwalimu wa elimu ya watu wazima katika Kijiji cha Lukenge anayesema tangu mwaka 2009 malipo ya kazi yake kutoka halmashauri yamekuwa yakipigwa danadana.
“Mimi sina elimu ya ualimu, nimesoma mpaka kidato cha nne tu, ila kutokana na wito nilionao nilipendezewa kufanya kazi ya ualimu, hususan kufundisha watu wazima nikijua wazi kuwa kadri ninavyoendelea baadaye hata Serikali inaweza ikaniendeleza, lakini naelekea kukata tamaa kutokana na malipo madogo na hata hayo madogo hayapatikani”, anasema.
Anatoa mfano wa mwaka 2012 ambao hakulipwa hata senti moja kati ya Sh20,000 alizoahidiwa kulipwa kila mwezi.
Hali halisi
Mratibu wa Elimu kata ya Magindu, William Mbagi anasema katika kata yake idadi ya watu wazima wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu inafikia watu 785, huku asilimia kubwa ikiwa ni wafugaji.
“Vituo vya Elimu ya Watu Wazima ndani ya kata ya Magindu vipo tu kimatamshi, lakini havifanyi kazi kama inavyostahili kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kubwa ya ukosefu wa fedha. Uongozi wa halmashauri hautoi pesa kwa ajili ya kazi hiyo, fedha hizi zinatakiwa zitumike kununua vifaa vya kufundishia na malipo kwa walimu,” anabainisha.
Kauli ya Serikali
Ofisa Elimu ya Watu Wazima katika Wilaya ya Kibaha, Mwebesa Muchunguzi anakiri na kuzorota kwa vituo vya elimu ya watu wazima, na kubainisha mambo mbalimbali yanayosababisha hali hiyo.
Sababu kubwa anayoitaja ni chombo kinachosimamia elimu hiyo kutopewa bajeti ya kutosha kutoka wizarani. Hivi sasa anasema kitengo hicho husubiri kupewa gawio dogo kutoka kwenye idara ya Elimu ya Msingi.
“Hivi sasa kitengo cha Elimu ya Watu Wazima hakipo kama moja ya idara kama zilivyo idara zingine, bali iko chini ya Idara ya Elimu ya Msingi. Hivyo ili kiweze kupata pesa ni lazima kwanza ifikiriwe na uongozi wa elimu ya msingi,’’ anasema na kuongeza:
“ Awali elimu ya watu wazima ilikuwa idara inayojitegemea kama zilivyo zingine, lakini Serikali ilileta mabadiliko kwa kuihamishia kama kitengo ndani ya Idara ya Elimu ya Msingi, hali hiyo ilipunguza utendaji kwa kiasi kikubwa.’’
Ushauri kwa Serikali
Mmoja wa wanafunzi wanaopata mafunzo katika Kituo cha Elimu ya Watu Wazima cha Kijiji cha Lukenge, Lusiana Kauzeni, anashauri mafunzo ya elimu ya watu wazima yaende sambamba na mambo muhimu yanayoizunguka jamii ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya ufugaji wa kisasa na kilimo bora.
“Ni vyema uongozi wa Halmashauri ukaliangalia hilo kwa ukaribu kuleta wataalamu wa masuala ya kilimo bora, na hata kutoa mikopo inayolenga kuboresha shughuli zetu, ili kumudu changamoto za maisha ya kila siku,’’ anasema.

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...