Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MWILI wa msanii Albert Mangwea, umezuiwa na Watanzania wanaoishi nchini Afrika Kusini wakiwa na lengo la kushiriki kumuaga, hivyo kulazimisha kupanguliwa kumleta nchini kesho (leo) na badala yake marehemu atawasili kesho Jumapili.
Marehemu Ngwea, enzi za uhai wake
Aidha, wadau mbalimbali wameendelea kushiriki kuchangia msiba wa marehemu Ngwea, wakiwamo Kampuni ya Clouds Media Group, sambamba na Studio za Bongo Records chini ya P-Funk Majani na Push Mobile ambao wote kwa pamoja wamechangia Milioni tano kila mmoja.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Addo Novemba, alisema kuwa wamepata taarifa kutoka Afrika Kusini kuwa mwili huo sasa utawasili kesho Jumapili ya Juni mbili badala ya Jumamosi ya Juni Mosi kama ilivyotangazwa awali.
Alisema kuwa Watanzania wanaoishi nchini Afrika Kusini nao wametaka kuweka utaratibu wa kuuaga mwili huo kabla ya kuletwa Tanzania, hivyo imelazisha kupangua ratiba ya kuwasili kwa mwili huo.
Naye Mkurugenzi wa Utafiti na Matukio wa Clouds Media Group, Ruge Mutaba, alisema kuwa wameamua kushirikiana kwa karibu na wadau wote katika kufanikisha kuuleta mwili huo hapa nchini.
Akizungumza na Mtanzania jana jijini Dar es Salaam, Ruge alisema Watanzania wote wameguswa na msiba wa msanii Mangwea kutokana na mchango wake kwenye sanaa.
Alisema kuwa kinachoangaliwa kwa sasa ni kukaa pamoja na wadau kwa ajili ya kufanikisha kuletwa kwa mwili wa marehemu Ngwea aliyefia nchini Afrika Kusini na kuhuzunisha wadau wengi.
“Clouds tumeshirikiana na wadau wote hasa wa Kamati ya Mazishi ambayo ipo chini ya mwenyekiti wake, Kenneth Mangwea ambaye ni kaka wa marehemu kwa ajili ya kufanikisha suala hilo,” alisemaa.
BASATA yamlilia Mangwea
Nalo Baraza la Sanaa la Taifa limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa msanii Mangwea, aliyefia nchini Afrika Kusini kwenye shughuli zake za kimuziki.
“Baraza limestushwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa ya kifo hiki cha Ngwea ambaye mchango wake unahitajika sana katika tasnia ya sanaa, pengo aliloliacha ni kubwa kwani ubunifu wake bado unahitajika katika tasnia hii,” alisema taarifa hiyo iliyotumwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Lebejo.”
Alisema Baraza linatoa pole kwa familia ya marehemu na wasanii wote nchini, aidha linawatakia moyo wa subira katika wakati huu wa majonzi ya kuondokewa na mpendwa wetu.
Ngwea atakumbukwa kwa mchango wake katika sanaa ya muziki wa kizazi kipya, akishiriki kuandaa nyimbo zilizopokelewa kwa shangwe, ukiwapo wimbo wa Gheto Langu.
No comments:
Post a Comment