Saturday 13 July 2013

Dawa ya sangoma yawageukia wanafamilia, wapata kichaa



Mwalimu aliyetumia uchawi kuwaroga wezi, amejikuta akiwaroga shemeji zake waliopata uchizi
Butiama. Ilikuwa kama simulizi ya kwenye filamu, baada ya mganga wa kienyeji aliyeletwa toka Kenya kuja kuwaroga wezi walioiba nyumbani kwa Mwalimu mstaafu, Raphael Omwando (60), baada ya dawa yake kuwatia uchizi ndugu wa mke mkubwa wa aliyeibiwa.
Mwalimu Omwando ambaye ana wake wawili alivamiwa na wezi waliomwibia pikipiki na mali nyingine, ikiwemo kumjeruhi yeye (Omwando) na mkewe mkubwa. Mke mdogo aliyemuoa hivi karibuni anaishi kwenye nyumba nyingine na hakuweza kuvamiwa na wezi hao, lakini mke mkubwa alipigwa hadi kulazimika kupewa matibabu hospitali.

Watu walio karibu na familia hiyo walisema kutokuelewana kati ya mke mkubwa na mdogo, kulimfanya mke mkubwa aliyejeruhiwa na majambazi kumtuhumu mke mdogo kwamba alishirikiana na majambazi hao.
Filamu hiyo ya familia ilianza kwa ndugu wa mume (Omwando) wanaoishi Kenya, kuleta sangoma kwa ajili ya kubaini wezi waliomwibia ndugu yao.
“Sijui nimefikaje hapa hospitali…maana kumbukumbu zinaishia pale nilipolazimishwa kunywa dawa na mganga wa kienyeji (Sangoma) anayedaiwa kutokea nchini Kenya …ili wezi wa pikipiki na vifaa vya mwalimu mstaafu virudishwe,” hiyo ni kauli ya mmoja kati ya watu wanne waliolazwa hospitali kwa madai ya kurukwa na akili.
Wagonjwa hao ni vijana wanne wa Kijiji cha Kirumi  Kata ya Bukanga, Tarafa ya Makongoro, Wilaya ya Butiama, mkoani Mara waliolazwa hospitali ya Mkoa wa Mara baada ya kunywa dawa hiyo na kupoteza fahamu huku wakionekana kama mazuzu (Mazombi).
Waathirika
Matiko Joseph (25) anasema yeye alilazimishwa kunywa dawa nyingi pamoja na makapi yake,” …Baada ya kumtajia mganga hivyo akasema ninyi kunyweni nyingi…dawa ilikuwa na ukakasi ilinikereketa sana. Baada ya kunywa niliondoka lakini baadaye hali ikabadilika sana,” anasema na kuongeza,
“Nilishtukia niko hospitali tayari ikiwa ni siku ya pili …Nikisimuliwa ilivyokuwa nazidi kushangaa…huyo mganga alilenga kutuua kabisa….maana wakati anatoa dawa alisema atakayepata madhara hatapona hata akipelekwa wapi mpaka vitu virudi ama fedha…akaondoka kwenda Kenya na hakuacha simu wala jina lake kujulikana,” anasema Joseph huku akipumua kwa harakaharaka.
Tura Joseph (30) anasema wengine walikunywa kidogo lakini wao wana ndugu walilazimishwa kunywa zaidi kwa kile kinachodaiwa kuwa walihisiwa kula njama za kumdhuru shemeji yao, na ndiyo walidhurika zaidi.
Anasema baada ya kunywa alihisi kitu kinamkaba shingoni na kuishiwa nguvu, akawa hoi na kuanza kuongea maneno yaliyowatia shaka, ndugu wakawabeba kwa bajaji hadi hospitali.
Boniphace Joseph (20)huku akisitasita, anasema ana habari kabla ya kunywa dawa lakini baada ya kunywa hakumbuki kilichoendelea mpaka alipopata fahamu na kuona watu wanamshangaa naye akiwashangaa.
Msira Magesa (17) anasema yeye baada ya kunywa alitoka kwenda kwenye shughuli zake, ghafla akazidiwa na kupewa dawa ya kutuliza maumivu aina ya panadol hali ikazidi kuwa mbaya na kufikishwa hospitali kwa matibabu
Hali ilivyokuwa
Julai 5, majira ya saa 5:15 usiku mwaka huu, Mwalimu mstaafu, Raphael Omwando (60) alivamiwa na watu wanaodhaniwa kuwa majambazi, wakamkata yeye, mkewe akapigwa na majambazi hao na baada ya kipigo waliiba pikipiki, mabegi ya nguo, sola, sanduku dogo la kuhifadhia nyaraka, simu ya mkononi na vitu vingine.
Omwando kutokana na majeraha aliyoyapata akapelekwa hospitali ya mkoa alikolazwa kwa matibabu, lakini ndugu zake wanaoishi Shirati na wale wanaoishi nchini Kenya baada ya kupata taarifa waliamua kuchukua mganga wa kienyeji kutoka Kenya, ambaye aliwahakikishia kuwa wahusika baada ya saa 3 watarudisha vitu walivyoviiba wakiwa wamejitwisha na pikipiki wakiwa wanaisukuma.
Mganga huyo alieleza dalili za awali zitakazowapata wezi hao kuwa ni kuchanganyikiwa, wengine watakuwa wanakula nyasi kama ng’ombe. Mganga huyo alitoa tangazo kwamba  Julai 9 majira ya saa 9:00 alasiri wanakijiji wote wajitokeze kunywa dawa hiyo ili kuwapata wahusika.
Vituko vyao walikojoleana, kutapikiana
Mmoja wa wauguzi katika hospitali hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe anasema, walipofikishwa hapo aliogopa,“ walikuwa wanakojoleana midomoni, wanatapikiana, huku wakiongea lugha za ajabuajabu, tuliogopa maana ni tukio la kwanza kutokea,” anasema.
Anasema walipewa dawa za kuwafanya walale lakini wakaonekana wanaendelea kuongea wengine kukimbia huku wakidai kuna watu wanataka kuwaua, lakini sasa wametulia wanaongea wenyewe.
Shuhuda mwingine Isa Magesa anayemuuguza ndugu yake anasema Matiko, mmoja wa waathirika hao alikuwa akikimbia kasi kwenda nje huku akipiga kelele, “Nililazimika kutoa msaada, nilipomkamata alionekana ana nguvu sana huku akisema…acheni kuniua…hao wanakuja kuniua…nisaidie …wabaya hao, huku akionyesha kwa vidole lakini wao hawawaoni,” anasema.
Mganga Mfawidhi.
Dk Iragi Ngerageza, Mganga Mfawidhi Hospitali ya Mkoa, anasema vijana hao walifikishwa hapo wakiwa hawajitambui huku ikidaiwa kuwa walipewadawa na mganga wa kienyeji na kuwapokea wakiwa na hali mbaya  na kuwa hali hiyo bado wanaendelea kuichunguza.
“Inakuwa vigumu kujua madhara ya hiyo dawa, kama tungeweza kuipata na kupeleka kwa mkemia ingetoa majibu, lakini kwa sasa sisi tunaendeleakuwatibu…lakini ni hatari maana kama walikunywa wakafikia hatua hiyo lazima kuna kitu, ikipatikana itatusaidia,” anasema.
Mke wake akamatwa.
Pilly Esther mke mdogo wa Mwalimu Omwando amekamatwa kwa kuhusishwa na tukio hilo,  kusaidia kumpata mganga aliyehusika na anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Butiama.
Hata hivyo akizungumzia tukio hilo anasema, wakati mume wake anavamia yeye alikuwa kwake na alisikia kelele za mbwa, lakini hakuelewa kilichotokea mwishoni akapigiwa simu na mke mkubwa kuwa wamevamiwa na kuumizwa. “Ndugu wa mume wangu akiwemo mke mkubwa ambaye ni Mjaluo wa kwao walinituhumu mimi kuwa ndugu zangu ndiyo wameiba mali kwa kuwanimeolewa hivi karibuni..au mpenzi wangu wa zamani ndiye amehusika, nilipokataa wakasema wanakuja na mganga kutoka Kenya ambayeanatoa majibu haraka,” anasema.
Anasema mganga aliomba mtendaji kualika wananchi wote lakini akakataa wakafika kama 40 wakiwemo kinamama, lakini kabla ya kutoa dawa akawaanasema wahusika ni kama anawaona hapo anawaomba wasinywe dawa, ajabuwaliopata madhara ni ndugu wa mke mkubwa.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...