Wednesday 31 July 2013

`MEMORY CARD`YALETA HOFU WAKAZI BUTIAMA


Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Angelina Mabula


Aina mpya ya ukatili wa kijinsia maarufu kama `memory card' unaohusisha wanawake kuuawa na kunyofolewa sehemu za siri, imezua hofu miongoni mwa wakazi wa wilaya Butiama mkoani Mara.

Kati ya kipindi cha Desemba mwaka jana na Julai, mwaka huu, jumla ya wanawake 14 wanasadikiwa kufanyiwa ukatili huo.

Ukatili huo umebainishwa na wanawake mbalimbali walipokuwa wakizungumza kwenye mdahalo wa kupinga ukatili wa wanawake na watoto wa kike uliofanyika katika kijiji cha Bisumwa, Wilaya ya Butiama mkoani Mara ambapo walisema mauaji hayo yanaongozwa na kundi la watu wanaojiita makhirikhiri.




Mdahalo huo ambao uliandaliwa na shirika la kutetea haki za wanawake na watoto wa kike la Kivulini kupitia kampeni yake ya Tunaweza, wanawake hao walisema ukatili huo umekuwa ukifanywa na watu walio karibu na familia zao.

Kwa mujibu wa wanawake hao, katika kutekeleza ukatili huo, kundi hilo la makhirikhiri huwavizia wanawake wanapokwenda kuteka maji au wanapokuwa shambani na kuwavamia, kuwakata shingo na kisha kunyofoa kiungo katika sehemu za siri.

Mmoja wa wanawake hao, Maria Michael, alisema wauaji hao huchukua kiungo hicho pamoja na damu waliyokinga kutoka shingoni na kupeleka kwa waganga wa kienyeji kwa ajili ya kutengenezewa dawa ya kupata utajiri.

“Mauaji ya wanawake na kukatwa sehemu zao za siri pamoja na kichwa yamerudisha nyuma uchumi kutokana na wanawake hivi sasa kuhofia kutoka majumbani mwao kwenda kushiriki kazi za kiuchumi,” alisema.

Aliongeza kwamba huo ni ukatili ambao unapaswa kukomeshwa mara moja kwani hakuna uthibitisho wowote unaoonyesha kuwa kiungo hicho cha kike kinaleta utajiri.

Kwa mujibu wa Maria, vitendo hivyo vya ukatili vimesababisha wanawake kuungana katika makundi wanapokwenda kuteka maji au katika shughuli nyingine za kiuchumi ili kuepuka kuvamiwa na kundi hilo la makhirikhiri.

Akitoa mapendekezo ya nini kifanyike ili kukomesha mauaji hayo, Elizabeth Samson, aliwataka viongozi wa serikali za mitaa kuacha urasimu katika kushughulikia keso za ukatili wa kijinsia.

Aliongeza kuwa polisi pia wamekuwa wakichelewa kushughulikia kesi za ukatili wa kijinsia na baadhi yao hupokea rushwa na kuwaachia watuhumiwa.

Akielezea hatua zilizochukuliwa ofisa wa sera na utetezi katika shirika la Kivulini, Khadija Liganga, alisema mauaji hayo hufanyika kwa siri na polisi walithibitisha kuyafuatilia kwa karibu ili kubaini maeneo yanayoongoza.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Angelina Mabula, alisema hivi sasa matukio hayo yamedhibitiwa na serikali kwa kupitia kamati zake za ulinzi na usalama za wilaya na mkoa pamoja na kuimarisha ulinzi shirikishi.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...