Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi
Bagamoyo. Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi amezindua maabara ya kisasa na kusema magonjwa mapya ya mlipuko ambayo yamekuwa yakitishia maisha ya wananchi sasa yatadhibitiwa.
Mwinyi alisema hayo jana mjini hapa, baada ya kuzindua maabara ya kisasa ya kutambua vimelea vya magonjwa ya milipuko inayoitwa Bio Safety level 3.
Dk Mwinyi alisema vimelea vya magonjwa ya milipuko yakiwamo dengu, ebola na Rift Valley sasa yatakuwa yakipimwa katika maabara hiyo ambayo ipo Katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo.
“Kuanzia sasa hata kama litajitokeza gonjwa jipya tutakuwa na uwezo wa kupima wenyewe kwenye maabara hii badala ya kupeleka Afrika Kusini,” alisema Dk Mwinyi katika hotuba iliyosomwa na Naibu wake, Seif Rashid.
“Tunaishukuru Serikali ya Italia kwa msaada huu na kwamba utatumika kuboresha sekta ya afya nchini,” alisema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Afya ya Ifakara (IHI), Dk Salim Abdulla alisema maabara hiyo ya ngazi ya tatu ni ukombozi katika sekta ya afya na kwamba taasisi hiyo ndiyo itakayoiendesha maabara hiyo.
“Hatufahamu kesho utajitokeza ugonjwa gani lakini kwa kupata maabara hii tunaweza kukabiliana na magonjwa yoyote ya milipuko ambayo husababishwa na virusi na bakteria,” alisema.
Alisema ni nchi chache barani Afrika zenye maabara hiyo ya daraja la tatu na kwamba taasisi yake itahakikisha inafanya kazi za kitafiti ili kuleta mapinduzi katika sekta ya afya.
Kwa upande wake,Balozi wa Italia nchini Tanzania, Pierluigi Velard alisema nchi yake itatoa wataalamu ambao watatoa mafunzo kwa watafiti wa IHI kwa ajili ya kutumia maabara hiyo.
Alisema pia itaendelea kuisaidia Tanzania hasa katika sekta ya afya ili kulinda maisha ya wananchi.
Balozi huyo alisema kutokana na mwingiliano wa watu kutoka katika maeneo mbalimbali, maabara ya daraja la tatu ina umuhimu mkubwa katika nchi yoyote duniani.
“Tumeona zawadi kubwa ambayo Watanzania wanastahili ni kuwapa vifaa vya maabara ambavyo wananchi wote watanufaika navyo ili kulinda afya zao na tutaendelea kuwasaidia,” alisema Velard.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi alisema ni bahati kubwa kwa wilaya hiyo kupata maabara ambayo itatumiwa katika mikoa yote na nchi za jirani.
“Tutatoa ushirikiano na IHI na wafadhili kuhakikisha kwamba maabara hii inafanya kazi iliyokusudiwa kwa masilahi ya taifa,” alisema Kipozi.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment