Judith na David Tebbut walikuwa likizo nchini Kenya wakati waliposhambuliwa na kundi la watu wenye silaha. David aliuawa na Judith alichukuliwa hadi Somalia ambako alishikiliwa mateka kwa miezi sita.
Ni baada ya mwaka mmoja tangu aachiliwe huru, anasimulia dhamira ya ajabu ya kusalimika mikononi mwa watekaji wake.
Alidhamiria kusalimika, na hilo ndilo lililomsukuma kuandika kitabu kuhusu maisha yake akiwa mateka, Safari Ndefu Nyumbani, na pia kuzungumza na BBC katika moja ya mahojiano nadra kuhusu mkasa huo.Unapokutana na Judith Tebbut – yeye anapenda kuitwa Jude – na utajiuliza kwanini, baada ya miezi sita ndani ya chumba kichafu, kilichojaa vitu, akila chakula cha mgao cha viazi na mchele, akidhihakiwa, kudhalilishwa na mara kwa mara akitishiwa kuuawa, anaonekana hakuumizwa na mvumilivu.
Jude, anayetokea mtaa wa Bishop’s Stortford, Hertfordshire, anataka kuwaonesha na kuwa mfano kwa wengine walioshikiliwa mateka kwa madai ya watekaji kulipwa fedha nyingi.
“Huo ndio ujumbe,” anasema, “Ni ujumbe kwa mateka yeyote duniani, hasa waliopo Somalia, kwa sababu nafahamu mazingira wanayopitia, wasikate tama. Matumaini ndiyo mwokozi wangu.”
Siku za kutisha zilianza kwa kile ambacho, mara ya kwanza, kilionekana kama mapumziko ya kukumbukwa na mumewe waliyedumu pamoja kwa zaidi ya miaka 30, David. Ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Fedha kwa kampuni ya mchapishaji inayojulikana kama Faber and Faber. Walikutana Afrika, na David alipapenda huko.
Mnamo Septemba 2011, baada ya kutembelea mbuga ya wanyama ya Masai Mara kwa wiki moja, waliwasili kwenye ufukwe wa bahari wa Kiwayu – katika kisiwa cha Lamu nchini Kenya, kilichopo kilomita 40 kutoka pwani ya Somalia.Jude hakuwa na furaha tangu mwanzo.
“Nilihisi jambo baya,” anasema. Palikuwa kimya sana. Nilipoambiwa hapakuwa na mtu isipokuwa sisi, nilihisi ajabu kabisa.“Chumba chetu kilikuwa mbali na majengo mengine. Lakini David akasema”Usihofu, hii itakuwa sawa na safari ya Robinson Crusoe.”
Lakini ule usiku wa kwanza, alishtushwa na sauti ya David akihangaika na mtu gizani. Na mara akapigwa na mtutu wa bunduki na kuburuzwa hadi ufukweni.
Akiwa peku amevalia nguo ya kulalia, alipelekwa hadi kwenye boti, na kusukumiwa kwenye mapipa ya mafuta, na kisha boti hiyo kuondoka kwa kasi.
“Nilijigonga kichwa na kuchana sehemu ya jicho langu. Akili yangu ilikuwa ikienda mbio…. nikijaribu kuvuta hisia kuhusu tukio hili la kuogofya,” anasema.
Ilikuwa wazi, sasa, licha ya matukio yale ya kushtua, Jude alikuwa akipiga hesabu namna ya kudhibiti hali ile. Kwa mfano alitoa tabasamu kwa watekaji wake kama njia ya kujenga urafiki nao.
Jude, ambaye amefanya kazi kama mtaalam wa magonjwa ya akili , aliamini kwamba, anahitaji kujihusisha na maharamia hao kwa kiasi kikubwa kadri inavyowezekana.
Wakati siku zake za kutekwa zikifikia wiki mbili, alijifunza kidogo lugha ya Kisomali ili aweze kusema “tafadhali” na “ahsante” na kuwafanya watekaji wake wamuone kuwa ni binadamu – si kama bidhaa inayosubiri kuuzwa.
“Ingawa niliwachukia watu hawa, nilifahamu kwamba nitakuwa nao kwa siku nyingi zijazo, nilihitaji kujaribu kujenga mahusiano nao, kujenga muingiliano.”
Nilijiona mshindi katika baadhi ya mambo madogo, kama kukataa kuvaa nguo rasmi za Kisomali.
“Walijaribu kila mara kunilazimisha nivae vazi la hijab, jilbab, na kila kitu. Na nilipovaa, mmoja wa maharamia alitamka “Aaah mrembo! Mwanamke mrembo wa Kisomali!”.
“Mimi sio mwanamke wa Kisomali, na sitaki kuwa mwanamke wa Kisomali – hivyo niliivua mara moja. Nikahisi kukosa hewa kufunikwa na nguo zote hizo, na pia mgeni.
“Hilo ni muhimu sana, kutopoteza utambulisho wako. Hata kama ni wakatili kiasi gani kwako, wakikudhalilisha, lazima ujikumbushe binafsi wewe ni nani kila mara. Mimi bado ni Jude, na ninataka kutoka mahali hapa nikiwa Jude. Nataka kutafuta maisha tena ya Jude.”
Akiwa amefungiwa ndani ya chumba chenye joto kali na kichafu, Jude alidhamiria kujiweka katika afya njema hivyo alitengeneza ratiba ya mazoezi – ya kutembea kwa saa moja kila siku.
Aliendelea na ratiba yake ya mazoezi wakati akiwa na nguvu za kutosha, lakini lishe duni ilimfanya adhoofike hadi kufikia mwisho wa kifungo chake.
Mazungumzo kuhusu kuachiliwa kwake yalianza siku chache mara baada ya kuwasili katika kijiji ambacho alifungwa. Baada ya wiki chache, mwanae wa kiume, Ollie, aliweza kuwasiliana naye kupitia simu ya maharamia.
“Nilimwambia Ollie ’Baba hajambo? Baba anachukuliaje suala hili?”.Jude alijipa matumaini kwamba, David alikuwa hai na alikuwa akishughulikia kuhusu kuachiliwa kwake.
“Lakini Ollie akasema, ‘Kuna jambo lazima nikuambie kuhusu baba. Hakupona majeraha yake…’ nikasema, ‘Nini unajaribu kuniambia, unaniambia baba amefariki?’ Ndipo nikasikia sauti ya haramia mmoja: ‘Dakika tatu za maongezi zimekwisha.’
“Maharamia wote walikuwa ndani ya chumba. Nikawaangalia wote na kusema, ‘ Mmemuua mume wangu!’
“Mmoja baada ya mwingine waliondoka nikabaki na kiongozi wao, nikasema ’ulikuwa wewe. Ulimuua mume wangu!’ Nilidhani nitamtazama usoni hadi ageuke upande mwingine, nikahisi chuki ya ajabu.”
Katika kipindi chote alichoshikiliwa, alijaribu kukusanya ushahidi kuhusu watekaji wake na kutengeneza maelezo ya kina kuwahusu na kujaribu kukusanya vinasaba waliposhika tochi yake, ama kitabu chake – akitumai kwamba, siku moja watakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Lakini anasema hataki watekaji nyara hao wauawe. Na pia hataki agubikwe na mawazo ya kulipiza kisasi. “Sitaki watu hao wawe na nguvu hiyo juu yangu. Wanakua mawazoni mwangu pale tu mimi ninapotaka.”
Baada ya wiki kadhaa, maharamia hao walimruhusu Jude kusikiliza radio, naye akaisikiliza BBC ikiwemo baadhi ya vipindi vinavyorushwa kutoka jamhuri iliyojitenga ya Somaliland.
“Nilikuwa nimekaa kwenye chumba chenye giza nene nikikusikiliza. Huwezi kutambua jambo hilo lilimaanisha nini kwangu, kweli huwezi kutambua.”
Na Jude ana ujumbe kwa wengine wanaoshikiliwa mateka nchini Somalia na kwingineko duniani. “Nataka niwaambie watu ‘Msikate tamaa, hamjasahaulika.’
CHANZO BBC
No comments:
Post a Comment