Sunday 28 July 2013

Tanesco yaongeza vituo vya kusambaza umeme Dar



Shirika la Umeme (Tanesco) limeanza kujenga vituo vidogo vya kusambaza umeme jijini Dar es Salaam ili kuongeza nguvu.
Katika hatua nyingine shirika hilo limesema kuwa asilimia 60 ya mapato yake yanatoka kwenye viwanda na kuahidi kuboresha umeme wa viwandani ili kuongeza tija na mapato yake.
Hayo yalisemwa jana jijini na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba, wakati alipokutana na wanachama wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI) kwa ajili ya kuangalia jinsi ya kutatua changamoto zinazowakabili katika nishati ya umeme ili kuongeza ufanisi kwenye viwanda.
Alisema mchakato wa kusambaza umeme jijini ujenzi umeanza katika vituo vitano kwenye maeneo ya Kinyerezi, Mbagala, Gongo la Mboto, Katikati ya jiji na Kurasini.


Mramba alisema vituo hivyo vipya vitafanya kazi kwa kushirikiana na vya awali ambavyo ni cha Ubungo, Tegeta, Kipawa, Ilala na Makumbusho ili kuongeza ufanisi katika kusambaza umeme.
Alisema Tanesco iliamua kukutana na wanachama wa CTI kwa ajili ya kujadiliana jinsi ya kuzitatua changamoto zinazowakabili katika kuwaboreshea uzalishaji wao.
Mramba alisema kwa sasa wamejitahidi kutatua tatizo la umeme kwa kiasi kikubwa na kwamba ifikapo Desemba mwaka huu patakuwa na nishati ya uhakika.
Hata hivyo, Mramba alisema changamoto kubwa wanayokutana nayo wateja inasababishwa na miti iliyopo kandokando ya waya za umeme.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CTI, Felix Mosha, alisema kwa sasa linachangia pato la taifa kwa asilimia tisa lakini malengo ya melenia yanawataka ifikapo 2015 kuchangia kufikia asilimia 15.
Alisema endapo Tanesco itawahakikishia kuwapatia umeme wa uhakika watafikia malengo hayo.
Mosha alisema kwa sasa sekta ya viwanda inachangia kwa asilimia kubwa katika kuimarisha uchumi wa nchi na sio kilimo tena.
Alisema mategemeo yao ni kuimarisha uchumi zaidi wenye manufaa kwa Watanzania.
Hata hivyo, Mosha alisema CTI imefurahishwa na mabadiliko ya umeme yaliyofanywa na Tanesco kwani kuwepo na nishati ya uhakika inasaidia vifaa vyao kutokuharibika.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...