Sunday 14 July 2013

URAIA WA NCHI MBILI UMEKWAMA?



Waswahili wanasema, ‘mwenye macho haambiwi tazama.’ Labda ilikuwa ni kwa makusudi, Rais Jakaya Kikwete, alipofanya mzaha wa aina yake katika hotuba ya kufungua mkutano wa ‘Smart Partnership’ hivi karibuni.
Mjadala wa wazi wa kuendeleza sayansi na teknolojia Afrika na kwingineko. Kwa mantiki ya mazungumzo hayo, ilikuwa ni nafasi muhimu kwake kutoa ya moyoni.
Moja ya sababu ikiwa ni kwamba muda wake wa utawala unaanza kufikia tamati kwa hatua, anaanza kuhisi kuwa yapo maeneo ambayo hataweza kubadili yale aliyoyakuta, licha ya kuwa na hamasa ya kufanya hivyo wakati akiingia madarakani.
Katika ‘mzaha’ huo wa kidiplomasia, Rais Kikwete alikuwa akielezea umuhimu wa kutumia hazina ya wataalamu kutoka nchi za Afrika waliopo ng’ambo, katika kufikia ngazi ya ziada ya sayansi na tekinolojia nchini.
Alisema suala la uraia wa nchi mbili lisipoibuliwa na kujadiliwa, moja ya hisia za karibu zaidi ilikuwa ni hoja kuwa waliondoka wenyewe, hivyo hakuna haja ya kuwahangaikia, halafu madai kuwa wanataka kufaidi huku na huku.
Yaani moyo wao hauko katika nchi walikotoka, kwani hawawezi kuuachia uraia wa nchi walikokwenda. Ni ‘hukumu’ ya kikereketwa, uzalendo ambao Rais Kikwete alionyesha kutoridhika nao.

Alichoainisha vile vile katika maelezo yake, hata ingekuwa ni kwa kutumia `mzaha’ huo, ni kuwa yeye binafsi hana la kufanya kuhusu uelekeo huo, ambao hadi kumlazimisha kuuzungumzia hadharani katika kadamnasi ya kimataifa ni kwa sababu umekuwa ni mzigo kwake.
Ni sehemu ya lawama nyingi ambazo zinaelekezwa kwake kama kiongozi, kuwa ameshindwa kupiga hatua katika suala hilo au lile, kile baadhi ya wakinzani wanachosema ni kufanya maamuzi magumu.
Wakati ambapo kiongozi anaongoza watu, na hachukui maamuzi kwa maoni yake tu, bila kushirikisha wengine na kupata maoni yao, ikionekana wazi walio wengi katika vikao vya juu wanapinga, hawezi kuamua kivyake.
Ni mazingira kama hayo ambayo yanaonekana kuhusu suala la uraia wa nchi mbili, ambao ungeruhusiwa wale wenye asili ya Tanzania wanaoishi ugenini.
Na hata waliofukuzwa katika baadhi ya matukio mabaya kama mauaji yaliyofuatia mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964, wangeanza kujisikia karibu zaidi na nchi yao ya asili.
Lakini hulka za mapinduzi na za kuwachukia hata hao waliopata nafasi ya kukaa na kustawi nchi za nje bado ipo.
Kwa mfano wasiwasi kuwa wakija huku watakuwa na nguvu ya kifedha na kuwa tabaka muhimu miongoni mwa watu, kitu ambacho baadhi ya hao wanaosema waache wakae huko wasingependa kitokee.
Hivyo ‘tunasamehe’ mitaji, ujuzi, tekinolojia kwa wingi. Mchomo huo ni sehemu ya nia za ‘Smart Partnership Dialogue,’ kuwa wanakutana watu wenye dhamana kubwa au ushawishi wa wazi katika jamii za nchi tofauti.
Wakiangalia ni maeneo yapi, kinachoweza kufanyika ni kipi, katika uendelezaji wa sayansi na tekinolojia.
Pale wazo linapoainishwa, ni suala la kila kiongozi kujaribu kuwashawishi watu wake, akifaulu watasonga mbele kimaendeleo, na akishindwa wataendelea kukwama, na ni moja ya matatizo ambayo yanaikumba Tanzania.
Ni vigumu kufikia makubaliano kuhusu uendelezaji huo wa tekinolojia kama bado tunafungiwa na mawazo ya uzalendo ukereketwa, jadi za mapinduzi na kuchukua ubepari.
Juhudi hizo za Rais Kikwete hazikuanza na wazo tu la uraia wa nchi mbili ila suala la kuwahusisha kwa karibu zaidi Wamarekani-Waafrika wenye hamu ya kuwa sehemu ya juhudi zetu za maendeleo.
Mradi wahakikishiwe kuwa na haki sawa na wengine, yaani uhuru wa kununua na kuuza, kama mwananchi.
Ndiyo hapo linakuja suala la uraia wa nchi mbili kwani anaweza kuwa ni mtu aliyetoka huku na ‘kuzamia’ huko, au mwanaye ambaye alizaliwa ng’ambo na kwa sheria za huko yeye ni mwananchi.
Lakini katika sheria zetu asingetambuliwa, kwani kinachoangaliwa ni uraia wa baba yake. Marekani ingekuwa kama sisi isingefaulu kuendeleza vipaji na ari ya Barack Obama; angeitwa Mkenya.
Kimsingi anachosema Rais Kikwete ni kuwa hulka hii inakwamisha mambo mengi nchini, siyo katika sayansi na tekinolojia peke yake ila pia katika kilimo na uwekezaji kwa jumla.
Kwa mfano walioasisi mradi wa Richmond ambao ulihitaji mkopo wa nyongeza na mashine hizo zingekuwa za Tanesco (kwa kununua) baada ya mwaka mmoja ni pamoja na Mohamed Gire, raia wa Marekani mwenye asili ya ki-Tanzania.
Na waliofaulu kupata mashine hizo bila mkopo, yaani Dowans, pia ni pamoja na wa-Tanzania waliohamia nje, kama Brigedia Jenerali Suleiman al-Adawi ambaye alizaliwa Zanzibar na familia yake ikaponea chupu chupu mapanga ya mapinduzi. Tunaandaa ‘Smart Partnership’ na hatufikii maadili?
Pia Rais Kikwete aliandaa mazungumzo na Wamarekani wenye asili ya Afrika pale Arusha mwaka 2008, ambako suala la haki sawa kwa wote litakuwa limejadiliwa pia, na kuwekewa vipingamizi na wakereketwa wa uzalendo; halikufika kokote.
Ndiyo maana ni muhimu kuendelea na majadiliano kama ‘Smart Partnership Dialogue’ ili kuweza kukumbushana wapi tumeacha njia, na nini kinawezekana, wanapokuwapo watu wengine kutoka kote duniani wenye uwezo wa kutoa mawazo, na hata kuunda mawasiliano.
Kwa mfano nchi za Ulaya tayari zina kompyuta kwa kila mwanafunzi, na nchi kadhaa za Afrika zinakamilisha mipango ya kompyuta za matumizi finyu zaidi na ziwe za bei ndogo zaidi. Ni ule msemo wa kompyuta ya dola 100 kwa kila mwanafunzi, hapa wanafunzi wa vyuo, hata sekondari, wazipate.
Pia, ukiundwa mfuko unaochangiwa na serikali, kampuni za kompyuta, na wafadhili kama Bill Gates, Bill Clinton, Mo Ibrahim, Alhaji Aliko Dangote, Aga Khan na wengineo iwe ni Afrika Mashariki, hapa nchini na kwingineko duniani.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...