Tuesday, 13 August 2013

DK NDALINACHO ‘ACHANACHANA‘ UBORA WA ELIMU TANZANIA


Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Nchini (Necta), Dk Joyce Ndalichako 
Arusha: Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Nchini (Necta), Dk Joyce Ndalichako amesema karatasi za majibu ambazo wamekuwa wakizipata kutoka kwa wanafunzi zinaonyesha kuwa, watoto wengi wanahudhuria shuleni lakini hakuna wanachojifunza.
Dk Ndalichako aliyasema hayo jana jijini hapa alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa mabaraza ya mitihani ya Afrika, ambao umejikita kujadili suala la tathimini ya elimu kwa nchi za Afrika.

Hii ni mara ya kwanza kwa Dk Ndalichako kuzungumza tangu Serikali itangaze kufuta matokeo ya kidato cha nne mwaka 2012 na kutaka yapangwe upya, suala ambalo lilipingwa na wadau wengi wa elimu.
Alisema kuwa wakati nchi nyingi za bara hili zikiwa zimejitahidi kuongeza upatikanaji wa elimu kwa watu, ubora wa elimu unaendelea kuwa tishio kwa watu wa bara hili kwa vizazi vijavyo.
“Kama mabaraza ya mitihani, tumekuwa tukiona karatasi za majibu kutoka kwa wanafunzi ambazo zinaonyesha kwa uwazi kabisa kuwa watoto wanahudhuria shuleni lakini hakuna wanachojifunza,” alisema Dk Ndalichako.
Kwa upande wake Profesa Justinian Galabawa, alisema ili kuendeleza elimu, lazima uamuzi wa kitaalamu usiingiliwe na siasa kwa namna yoyote ile.
Alitolea mfano kitendo cha Serikali kufuta matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka 2012 akisema hakikuwa sahihi hata kidogo.
Alisema lazima vyombo vilivyopewa mamlaka kisheria kama Necta viachwe vifanye kazi bila kuingiliwa kwani kufanya hivyo kutaporomosha elimu.
Alisema pia lazima kuwa na sera ya nchi ya kufanya tathmini ambayo ili ifanye kazi lazima ishirikishe wadau wote na kila anayehusika kuitekeleza awe nayo.
“Jambo la kwanza ni lazima tuheshimu wataalamu na wasiingiliwe na wanasiasa, taasisi zilizoundwa kisheria na kupewa mamlaka ya kupima na kutambua watu ni lazima ziheshimiwe. Kama mtoto amepata daraja la nne huwezi kumpa la kwanza,” alisema Profesa Galabawa.
Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Seif Ali Iddi alisema mkutano huo ni sehemu nzuri ya Tanzania kujifunza kutoka kwenye nchi nyingine kujua ni nini watu wengine wanafanya.
Alisema uzoefu utakaopatikana kutokana na mkutano huu utasaidia katika kujipima na kuendeleza elimu nchini.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo, Philipo Mulugo alisema kwa siku ya kwanza tu wamebaini kuwa zaidi ya asilimia 80 ya nchi za Afrika tayari wanatumia mfumo wa usahihishaji kwa kutumia mashine maalumu (OMR) ambao bado baadhi ya watu nchini wanaulalamikia.
Alisema baadhi ya nchi sasa wameanza kusahihisha kwa kutumia kompyuta hata maswali ya kujieleza, hivyo akawataka Watanzania waache kujirudisha nyuma.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...