Saturday 31 August 2013

Hatma ya watuhumiwa wa dawa za kulevya JNIA Sept. 5


Waziri wa Uchukuzi, Dk.Harrison Mwakyembe
Hatma ya Maofisa wanne wa usalama wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wanaodaiwa kuhusika kula njama kusafirishwa dawa za kulevya zenye thamani ya Sh. bilioni 6.8 itajulikana Septemba 5, mwaka huu.

Maofisa wanaotuhumiwa katika kashfa hiyo ni Yusufu Daniel Issa, Jackson Manyonyi, Juliana Thadei na Mohamed Kalungwana. 




Maofisa hao wameshakabidhiwa barua ya tuhuma zao Agosti 23, mwaka huu na baada ya siku 14 tangu wakabidhiwe taratibu zitakazofuata ni kufukuzwa kazi rasmi au kushitakiwa mahakamani kutokana na agizo la Waziri wa Uchukuzi, Dk.Harrison Mwakyembe.

Meneja wa Usalama wa uwanja huo, Clemence Jingu, akizungumza na NIPASHE jana alisema maofisa hao watatakiwa kujitetea ndani ya siku 14 kabla hatua za kuwafukuza kazi hazijachukuliwa.

Jingu ambaye alikuwa akitoa ufafanuzi kufuatia baadhi ya vyombo vya habari (siyo NIPASHE) kueleza kuwa maofisa wamefukuzwa kazi, alisema kama majibu yao watakayoyatoa yatahitaji kuundwa tume utaratibu huo utafanyika na kama hakutakuwa na haja watafukuzwa kazi moja kwa moja.

“Maofisa hao bado hawajafukuzwa kazi, kilichofanyika baada ya agizo la waziri waliandikiwa barua ya kusimamishwa kazi, na Ijumaa iliyopita walikabidhiwa hati/barua ya tuhuma zao,”alisema Jingu.

Agosti 16 mwaka huu, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Mwakyembe aliwagiza viongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) kuwachukulia hatua ikiwamo kuwafukuza kazi maofisa hao kwa kudaiwa kuhusika katika njama za kusafirisha dawa za kulevya.

Dk.Mwakyembe alitoa agizo hilo kufuatia kilo 150 za dawa za kulevya zenye thamani ya Sh.bilioni 6.8 zilizokamatwa Julai 5, mwaka huu nchini Afrika Kusini zikitokea Tanzania baada ya kusafirishwa kupitia uwanja wa JNIA.  
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...