Sunday 25 August 2013

Kanisa lalipuliwa kwa mabomu Dar




Yalitengenezwa kwa chupa kujazwa petroli
 Madhabahu, gari la mchungaji vyaunguzwa
Matukio ya mabomu kurushwa kanisani yanaendelea nchini, kufuatia kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Usharika wa Segerea, jijini Dar es Salaam kunusurika kuteketea kwa moto uliotokana na milipuko ya mabomu usiku wa kuamkia jana.
Tukio hilo la kustaajabisha, lilitokea wakati waumini wakiwa katika ibada ya mkesha na ndipo mabomu matatu ya kienyeji yaliporushwa ndani ya kanisa hilo.

Mabomu hayo ya kienyeji ambayo yalirushwa na watu wasiofahamika, yalitengenezwa kwa chupa zilizojazwa mchanganyiko wa mafuta ya taa na petroli na kuwashwa moto ambapo yaliunguza eneo la madhabahu na sehemu kubwa ya gari binafsi la mchungaji.
NIPASHE Jumapili, ilifika eneo la tukio na kushuhudia sehemu ya madhabahu ya kanisa hilo ikiwa imeharibiwa na mabomu hayo.
Mchungaji wa Usharika wa Segerea, Noah Kipungu, akielezea tukio hilo, alisema chupa za bia zilizojazwa mafuta hayo zikiwa zimezibwa na mifuniko iliyotobolewa tundu la utambi ziliwashwa moto ili kuchochea mlipuko.
Hata hivyo, alisema hakuna majeruhi wala vifo vilivyotokea kwenye mlipuko huo licha ya watu kukumbwa na taharuki.
Kadhalika, kanisa hilo lililojengwa kwa mbao na mabati lilinusurika kuungua pamoja na samani hasa viti vya plastiki, ala za muziki –ngoma, vipaza sauti na vifaa vya ibada kama mimbari ya kioo havikuathirika.
MASHAMBULIZI
Kipingu alisema waumini zaidi ya 30 wakiwa wameshikana mikono kwenye mduara huku wakiomba walipigwa na taharuki baada ya kusikia kishindo cha mlipuko kilichoambatana na moto.
Mchungaji alisema watu wasiofahamika waliokuwa nje ya kanisa hilo, walirusha chupa tatu zilizopitia kwenye mtambaa wa panya na kuangukia ndani ya kanisa sehemu ya madhabahu na kuunguza kurasa chache za Biblia zilizokuwa zimefunguliwa, mto wa kupigia magoti, kipande cha sakafu ya altare na nyaya za spika.
Alisema ‘bomu‘ lingine lilitegwa chini ya gari yake binafsi iliyokuwa imeegeshwa nje wakati wa ibada, na lilipolipuka liliunguza gari baada ya kutegeshwa chini ya tangi la mafuta.
Mabomu hayo yalitupwa kati ya saa 7:45 na saa 8:00 usiku, kipindi hicho waumini wakisali kwenye mkesha wa kuombea mkutano wa Injili unaotarajiwa kuanza leo.
Polisi na waumini waliokagua eneo la tukio waliokota chupa nyingine tatu ambazo hazijalipuka zikiwa zimetupwa na wahusika kukimbia.
Mchungaji huyo alisema baada ya tukio hilo walitoa taarifa polisi ambao waliwahi kufika kanisani hapo.
Aliongeza kuwa baada ya taharuki hiyo, waumini waliendelea na ibada huku akisisitiza kuwa mkutano huo wa injili utafanyika.
Hata hivyo, mchungaji Kipingu alisema hajui sababu ya mashambulizi hayo na hawezi kumtuhumu mtu yeyote kuhusika na tukio hilo.
Alisema hakuna mtu aliyekamatwa hadi jana mchana na polisi wapelelezi walikuwa kwenye eneo la tukio wakiendelea na uchunguzi.
KAULI YA POLISI
Kamanda wa Polisi mkoa wa kipolisi Ilala, alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo, Marietha Minangi, alisema yuko nje kwa dharura.

ULINZI KANISANI
Baadhi ya waumini na viongozi waliozungumza na gazeti hili akiwamo naibu mwekahazina na kiongozi wa kwaya, Godfrey Chambile, alisema kanisa lina walinzi wa kampuni binafsi wanaotumika usiku na mlinzi wa Usharika anayefanyakazi mchana. Wakati wa mlipuko mlinzi wa kampuni binafsi alikuwa kazini.
Alisema kanisa hilo limekuwapo mahali hapo kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 1990 na hajawahi kusikia ugomvi baina ya Usharika na majirani.
Mzee wa Kanisa Itunda Mbwambo, akizungumza na gazeti hili alisema madhara yamedhibitiwa kwa vile waumini walikuwapo na kuudhibiti moto bila hivyo kanisa lingeteketea.
Alisema hakuna haja ya kushuku bali kuwaachia polisi wafanye uchunguzi ili ukweli ujulikane pia aliwataka waamini kuomba amani na kuendelea na utulivu.
Hili ni tukio la pili kutokea kwa mwaka huu la kutupa mabomu kanisani. La kwanza lilitokea kwenye Kanisa Katoliki la Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi lililoko Olasiti jijini Arusha.
Mlipuko huo uliotokea mwezi Mei uliua watu wawili na kujeruhi zaidi ya 50 katika mashambulizi yaliyofanywa wakati Balozi wa Papa nchini, Francisco Padilla na Askofu wa Jimbo Kuu la Arusha Josephat Lebulu, wakitabaruku kanisa hilo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...