Na Mwandishi Wetu, Arusha
MAUAJI ya bilionea ambaye ni mfanyabiashara mkubwa wa madini ya Tanzanite huko Mererani mkoani Arusha, Erasto Msuya aliyeuawa kwa kumiminiwa risasi kibao juzi, yamesababisha kutanda kwa hofu jijini hapa.
Tukio hilo lililojiri maeneo ya KIA alipokuwa akitokea Mererani kuelekea Moshi, Kilimanjaro limeacha maswali mengi ambayo yanahitaji majibu.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa, bilionea huyo anayemiliki Hoteli ya SG Resort iliyopo Sakina jijini hapa alipigiwa simu akielezwa kuwa kuna biashara ya kufanya Moshi lakini kabla ya kufika alivamiwa njiani.
Ilidaiwa kuwa Erasto aliuawa akiwa na gari lake jipya aina ya Range Rover Voque la 2013 alilonunua hivi karibu kwa dola za Kimarekani 250,000 (zaidi ya Sh. milioni 400 za Kitanzania).
Habari za kiuchunguzi zilibaini kuwa kuna vitu vingi nyuma ya mauaji hayo huku suala visasi vya kibiashara likipewa kipaumbele.
“Kuna jamaa mwingine aliuawa juzikati kule Mererani, walikuwa wakifanya biashara na Erasto hivyo inawezekana ikawa ni kisasi katika mambo ya biashara ya madini.
“Unajua hii biashara ni ya kuvizianaviziana sana kwa hiyo itakuwa ni njama kwa sababu kuna watu wanadai wakati anaondoka Mererani alikuwa ameshanunua mzigo mkubwa.
“Pia inawezekana kweli ni majambazi ambao walijua kabisa Erasto ana mzigo ndiyo maana wakamfanyizia na kuchukua mzigo.
“Hii inaonesha kuna aina fulani ya utekaji na majibizano ya risasi kwa sababu tukio lenyewe limefanyika nje ya barabara, porini kabisa na gari linaonekana limepaki kwa utaratibu wa kawaida bila vurugu ‘so’ kwa vyovyote ni ishu iliyopangwa,” alisema mmoja wa wafanyabiashara wa madini aliyefika eneo la tukio.
Uchunguzi mwingine uliibuka na madai kuwa huenda kuna visasi vya kimapenzi lakini kuvizungumzia inakuwa ngumu kwa sababu ya kukosekana kwa ushahidi wa moja kwa moja.
“Mimi nakwambia tusubiri, mauaji haya yataibua mambo mengi sana kwa sababu ndani ya kipindi kifupi kumetokea vifo vya vijana matajiri wenye umri mdogo kati ya 37 na 40.
“Ukihesabu sasa hivi wanafika matajiri kama watano na wote walikuwa ni ‘kampani’ moja.
“Alianza Wakili Mawala aliyejirusha gorofani Nairobi, Kenya. Akafuatia Henry Nyiti, akaja Babu Sameke, akafuatia yule jamaa aliyejirusha gorofani Kariakoo na yule mwingine aliyepigwa risasi kule Masaki, Dar.
“Sasa Erasto naye ameuawa. Kwa vyovyote kuna kitu. Kama siyo mambo ya kulogana, basi kuna kitu waligusa,” alisema jamaa mwingine anayewajua vizuri wafanyabiashara wa madini Arusha.
Habari zinadai kuwa baadhi ya matajiri wamepanga kulikimbia jiji hilo kutokana na hofu juu ya maisha yao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alipotafutwa na gazeti hili, simu yake iliita bila kupokelewa.
CHANZO: GPL
No comments:
Post a Comment