Dar es Salaam. Mfanyabiasha wa kahawa,Tony Afred ameibuka mshindi wa shindano la kutwiti wazo la kuondokana na umaskini linalodhaminiwa na Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk Reginald Mengi.
Afred ambaye anafanya biashara ya kuuza kahawa kwa vikombe katika shindano hilo,amejinyakulia Sh1 milioni baada ya kutwiti swali lililoulizwa ‘kijana asiyekuwa na ajira wala fedha anaweza kuanza kujijenga kiuchumi? Ambapo alijibu kuwa popote kijana alipo asijali kwamba hana fedha wala ajira bali aangalie ni nini anachoweza kuifanyia jamii na huo ndiyo utakuwa mtaji wake.
Kutokana na majibu hayo twiti yake iliweza kuingia mara tano katika kumi bora na kuibuka ya kwanza ambapo aliwaasa vijana wachukue wazo hilo na kulifanyia kazi ipasavyo kwani hawataweza kupata shida.
“Mtu yoyote akipata wazo hili atajua mahali pa kuanzia na hatimaye kujikwamua kiuchumi,” alisema Alfred.
Mshindi wa pili John Mkungu ambaye alipata Sh500,000 alitwiti kuwa, kijana anatakiwa atambue fursa anayoipenda na kuimudu aanze kujitolea, ubora wa huduma ukijulikana watu watamfuata.
Maduhu Jumanne, alipata Sh300,000,kwa kutwiti kuwa kama kijana yupo kijijini anaweza kulima na akiuza mazao yake anaweka akiba, kama yupo mjini anatafuta vibarua na kuweka akiba hatimaye kuwa mjasiriamali. Dk Mengi alisema shindano hilo ni la tatu na litakuwa endelevu huku twiti zilizopatikana zinafanyiwa utaratibu wa kuwekwa ili zisambazwe katika shule na vijana watapata fursa ya kusisoma.
CHANZO: Mwananchi
No comments:
Post a Comment