Friday 23 August 2013

NHC: `Vimemo` vya wakubwa vinakwamisha utendaji wetu


James Lembeli,Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), limesema baadhi ya wanasiasa walioko katika mamlaka za juu serikalini, watu maarufu pamoja na matajiri, wamekuwa wakiendesha vitendo vya hujuma za makusudi kwa nia mbaya ya kukwamisha kasi ya utendaji kazi mzuri wa shirika.

Baadhi ya watu hao wanadaiwa kufanya hujuma hizo kwa kuvamia viwanja na nyumba za NHC na kujimilikisha kinyume cha sheria.

Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria wa NHC, Martin Mdoe, alisema hayo wakati Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, ilipokutana na uongozi wa shirika hilo, jijini Dar es Salaam jana.

Mdoe alisema kuna kesi nyingi mahakamani zinazotokana na watu hao kuvamia nyumba na viwanja vya shirika.

Alisema katika mlolongo huo, baadhi ya watu hao wamefungua kesi mahakamani kudai kwamba, ni wamiliki halali wa viwanja na nyumba za shirika, wakati si kweli.

Kwa mujibu wa Mdoe, kati ya watu hao, wengine wamefungua kesi mahakamani wakidai wapewe haki ya kuendeleza sehemu ya maeneo ya shirika, wakati si wamiliki halali wa maeneo hayo.

Alisema baya zaidi, inapotokea NHC kutaka kukata rufaa kupinga uamuzi wa mahakama dhidi yake, kumekuwa na ‘vimemo’ kutoka kwa baadhi ya wanasiasa walioko mamlaka ya juu serikalini kwenda kwenye uongozi wa shirika kuuzuia kufanya hivyo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambaye ni Mbunge wa Kahama, James Lembeli, aliutaka uongozi wa NHC kutorudi nyuma katika mpango wake wa kukata rufaa akisema hakuna mwenye uwezo wa kuwazuia kufanya hivyo.

Pia aliwataka wanasiasa na watu maarufu nchini kuacha vitendo vya uvamizi wa ardhi, nyumba na maliasili za umma.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...