Moshi na Arusha: Polisi nchini limesema mauaji ya mfanyabiashara tajiri wa madini wa Mirerani, Erasto Msuya yalipangwa na baadhi ya wafanyabiashara wa madini ya Tanzanite kwa lengo la kulipiza kisasi.
Kauli hiyo imetolewa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz ambaye pia alimtaja mfanyabiashara tajiri wa madini kuwa ni miongoni mwa watu waliokamatwa hadi sasa.
Mfanyabiashara huyo aliuawa kwa kupigwa risasi nyingi kwa bunduki ya kivita aina ya Sub Machine Gun (SMG) Agosti 7 mwaka huu eneo la Mijohoroni wilayani Hai Kilimanjaro, ambapo katika eneo la mauaji hayo lilipo hatua zipatazo 70 kutoka barabara kuu ya Moshi-Arusha, yaliokotwa maganda 21 ya risasi za SMG lakini inaelezwa risasi zilizompata zilikuwa ni 12.
Wakati polisi wakimshikilia mtu anayedaiwa kuhusika na tukio hilo, watu wanaosadikiwa kuwa majambazi wamevamia nyumbani kwa bilionea mwingine Arusha kupora kiasi kikubwa cha pesa kabla ya kumfyatulia risasi mlinzi na kusababisha kifo chake.
Kamanda Boaz aliwataja wanaoshikiliwa kuwa ni pamoja na mfanyabiashara Shariff Mohamed Athman (31) Mkazi wa Kimandolu na dereva aitwaye Mussa Mango (30) Mkazi wa Shangarai Arusha.
Kwa mujibu wa Kamanda Boaz, mwingine aliyekamatwa ni Shwaibu Jumanne Said(38) maarufu kwa jina la Mredii, Mkazi wa Mererani Wilaya ya Simanjiro katika Mkoa wa Manyara.Kamanda Boaz alikataa kueleza ushiriki wao akisema hilo lingeweza kuathiri uchunguzi unaoendelea wa mauaji hayo yaliyotikisa miji ya Arusha, Mererani na Moshi.
Imeandikwa na Daniel Mjema, Rehema Matowo (Moshi) na Peter Saramba (Arusha).
CHANZO: Mwananchi
No comments:
Post a Comment