(Picha: AP/Tsvangirayi Mukwazhi)
RAIS Robert Mugabe wa Zimbabwe leo ameapishwa kwa mara ya saba kama kiongozi wa nchi hiyo na ataingoza nchi hiyo kwa miaka mingine mitano.
Sherehe za kuapishwa rais huyo mwenye umri wa miaka 89 zilikuwa zikicheleweshwa kwa sababu ya kesi iliyokuwa imewasilishwa mahakamani kupinga kuchaguliwa kwake na mpinzani wake mkuu Morgan Tsvangirai, ambaye alidai kulikuwa na wizi wa kura.
Tsvangirai pia anadai wapiga kura wake waliondolewa kwenye vituo vya kupigia kura katika maeneo ya mijini, yanayoaminiwa kuwa ngome yake ya kisiasa.
Itakuwa ni fursa nyingine kwa rais Robert Mugabe kutoa hotuba zake zenye makali hususani kuyashutumu mataifa ya magharibi kutokana na vikwazo vilivyowekwa kwa Zimbabwe na kuuponda upinzani unaoongozwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Morgan Tsvangirai.
Zaidi ya marais arobaini wa mataifa ya kigeni wamealikwa katika sherehe za leo kushuhudia kuapishwa kwa Robert Mugabe katika uwanja mkubwa zaidi wa michezo nchini Zimbabwe uliopo mjini Harare.
Waandaaji wamesema kuwa sherehe za leo zinatarajiwa kuwa za hali ya juu kuliko sherehe za mwaka 1980 baada ya Zimbabwe kupata uhuru.
CHANZO: GPL
No comments:
Post a Comment