Friday, 30 August 2013

SAA 4 ZAWATENGANISHA PACHA WALIOUNGANA


Daktari Bingwa wa Watoto katika Hospitali ya Muhimbili, Profesa Karim Manji (wa pili kushoto) akifurahia na wenzake baada ya kufanikiwa kwa operesheni ya kuwatenganisha watoto walioungana, kazi iliyofanywa na jopo la madaktari bingwa saba kwa saa 4. Picha na Michael Jamson 

Dar es Salaam. Jopo la Madaktari Bingwa Saba wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Mifupa ya hospitali hiyo (Moi), wamefanikiwa kuwatenganisha pacha waliokuwa wameungana kiwiliwili.
Iliwalazimu mabingwa hao kutumia saa nne kufanikisha upasuaji huo. Mmoja wa watoto hao waliotenganishwa, amelazwa kwenye Wodi ya Uangalizi Maalumu (ICU) Taasisi ya Mifupa Moi wakati kiwiliwili kingine kilifariki.

Jopo la madaktari waliofanikisha upasuaji huo ni; bingwa mstaafu wa watoto ambaye aliitwa maalumu kwa kazi hiyo, Petronila Ngiloi, Dk Robert Mhina (mifupa) na Profesa Karim Manji aliyekuwa akifuatilia kwa karibu mapigo ya moyo.
Wengine ni Dk Karima Khalid aliyekuwa akiratibu dawa ya usingizi, Dk Hamis Shaaban (ubongo na uti wa mgongo), Dk Zaitun Bokhary (bingwa upasuaji watoto) na Dk Nyangasa (moyo na mishipa ya fahamu).
Akizungumza baada ya upasuaji huo, Dk Shaaban alisema walimfanyia vipimo mtoto ambaye hakuwa amekamilika na kugundulika kuwa hakuwa amekamilika viungo vyote achilia mbali kutokuwa na kichwa na macho pia hakuwa na moyo, figo, tumbo, maini ila alikuwa na uti wa mgongo.
“Uti wa mgongo ulikuwepo na ndio uliokuwa umeshikana na mwenzake na kuna mshipa mmoja wa fahamu ulikuwa unafanya kazi ndio maana alikuwa ukimgusa anachezesha mguu.”
Alisema kinachoratibiwa kwa sasa ni kuangalia dawa ya usingizi aliyopewa mtoto ambaye anaendelea kupumua na kwamba ndani ya saa 24, dawa ya usingizi waliyomuwekea mtoto huyo itakuwa imeisha na ataanza kunyonya kama kawaida.

Upasuaji

Kazi ya upasuaji huo ilianza saa mbili asubuhi kwa mtoto huyo wa jinsi ya kike aliyetimia kuchukuliwa vipimo mbalimbali ikiwemo CT Scan, MRI, Ultra sound na vingine vingi kabla ya upasuaji kamili kuanza saa tano asubuhi.
Dk Shaaban alisema ni mara ya kwanza kwa Moi kufanya upasuaji wa aina ile na kwamba mara nyingi wamekuwa wakifanya upasuaji wa watoto wanaozaliwa na vichwa vikubwa pamoja na mgongo wazi ambao tatizo hilo linasababishwa na upungufu wa madini ya folic acid.
Kabla ya upasuaji kuanza, mama wa mtoto huyo Pili Hija (24) alitumia muda wa nusu saa kufanya maombi maalumu ya kumwombea mtoto wake kisha kuwaruhusu madaktari kuendelea na upasuaji huo.
Akizungumza muda mfupi baada ya kuruhusiwa kumwona mtoto wake, Hija alisema: “Ninamshukuru Mungu kwa yote na nazidi kumwomba amjalie mwanangu apone kabisa, nawashukuru na nitazidi kuwaombea madaktari wanaomtibu mwanangu.”
Alijifungulia nyumbani Agosti 18 maeneo ya Jang’ombe, Zanzibar watoto pacha walioungana mmoja akiwa amekamilika viungo vyote na mwingine akiwa na kiwiliwili.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...