Dawa za kuchochea uchungu kwa wajazito zikiwamo ‘misoprostol’ , ‘oxytocin’ , `Mifecon-Mkit’ kupatikana kiholela kwenye maduka ya dawa kumechochea utoaji mimba kufanyika bila hofu wala kipingamizi.
Utoaji mimba wa kutumia dawa hizo na njia nyingine za kienyeji unafanyika kwenye mazingira duni, kwa kutumia vifaa vichafu wanavyotumia wauguzi ‘vishoka’ .
Hali hiyo inasababisha mabinti na wanawake kuambukizwa maradhi ya mfumo wa uzazi mfano (PID), Ukimwi na VVU na wengine kuharibu mfuko wa uzazi na kusababisha ugumba.
Uchunguzi wa NIPASHE Jumapili, uligundua kuwa vidonge hivyo hupatikana kwa urahisi kwenye maduka ya dawa muhimu na hivyo wanawake huzipata kwa urahisi wanapotaka kuharibu mimba.
Baadhi ya wateja wanaeleza kuwa wahudumu kwenye maduka hayo wanawaelekeza na kuwapa ushauri wajawazito wanaotaka kutoa mimba.
Walisema dawa hizo hupatikana kwa bei kubwa mfano Mifecon-Mkit huuzwa kwa Sh. 30,000 hadi 50,000 wakati ‘misoprostol’ inapatikana kuanzia Sh. 10,000 na zaidi kutegemeana na mahali zinapopatikana na soko lilivyo wakati huo.
Wauza dawa hizo hupandisha bei ili kuwahadaa wajawazito hao kwa ajili ya kupata faida zaidi licha ya kwamba maeneo mengine dawa hizo zinaweza kupatikana kwa bei ya chini.
DAWA ZINAZOTUMIWA
Misoprost -200 maarufu kama ‘miso’ ni vidonge vinavyotumiwa vibaya sehemu nyingi jijini Dar es Salaam kwa kutoa mimba kwa maelekezo yanayotolewa na wahudumu wa maduka ya dawa, wahudumu wa afya wasio na maadili na madaktari ‘vishoka’ mitaani.
Wanadaiwa kuwaelekeza wateja kuweka vidonge chini ya ulimi ili viyeyuke na vingine huingizwa sehemu za siri karibu na shingo ya uzazi.
Aidha dawa hiyo ya aina moja hutolewa maelekezo tofauti huku wengine wakitoa dozi kubwa zaidi, alisema mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ualimu cha Dar es Salaam (DUCE).
Vidonge hivyo hupanua shingo ya kizazi na kusababisha hewa kupita kwenye nyumba ya uzazi na kubomoa ukuta wa tumbo la uzazi na kuharibu mimba.
Kwa upande wa ‘mkit’ ambalo katika mahojiano na baadhi ya mabinti wanaofanyabiashara ya ngono Buguruni, jijini Dar es Salaam, walisifia kwa kuipa jina la ‘kubwa la maadui’ walidai inatoa mimba yenye umri wowote hata pale ‘miso’ inaposhindwa .
Baadhi ya wauzaji waliitaja kuwa ni bingwa na wanawapatia wateja wao hasa wenye mashaka na dawa nyingine.
‘Mkit’ kwa mujibu wa wataalamu inatumiwa kuharakisha uchungu kama ilivyo kwa ‘miso’ lakini inatumiwa vibaya pale inapomezwa ili kuharibu mimba.
Baadhi ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu walikiri kuwa dawa hii inawasaidia lakini wengine walisema si wakati wote kwani wapo waliodai waliitumia lakini badala ya kuharibu ilikuza mimba.
Tembe nyingine zinazotumiwa ni ‘arzithromycin-500’ ambazo huingizwa sehemu za siri na nyingine humezwa.
Mmoja wa madaktari ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini alisema kuwa dawa hii si ya kuharibu mimba bali inatumika kutiba maradhi mbalimbali kama kifua, magonjwa ya ngono na kukausha vidonda vilivyotokana na kushambuliwa na vimelea .
Kwa upande wa ‘oxytocin’ watumiaji hununua na kuchomwa sindano kisha kurudi nyumbani kusubiria mimba kuharibika.
UTOAJI MIMBA KIENYEJI
Baadhi ya mabinti hutolewa mimba kwa kutumia kijiti cha jani la mhogo na miti ya mbaazi, vyuma vya baiskeli (spoku) , sindano, majani ya aloivera, mwarubaini, kunywa chai ya rangi yenye majani mengi, kemikali zikiwamo shabu inayotumiwa kusafishia maji na hata kuingiziwa dawa za kienyeji sehemu za siri.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi inayojishughulisha na kukuza, kuendeleza haki na maendeleo kwa watoto, vijana na wanawake (Kiwohede), Yusta Mwaituka, ambaye pia ni muuguzi na mkunga anasema utoaji mimba kienyeji umeshamiri sehemu nyingi.
Anaeleza kuwa utoaji mimba unafanywa kienyeji kwa kutumia spoku, miti ya kisamvu ama vijiti vya mbaazi ambavyo mabinti na wanawake huvipitisha sehemu za siri na kutoboa mfuko wa uzazi na wakati mwingine sindano zenye dawa au maji dawa hutumika.
Mwaituka anasema tatizo la utoaji mimba kienyeji hukuzwa na uwapo wa wataalamu `feki' mitaani ambao wanafahamika na jamii lakini hawachukuliwi hatua na wameendelea kuneemeka.
Mwaituka anaeleza kuwa wakati mwingine wazazi wanachangia kusababisha mabinti kupata na kuharibu mimba kutokana na kuwaelekeza kushiriki ngono.
“Mzazi anamwambia binti yake umekuwa mkubwa baba yake hawezi kununua losheni na nguo za ndani tafuta mfadhili. Malezi hayo husababisha wasichana kufanya ngono mapema, kupata ujauzito na kutolewa mimba kienyeji mitaani.”
MAENEO MAARUFU
Zipo sehemu mbalimbali zinazojihusisha na utoaji mimba zikiwamo hospitali za umma, binafsi na zahanati bubu zinazojulikana kwa kazi hiyo.
Jijini Dar es Salaam baadhi ya madaktari wa hospitali za umma na binafsi wanatajwa kufanya kazi hiyo, wakati wanafunzi wa vyuo vikuu vya tiba nao wanatuhumiwa.
Zipo zahanati maarufu kwa ajili ya utoaji mimba na zinazojulikana baadhi zipo karibu na mabweni ya wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu. Baadhi ya wakazi wa meneo ya Kinondoni Mkwajuni, Yombo Kilakala, Dovya , Tandika na sehemu za Tabata walieleza kuwapo uhalifu huo.
MAELEZO YA MSD
Ili kujua sababu za dawa zinazochangia utoaji mimba kuuzwa madukani gazeti hili liliwasiliana na Bohari ya Dawa (msd) kupata ufafanuzi na kufahamishwa kuwa dawa kama ‘misoprostol’ zinaagizwa na kuuzwa nchini kisheria.
Kwa mujibu wa Meneja Manunuzi wa Msd, Nichodemus Frederick, dawa hizo hutumika kuzuia kutokwa damu nyingi baada ya kujifungua ama kuchochea uchungu mjamzito anapokawia kujifungua.
Frederick ambaye kitaaluma ni daktari, alisema dawa hizo hutolewa kwa kipimo maalumu na kwa maelekezo ya wataalamu.
Kuhusu ‘ oxytocin’ ambayo hujulikana kama maji ya uchungu kwa mujibu wa Frederick, inatumiwa kama sindano ili kuongeza kasi ya uchungu kwa mjamzito.
Katika muongozo wa tiba wa taifa unaotolewa na Wizara ya Afya, dawa hiyo ni ya sindano na kwamba hutolewa kupitia dripu ambayo mjamzito hulishwa .
“Dawa hizo kuuzwa kwenye maduka ni utaratibu unaokubalika kisheria kwa kuwa lengo lake ni kuwasaidia wanaozihitaji kwa mujibu wa malekezo ya wataalamu na siyo kutoa mimba,” alisema Frederick.
Aliongeza kuwa kuzitumia kuharibu mimba ni matumizi mabaya na kusisitiza kuwa vidonge hivyo vinaagizwa na msd kwa ajili ya kufungashwa kwenye fungashio la mama mjamzito kwa ajili ya kuzuia kutokwa damu nyingi baada au kubla ya kujifungua au kumuongeza uchungu.
MADHARA
Frederick anataja athari za utoaji mimba kwa kutumia dawa hizi kuwa ni pamoja kuharibu taratibu za kimaumbile kwenye kizazi na kusababisha ugumba.
Zikitumiwa vibaya husababisha kutoka damu nyingi na kupoteza maisha kutokana na kukosea maelekezo ya wataalamu.
Anataja madhara ya kisaikolojia na kusononeka kutokana na moyo kujuta kutokana na kutoa mimba.
Mwaituka anataja tatizo la kupata magonjwa sugu ya via vya uzazi yanayoathiri shingo ya kizazi na mirija ya mayai.
Wanaotumia arzithromycin-500 wanaweza kujisababishia vidonda sehemu za siri na kwamba ni makosa kuzitumbukiza sehemu hizo pia kuna uwezekano wa kupata saratani maeneo ya uzazi kwa vile tembe hizi ni za kunywa.
SHERIA
Utoaji mimba ni kosa kisheria kwa Tanzania kwa mujibu wa sura ya 16 kifungu cha 150 – 152 cha kanuni za adhabu watuhumiwa watatu wanaweza kufungwa kutokana na kosa la utoaji mimba ambao ni mjamzito, daktari anayemtoa na anayetoa vifaa au kugharamia kazi hiyo.
Anayetoa mimba anaweza kufungwa miaka 14 au hata maisha , anayeomba kutolewa mimba anaweza kufungwa miaka saba na anayetoa vifaa au dawa kugharamia utoaji huo anafungwa miaka mitatu.
Kwa ujumla kutaka kutolewa mimba, kushiriki kuitoa na kugharamia ni kosa la jinai ni halali tu iwapo mimba inatolewa kwa idhini ya madaktari ili kuokoa maisha ya mama au kumkinga na madhara ya kiafya .
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment