Hospitali ya Taifa Muhimbili
Gharama za huduma za kulipia matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili zimepanda maradufu.
Hatua hiyo inayotekelezwa bila kuwashirikisha wadau na watoa huduma ilianza Septemba mosi mwaka huu na kulalamikiwa na wagonjwa na wafanyakazi.
Kwa mujibu wa tangazo la Mkurugenzi wa MNH, lililobandikwa kwenye ubao wa matangazo wa jengo la mateniti la kulipia huduma IPPM, inaonyesha kuwa gharama zilipanda kuanzia Septemba 2, wakati notisi hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi ilitolewa Septemba 4.
Wagonjwa wanaolipia matibabu binafsi Muhimbili waliliambia gazeti hili kuwa wateja wanaotumia ‘ast truck’ na huduma ya uzazi inayotolewa na kitengo cha mateniti- IPPM ndizo zilizoongezeka.
Kuanzia sasa upasuaji wazazi unalipiwa Sh. 500,000 badala ya 350,000 za awali. Uzazi wa kawaida ni Sh. 250,000 badala ya Sh. 150,000 zilizokuwa zikitozwa mwanzo.
Walisema kulala kunagharimu Sh. 20,000 badala ya 15,000 wakati tozo la kumuona daktari kwa mara ya kwanza ni Sh. 30,000 badala ya Sh. 20,000 za awali.
Kumuona daktari kwa ajili ya kufuatilia huduma na matibabu zimepanda hadi Sh. 20,000 kutoka Sh. 10,000.
Huduma nyingine kama dawa na uchunguzi wa maabara
zimepanda japo bei zake hazikutangazwa kwenye ubao wa matangazo.
Kwa wagonjwa wa kujifungua kawaida ambao hawalipii gharama watatozwa gharama ambazo hazikafafanuliwa ingawaje serikali inataka watibiwe bure.
“Mfano mjamzito akipata uchungu ghafla na kufika Muhimbili bila rufaa atatakiwa kalipia gharama” alisema mjamzito jina tunalo.
Msemaji wa MNH Aminieli Aligaesha, alikiri kuongezeka gharama hizo ziliongezeka na kuongeza kuwa sababu ya ongezeko hilo ni gharama kubwa za uendeshaji.
Hata hivyo alikataa kutoa maelezo zaidi na kutaka mwandishi wetu kwenda ofisini kwake kwa maelezo zaidi.
Hospitali ya Muhimbili inatoa huduma kwa utaratibu wa aina mbili kuchangia matibabu kunakofanywa na mgonjwa wa rufani pamoja na serikali.
Njia nyingine ni wagonjwa kulipia gharama zote za tiba kama ambavyo wanafanya kwenye hospitali za binafsi.
Hata hivyo gharama za tiba kwa wale wanaochangia matibabu na wale wa rufaa hazijaongezeka.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment