Thursday, 19 September 2013

HAUSIBOYI AMWIBIA BOSI WAKE GARI

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi


Mfanyakazi za ndani, Almas Stephen (18), mkazi wa Tabata Chang'ombe jijini Dar es Salaam, amemwibia bosi wake gari aina ya Rav4 lenye thamani ya mamilioni ya Shilingi.

Kufuatia tukio hilo, mfanyakazi huyo wa ndani pamoja na watu wengine wawili, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala.

Kijana huyo na wenzake hao wawili, wanatuhumiwa kumwibia bosi wake gari aina ya Rav4 lenye namba za usajili T553BMN. 

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, halikumtaja jina la bosi wa kijana huyo aliyeibiwa gari hilo isipokuwa alieleza kuwa ni mkazi wa Masaki, jijini Dar es Salaam.


Kamanda Minangi alisema kuwa mfanyakazi huyo wa ndani alimfuata mfanyakazi wa kike wa ndani wa bosi wake na kumwambia ampatie ufunguo wa gari hilo kwa maelezo kuwa ametumwa na bosi kwenda Supermarket.

Kwa mujibu wa Kamanda Minangi, Stephen baada ya kupewa funguo hizo na mfanyakazi wa kike, alichukua gari hilo na kujieleza kwa walinzi getini kuwa ametumwa na bosi wake ambapo nao bila kushuku chochote, walimruhusu kutoka na gari hilo.

Kamanda Minangi alifafanua kuwa baadaye bosi alimpigia simu mfanyakazi  wa kike kumuuliza alipo Stephen, ndipo alipojibiwa kuwa ameondoka na gari kwa madai kuwa yeye (bosi), alimtuma Supermarket.

Kamanda Minangi alisema mmiliki huyo baada ya kuelezwa na mfanyakazi wa ndani wa kike, aliifuatilia gari hilo kwa kutumia kifaa maalum kijulikanacho kwa kama ‘Car Track’ na kugundua gari lake lilipo na kuwasiliana na Jeshi la Polisi.

Alisema gari hilo lilikamatwa likiwa katika eneo laTabata Segerea.

Kamanda Minangi aliongeza kuwa ndani ya gari hilo alikuwapo Stephen na  watu wengine wawili ambao aliwataja kwa majina ya Ismail Stephen na Ramadhan Ismail.

Alifafanua kuwa watuhumiwa hao baada ya kukamatwa na Polisi na kuhojiwa, walieleza kuwa walikuwa wanalipeleka gari hilo kumuuzia mtu waliyemtaja kwa jina moja la Kinyerefezi, ingawa haikuelezwa ni mkazi wa wapi.

Hata hivyo, Kamanda Minangi alisema kuwa Jeshi hilo linamsaka mtu huyo ili kumhoji na ikiwezekana kumuunganisha na watuhumiwa hao watatu ambao wamefunguliwa kesi namba TBT/RB/383.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...