Dar es Salaam.Kesi ya dawa za kulevya inayomkabili raia wa Kenya, Mwanaidi Ramadhani Mfundo na wenzake saba, leo inatarajiwa kuanza kuunguruma katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.
Mwanaidi anafahamika pia kwa majina ya Mama Leila au Naima Mohammed Nyakiniwa.
Anadaiwa kuwa mfanyabiashara wa kimataifa wa dawa za kulevya ambaye amewahi pia kutajwa na Rais Barrack Obama wa Marekani kuwa ni mtu hatari kwa biashara hiyo.
Katika kesi hiyo yeye na wenzake, wanakabiliwa na shtaka la kuingiza nchini, dawa za kulevya aina ya Cocaine, zenye uzito wa kilo tano zikiwa na thamani ya Sh225 milioni.
Washtakiwa wengine ni Antony Arthur Karanja na Ben Ngare Macharia (wote Wakenya) na Watanzania Sara Munuo, Almas Said, Yahya Ibrahim, Aisha Kungwi na Rajabu Juma Mzome.
Kesi hiyo imepangwa kuanza kusikilizwa leo na Jaji Grace Mwakipesile ambapo upande wa Jamhuri utaanza kutoa ushahidi dhidi ya washtakiwa hao.
Washtakiwa walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Juni 3 mwaka 2011, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa shtaka la kuingiza nchini dawa hizo.
Kesi hiyo ilisikilizwa na Hakimu Mkazi Mustafa Siyani.
Akiwasomea shtaka hilo, Wakili wa Serikali, Patrick Malogoi, alidai kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo kinyume cha kifungu cha 16 (1) b (i) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, sura ya 95 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2009.
Inadaiwa kuwa walikamatwa na Polisi Juni mosi mwaka 2011 katika nyumba inayomilikiwa na Mama Leila iliyoko maeneo ya Mbezi Beach, wakiwa na dawa hizo.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment