Wednesday, 18 September 2013

MAWAKILI WATOANA JASHO KATIKA KESI YA DAWA ZA KULEVYA


Madawa ya Kulevya
Dar es Salaam. Kesi ya dawa za kulevya inayomkabili raia wa Kenya, Mwanaidi Ramadhani Mfundo, maarufu kwa jina la Mama Leila au Naima Mohammed Nyakiniwa na wenzake wanane, imeendelea kugubikwa na utata wa kisheria na kuzua mvutano uliosababisha iahirishwe kwa mara nyingine ili kusubiri uamuzi wa Mahakama.
Jana, Mahakama Kuu ilitengua hoja iliyozua mvutano mkubwa juzi kwa kuruhusu upande wa mashtaka kuwasilisha notisi ya kuongeza shahidi muhimu kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Eva Mamuya jambo lililopingwa na upande wa utetezi.
Mbali ya Mama Leila, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Anthony Arthur Karanja na Ben Ngare Macharia (wote Wakenya). Wengine ni Watanzania watano, Sarah Munuo, Almas Said, Yahya Ibrahim, Aisha Kungwi, Rajabu Juma Mzome na John William.
Wakati upande wa utetezi ukipinga uamuzi huo wa jana, upande wa mashtaka ulitoa hoja nyingine ya kuongeza shahidi wa pili, ASP Neema na kuibua mvutano mkali wa kisheria uliomlazimu Jaji Grace Mwakipesile anayesikiliza kesi hiyo, kuiahirisha hadi Ijumaa wiki hii atakapotoa uamuzi kama upande wa mashtaka ulikuwa sahihi au la kuwasilisha notisi hiyo mahakamani kabla ya uamuzi wa jana.
Mvutano wa kisheria
Ubishi ulianza mapema mahakamani wakati Jaji Mwakipesile alipokuwa akijiandaa kusoma uamuzi wake juu ya maombi ya upande wa mashtaka kuwasilisha notisi ya kuongeza shahidi.

Wakili wa utetezi, Yassin Member alisimama na kumwomba jaji kutokusoma uamuzi wake kwani tayari walikuwa na notisi ya upande wa mashtaka ya kuongeza ushahidi wakati ni kinyume cha sheria.
Member alilalamika kuwa upande wa mashtaka uliomba kuongeza shahidi mmoja lakini notisi ilionyesha walikuwa wanataka kuongeza mashahidi wawili.
“Mheshimiwa tunaomba usisome kwani tunashangaa tayari tumepewa notisi ya upande wa mashtaka wakati ukiwa bado hata hujatoa uamuzi wa maombi yao ya kuwasilisha notisi ya kuongeza shahidi. Kibaya zaidi wanataka kuongeza mashahidi wawili na siyo mmoja,” alisema Member.
Jaji Mwakipesile alijibu kwa kutaka upande wa utetezi kuipa nafasi mahakama kutoa uamuzi wake wa maombi ya upande wa mashtaka yaliyosababisha kesi hiyo kuahirishwa juzi.
“Ipe nafasi Mahakama kutoa uamuzi wake wa ombi la upande wa mashtaka la kuahirisha kesi ili waweze ku-file notice (kuwasilisha taarifa) ya additional witness (shahidi wa nyongeza), jambo ambalo ninyi mlipinga,’’ alisema Jaji Mwakipesile na kisha kutoa uamuzi wake na kukubali upande wa mashtaka kuongeza shahidi.
Uamuzi huo ulisababisha mvutano mkali mawakili wa utetezi wakisema haikuwa sahihi kwa upande wa mashtaka kuongeza mashahidi wakati ulishindwa kwenye Mahakama za chini wakati wa usikilizwaji wa mwanzo.
Wakili wa utetezi, Evod Mmanda alisema haikuwa sahihi kwa upande wa mashtaka kuwasilisha taarifa hiyo mahakamani hata kabla ya uamuzi wa Mahakama.
“Mheshimiwa Jaji, Prosecution (upande wa mashtaka) waliomba jana ahirisho ili waweze ku- file (kuwasilisha) hicho walichokiomba (taarifa ya kumwongeza shahidi), ruhusa umeitoa leo kwenye uamuzi wako, hivyo walitakiwa wa-file notice yao hiyo baada ya uamuzi wako (wa leo),” alisema na kuongeza:
“Hivyo hakuna notisi halali hapa mahakamani. Notisi halali ni ile watakayoiwasilisha baada ya uamuzi wako. Kwa hiyo sisi tunasema kuwa hadi sasa hakuna notisi halali ya kuita mashahidi wa ziada.”
“Kama Mahakama yako itaikubali hii wanayoita notisi, ingawa sisi tunasema siyo notisi halali, basi tunaomba Mahakama yako ione kuwa haikutolewa ‘in a reasonable time’ (wakati mwafaka).”
Pia alidai kuwa hata hiyo taarifa inayodaiwa na upande wa mashtaka kuwasilishwa, walipewa muda mfupi baada ya kuingia mahakamani na kwamba upande wa mashtaka katika maombi yao juzi walimtaja shahidi mmoja, Mamuya, lakini taarifa waliyopewa inawataja mashahidi wawili.
Wakili Mmanda aliiomba Mahakama chini ya Kifungu cha 289 (3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), iamue kama huo ni wakati mwafaka, kwa kuzingatia vigezo vya mazingira na wakati ambao upande wa mashtaka ulibaini umuhimu wa kuwaongeza mashahidi hao.
“Hawa wanatajwa kuwepo katika mchakato tangu mwanzo. Mamuya anakiri kupokea kifurishi (bahasha yenye vielelezo) Juni 16, 2011, hadi leo ni miaka miwili na miezi mitatu imepita. Hivyo walijua uwepo wa Mamuya mapema. Huu si wakati mwafaka,’’ alisema Wakili Mmanda.
Hata hivyo, alisema hawana maelezo ya maandishi ya Mamuya wala ya ASP Neema huku akidai kuwa maelezo ya ASP Neema yanaonyesha kuwa yameandikwa Juni 11, mwaka huu wakati hatua ya maelezo ya kesi ilishakamilika.
Hoja hizo za Wakili Mmanda ziliungwa mkono na Wakili mwingine wa utetezi, Jamhuri Johnson ambaye pia alidai hadi wakati huo alikuwa hajaona taarifa ya upande wa mashtaka kuongeza mashahidi.
Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali, Prosper Mwangamila alidai kuwa katika kesi zote za jinai si jukumu la upande wa mashtaka kuwapatia upande wa utetezi nyaraka mbalimbali wanazokusudia kuzitumia katika kesi, bali Mahakama.
“Notisi wanayoitaja iko mahakamani tangu jana, hivyo utaratibu uliotumika wao kupata nyaraka nyingine ndiyo unaotumika kuwapatia notisi hii. Hivyo hoja ya upande wa mashtaka kuchelewa kuwa ‘serve’ (kuwapatia) haina msingi,” alisema Wakili Mwangamila.
Alisema taarifa hiyo iko mahakamani kisheria kwa mujibu wa Kifungu cha 289 (1) na (2) cha CPA na kuiomba mahakama ione kuwa imewasilishwa katika muda mwafaka.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...