Kadri matatizo ya uzazi yanavyoendelea kukithiri duniani kote, wataalamu wa afya nao wanaendelea kuvumbua njia mbalimbali za kuwasaidia wenye matatizo ya kukosa watoto.
Katika harakati hizo Kliniki ya Upandikizaji ya Dar es Salaam, (Dar IVF and fertility clinic) wameanzisha huduma ya kununua mbegu za kiume na mayai ya wanawake, kwa ajili ya kutoa huduma ya uzazi kwa njia ya upandikizaji au IVF.
Gazeti hili lilipiga simu katika kliniki hiyo kutaka kujua iwapo linaweza kuchangia mayai na daktari aliyekuwapo zamu alijibu; “inawezekana”.
Daktari huyo ambaye hata hivyo alisema kliniki hiyo bado haijaruhusiwa kujitangaza katika vyombo vya habari, alisema kwa sasa kifaa cha kuhifadhi mayai (ya mwanamke) hakipo ila kifaa cha kuhifadhi mbegu za kiume kipo na wanapokea wachangiaji wanaotaka kuuza mayai hayo kwa makubaliano rasmi.
“Ukija tutajadiliana bei, kwa sasa hatuna bei rasmi, lakini nadhani ukija tutakubaliana. Siku ukiwa tayari njoo tujadili. Bei ni makubaliano,” alisema daktari huyo.
Alisema kwa kuwa kifaa cha kuhifadhi mayai hakipo hivyo mchangiaji atakapochangia mayai, yatatakiwa yatumike siku hiyo hiyo katika upandikizaji, lakini kifaa cha kuhifadhi mbegu za kiume, kipo.
Dk huyo (tunamuhifadhi jina kwa sababu ya sheria za hospitali hiyo), alisema mchangiaji wa mbegu au mayai atatakiwa kupimwa kwa kina, kwanza atapimwa damu kama ana maambukizi ya VVU, atapimwa iwapo ana maradhi ya urithi na kundi la damu kabla ya kukubaliwa kuchangia.
Tovuti ya kliniki hiyo inaeleza wazi huduma zinazotolewa ambapo mbali na uchangiaji wa mbegu na mayai, lakini huduma kuu ni kuwasaidia wenye matatizo ya uzazi, kupata watoto kwa njia ya upandikizaji.
Huduma nyingine ni kutibu matatizo ya ugumba kwa wanawake na wanaume, kuchagua jinsia ya mtoto, upasuaji wa kukaza kizazi kuzuia mimba kutoka (shridkar shuture) pamoja na huduma za matenite.
Madhumuni ya watu kuchangia mbegu au mayai ni katika kuhakikisha hakuna upungufu wa mbegu, na kuwasaidia wale wote ambao wameshindwa kutimiza ndoto za kuwa na familia.
Dk Henry Mwakyoma, Daktari Bingwa wa masuala ya uzazi wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Muhimbili anasema, maendeleo hayo yanafanikiwa zaidi nchi za nje ambako kuna teknolojia na utayari wa watu.
“Kwa hapa kwetu kwanza teknolojia hii bado haijapata umaarufu, lakini ni lazima kuhakikisha kuwa Watanzania wenyewe wapo tayari kukubali uzazi wa njia hii,” alisema Dk Mwakyoma
Alisema mchakato wa uhifadhi wa mayai unahitaji mazingira rafiki ya maabara ambayo yanafanana na mazingira yaliyo tumboni mwa mama.
“Wakati wa upandikizaji huu, ni lazima mbegu ziwekwe kwenye chombo chenye kiwango fulani cha joto, kemikali na viini lishe ili kulisaidia kurutubishwa kabla halijawekwa tumboni mwa mama,” anasema Dk Mwakyoma.
Hata hivyo, baadhi ya wataalamu wa afya na saikolojia wamekosoa azimio hili wakidai kuwa, litawafanya wasichana na vijana wenye tamaa ya fedha kukimbilia kutoa mbegu zao bila kutafakari madhara ya baadaye.
“Kwa jinsi dunia ilivyozingirwa na mahitaji ya fedha kwa kiasi kikubwa, lazima vijana wadogo watumie nafasi hii wakidhani itawapunguzia makali ya maisha.” Anasema kiongozi wa kampeni ya maadili ya uzazi,” Josephine Quintavalle,
Moja ya madhara hayo ni yale yanayosababishwa na sindano zinazotumika kuyavuta mayai ambazo husababisha mirija ya uzazi kufanya kazi kwa kulazimishwa.
Mirija ya uzazi inapolazimishwa kufanya kazi kwa nguvu kinyume na mfumo wake, husababisha ishindwe kufuata mfumo wa kawaida wa kuyatoa mayai.
Vilevile, wataalamu wa saikolojia wanasema kuwa kuchangia mayai, ukiwa kijana au binti mdogo kunaweza kusababisha kushindwa kupata watoto siku za usoni, hasa kisaikoloia kwa kuhisi kuwa tayari una watoto sehemu mbalimbali duniani.
Hivi karibuni kliniki ya wanawake nchini Uingereza ilianzisha benki ya kuhifadhi mbegu na mayai kwa wenye matatizo ya uzazi.
Mkurugenzi wa kliniki hiyo, Dk Kamal Ahuja anasema, anatarajia wengi watakaochangia mayai wawe ni wanawake ambao tayari wana watoto na wangependa kuwasaidia wanawake wenye matatizo ya uzazi.
“Wachangiaji wengi wanaokuja hapa ni wale ambao tayari wana watoto wana uhusiano wa muda mrefu na wameona jinsi watu wenye matatizo ya uzazi wanavyoteseka, hivyo wameguswa kusaidia,” anasema Dk Ahuja.
Kwa kliniki hiyo mchangiaji hulipwa dola za Marekani 750 (sawa na Sh1.2 milioni)kila anapochangia mbegu au mayai.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment