Thursday, 5 September 2013

Mfanyabiashara mbaroni kesi ya billionea Msuya



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz

Wakati sakata la mauaji ya mfanyabiashara, bilionea wa Tanzanite, Marehemu Erasto Msuya (43), aliyeuawa kwa kupigwa risasi 13 mwezi uliopita, likiwa halijatulia katika miji ya Moshi na Arusha, Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro limetangaza kumnasa mtuhumiwa mwingine, milionea wa madini hayo anayedaiwa kushiriki kupanga njama za mauaji hayo.


Milionea huyo, Joseph Damas maarufu kama Chusa (36), alikamatwa juzi na makachero wa Polisi mkoani humo, kisha kupelekwa Kilimanjaro kwa ajili ya mahojiano na jeshi hilo.

Taarifa zilizopatikana jana mjini hapa na baadaye kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, zilieleza kuwa mtuhumiwa  huyo jana angefikishwa mahakamani na kuunganishwa na washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya mauaji hayo.

Washitakiwa  hao ni Sharif Mohamed Athuman (31), mchimbaji mdogo wa madini na mkazi wa Kimandolu mkoani Arusha; Shaibu Jumanne Saidi maarufu kama Mredi (38), mkazi wa Songambele Wilaya ya Simanjiro na Mussa Juma Mangu (30), mkazi wa Shangarai kwa mrefu mkoani Arusha.


“Leo (jana) kwenye kesi ya mauaji ya mfanyabiashara Erasto (marehemu Msuya) ataongezwa kwenye mashtaka mtuhumiwa Joseph Damas maarufuku kama Chusa (36), mfanyabiashara wa madini, alishiriki kupanga mauaji,” alisema Kamanda Boaz jana katika taarifa yake iliyotumwa kwa  waandishi wa habari kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno (sms) kwa kutumia simu yake ya kiganjani.
 Hata hivyo, mtuhumiwa huyo jana hakufikishwa mahakamani. 


NIPASHE ilipowasiliana na Kamanda Boaz kwa njia ya simu ili kupata ufafanuzi ni kwa nini mtuhumiwa huyo wa nne, hakuonekana mahakamani, alisema kuwa upelelezi wake haukukamilika na kwamba alikuwa kwenye kikao katika Wilaya ya Same.


WASHTAKIWA WATINGA MAHAKAMANI
Awali, Wakili wa Serikali, Stella Majaliwa alidai mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Kilimanjaro, Theotmus Swai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kwamba mshitakiwa wa pili, Shaibu Jumanne Saidi maarufu kama Mredi (38), hakufika mahakamani kutokana na kuugua.


“Mheshimiwa hakimu, kesi hii ilikuwa inakuja mahakamani hapa kwa ajili ya kutajwa, tunaomba tarehe nyingine. Mtuhumiwa wa pili hakuweza kufika mahakamani kwa sababu anaugua,” alidai bila kueleza alikuwa anaumwa ugonjwa gani.

Washitakiwa hao, wanakabiliwa na kosa la mauaji ya kukusudia, kinyume cha kifungu cha 196 cha kanuni ya adhabu, sura ya 16 ya mwaka 2012.

Kwa upande wake, wakili wa utetezi, Hudson Ndusyepo, anayewatetea mshtakiwa wa kwanza na watatu, aliiomba mahakama hiyo kuuagiza upande wa mashitaka kukamilisha upelelezi wa shauri hilo haraka ili kuwatendea haki wateja wake.


Kesi hiyo ya mauaji namba 06 ya mwaka 2013, imeahirishwa hadi Septemba 18,  mwaka huu itakapotajwa tena mahakamani hapo na kuamuru washtakiwa hao kurejeshwa rumande kutokana na kesi za mauaji kutokuwa na dhamana.

DADA WA MAREHEMU MSUYA WAZIRAI  
Katika hatua nyingine, ndugu wawili ambao ni dada wa marehemu  Msuya, Antuja Msuya na Bahati Msuya, walianguka na kuzirai kwa dakika kadhaa nje ya mahakama hiyo baada ya hakimu
kuahirisha kesi hiyo.


Iliwalazimu makachero wa Polisi waliovaa nguo za kiraia na wale askari wa kikosi cha operesheni mkoa wa Kilimanjaro wenye magari namba PT 1180 na PT 1506  na wa doria ya pikipiki kuwaondoa watuhumiwa hao mahakamani chini ya kwa ulinzi mkali.

Msuya aliuawa Agosti 7, mwaka huu saa 6:30 mchana kwa kupigwa risasi kando ya barabara kuu ya Arusha-Moshi katika eneo la Mijohoroni Wilaya ya Hai karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Alifika kwenye eneo hilo akiwa peke yake baada ya kupigiwa simu na watu anaowafahamu kwenda kufanya nao biashara inayohisiwa kuwa ni ya madini ya Tanzanite.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...