Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe ameowanya watu wanaohujumu miundombinu ya reli na kuiba mataruma kwamba wakikamatwa atawanyoa nywele kwa chupa.
Alitoa onyo hilo juzi katika kikao cha wadau wa sekta ya uchukuzi mkoa wa Tanga kilichofanyika jijini hapa.
Alisema kuna baadhi ya watu wamekuwa na tabia ya kuhujumu miundombinu ya reli kwa kuiba mataruma na kusababisha sekta ya usafirishaji kwa njia ya reli kudorora na kusababisha hasara kubwa kwa taifa na jamii.
Dk. Mwakyembe alisema hivyo baada ya kupata taarifa kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa kwamba kuna baadhi ya miundombinu ya reli imehalibika katika eneo la Mkomazi na kuomba itengenezwe.
Kwa upande mwingine, Dk. Mwakyembe alisema katika kutekeleza mpango wa matokeo ya haraka sasa (Big Result Now), sekta ya uchukuzi imepewa miaka mitatu iwe imefikia tani milioni 18 badala ya tani milioni 12 za sasa za mizigo katika bandari ya Dar.
Alisema kwa upande wa reli kuna lengo la kusafirisha tani milioni tatu baada ya tani 200, 000 za sasa za mizigo kwa mwaka, huku wakijipanga kupunguza vituo vya kuchunguza mizigo barabarani ili kupunguza msongamano bandarini na mizigo ifike kwa wakati inakokwenda.
Alisema pia kuna mpango wa kupanua Kiwanja cha Ndege cha Tanga ili kiweze kutua ndege kubwa za kubeba mizigo kama vile matunda na mbogamboga ambapo pia kitapewa hadhi ya kutoa mafunzo kwa marubani wa ndege.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment