Thursday, 19 September 2013

TANZANIA YAMKATAA BALOZI WA UJERUMANI


Balozi Margit Hellwig-Boette 
Dar es Salaam. Tanzania imemkataa Balozi mteule wa Ujerumani ambaye alitakiwa kuja kufanya kazi nchini.
Balozi huyo, Margit Hellwig-Boette alikuwa amemaliza muda wake nchini Kenya na alitakiwa kuja kuiwakilisha nchi yake Tanzania.
Balozi Hellwig-Boette alikaririwa na Gazeti la Standard la Kenya akieleza kuwa anajipanga kurudi kwao baada ya kukataliwa na Serikali ya Tanzania.
Alipoulizwa juu ya suala hilo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alikataa kuzungumzia suala hilo akisema: “Watu wa Wizara ya Mambo ya Nje ndio wanaoshughulika na hayo mambo, waulizeni.”
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mkumbwa Ally alisema wizara yake haijapata taarifa za kukataliwa kwa balozi huyo.
“Suala hilo linahusu ofisi ya Rais, mambo ya uteuzi ni ya Rais. Wizara ya Mambo ya Nje haina hiyo taarifa na hata kama ingekuwapo hiyo taarifa siyo ya `public’.
“Siyo taarifa ya umma kwa maana kwamba, mchakato wake ni wa siri na hayo mambo hayana kuuliza kwa nini. Ukileta jina la mtu unayetaka aje kuwa balozi likikataliwa, hakuna kuuliza eti ni kwa nini.

“Unachofanya ni kuleta jina jingine, hata Rais hapa akipeleka jina la mtu kwenye nchi nyingine lisiporudi, hakuna kuuliza unachofanya ni kuteua tu jina jingine,” alisema Mkumbwa.
Alikariri Kifungu cha Nne cha Azimio la Vienna ambacho kinaruhusu nchi kukataa balozi wa nchi nyingine bila ya kutoa sababu.
“Nchi inayopeleka balozi katika nchi nyingine inatakiwa kutoa jina mapema kwa nchi nyingine. Hata hivyo, nchi hiyo ina uwezo wa kumkubali au kukataa uteuzi,” kinaelekeza kifungu hicho.
Gazeti hilo la The Standard, lilimkariri Balozi Hellwig-Boette akisema kuwa amekataliwa kuja Tanzania bila ya kuelezwa sababu.
“Ndiyo, Tanzania imekataa uteuzi wangu. Kwa mujibu wa itifaki za kidiplomasia, nchi husika ina haki ya kumkataa mtu aliyeteuliwa kwenda kuwakilisha nchi yake au kumkubali.
Tanzania imenikataa lakini haijatoa sababu yoyote ya kufanya hivyo.
“Nitaondoka Nairobi kurudi Berlin Alhamisi (leo) asubuhi ili nikapangiwe sehemu nyingine,” lilieleza gazeti hilo.
Hivi karibuni aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga aliandaa chakula cha jioni, lengo likiwa ni kumuaga balozi huyo baada ya kumaliza kipindi cha miaka minne akiwa anaiwakilisha Ujerumani nchini Kenya.
Misimamo yake imemponza
Gazeti hilo limesema Hellwig-Botte ambaye alikuwa Balozi wa Ujerumani nchini Kenya tangu mwaka 2009, alikuwa anajulikana kutokana na misimamo yake na hasa kupinga ukiukwaji wa haki za binadamu na mara nyingine kuunga mkono vyama vya upinzani.
Anadaiwa kutokuwa na uhusiano mzuri na Serikali ya Kenya kutokana na msimamo wake wa kuunga mkono Rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta na Naibu wake, William Ruto kushtakiwa kwenye Mahakama ya Makosa ya Jinai ya Kimataifa huko The Hague, Uholanzi kutokana na kuhusishwa na vurugu za uchaguzi.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...