Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TSPF), Dk. Reginald Mengi (kulia), akimpongeza Mhandisi Patrick Ngowi, ambaye alitunukiwa tuzo na TPSF kwa kutambua mafanikio
Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Dk. Reginald Mengi, amewataka vijana kutokata tamaa na badala yake wajitahidi kujaribu na kuthubutu ili waone fursa za kufanya biashara.
Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam katika hafla ya utoaji wa tuzo maalum kwa kijana aliyefanikiwa kibiashara akiwa na umri wa miaka 28, Patrick Ngowi.
Alisema Ngowi ni miongoni mwa vijana wa kuigwa nchini na nje ya nchi na kwamba kitu pekee kilichomwezesha kufikia hapo alipo ni uthubutu wake wa kujaribu kufanya biashara.
Ngowi alianza biashara yake kwa kukopa mtaji kwa mama yake wa Dola 1,800 na kwa sasa ameweza kufanikiwa kibiashara.
Dk. Mengi aliongeza kuwa hakuna umri wa mtu anaopaswa kufikia ili aanze kufanya biashara na kwamba vijana wengi wana macho, lakini hawazioni fursa zinazowazunguka ili waweze kuzitumia.
Dk. Mengi alisema anatamani kuona vijana wengi nchini wanapata mafanikio, lakini baada ya kuyapata wasitumie fedha zao kuwadharau wenzao wasiokuwa na kitu na kuwanyanyasa.
Ngowi alianza kufanya biashara akiwa na umri wa miaka 15, na tangu hapo amekuwa akifanya biashara mbalimbali na kwa sasa anauza umeme wa Jua.
Miaka mitano iliyopita Ngowi alikuwa na mtaji wa Sh. bilioni nne, lakini kwa sasa ameweza kupiga hatua kubwa ikiwamo kupata fedha nyingi ambazo sehemu yake ameweza kuzitumia kusaidia wanawake 1000 hususani vijijini kwa kuwasaidia kupata umeme.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Ngowi aliishukuru TPSF kwa kutambua mchango wake kama kijana na kuwataka vijana nchini kutokata tamaa na kujiona kama hawawezi kufanya biashara.
Tuzo hiyo ilikabidhiwa kwa Ngowi na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Regina Kikuli.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment