Ofisa Habari wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA),Gaudensia Simwanza
Afya za Watanzania zitaendelea kuwekwa rehani kutokana na kuuziwa vyakula visivyo na viwango huku mamlaka husika, Shirika la Viwango nchini (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) zikikiri kufahamu uwapo wa vyakula hivyo.
Uchunguzi wa muda mrefu uliofanywa na NIPASHE umeibua aina nyingi ya bidhaa za vyakula, zikiuzwa sehemu mbalimbali nchini, huku vikiwa havina nembo ya ubora unaotolewa na TBS.
Baadhi ya bidhaa zilizokutwa sokoni bila ya kuwa na nembo ya ubora zinaonyeshwa kutengenezwa nchini na zingine zikiwa zimetoka nje ya nchi.
Kwa mfano katika jiji la Dar es Salaam, NIPASHE ilifanikiwa kununua kwa uchache aina saba ya vyakula kutoka sokoni, zikiwamo bidhaa zinazopendwa na kuliwa kwa wingi na watoto na kina mama vile vile.
Bidhaa hizo za vyakula ni pamoja na Simba Creamy Cheddar Flavoured Potato Chips maarufu kama chama, ambazo zinapendwa sana na watoto, zenye uzito wa gramu 36 zinazotengenezwa Afrika Kusini, na Simba (Pty) Ltd.
Katika kundi hilo kuna biskuti aina ya Spider-Man (gramu 30), Best Biscuits (gramu 55) zinazotengenezwa na Gulled Industry Limited ya jijini Dar es Salaam.
Bidhaa zingine ni U-Fresh tropical fruit ml 350, ml 150 na ml 80, zinazotengenezwa na U-FRESH FOOD.CO. LTD pia ya jijini Dar es Salaam.
Aidha NIPASHE ilipata sokoni bidhaa iitwayo Daima Thick Yoghurt Plain, yenye gramu 150, inayotengenezwa na Sameer Agriculture and Livestock (K) Ltd ya Nairobi, Kenya.
Ukiacha wahusika wa kampuni ya U-FRESH ambao walizungumza na gazeti hili kupitia kwenye mawasiliano yanayopatikana kwenye bidhaa zao, mawasiliano na kampuni zingine hayakupatikana kutokana na kutofikiwa, kwa kutumia namba za simu na anwani za barua pepe zilizoko kwenye bidhaa hizo.
Kwa mfano NIPASHE ilipiga simu namba 0861100097 ya kitengo cha huduma kwa wateja, cha kampuni ya Simba (Pty) Ltd ya Afrika ya Kusini, ambayo haikupatikana kabisa na hata ilipoandika ujumbe kupitia anwani ya barua pepe ya kampuni hiyo ‘talk to.simba@pepsico.com, bado ulikataa kwenda.
Hivyo hivyo kwa mawasiliano ya simu namba 254-020-8016161 ya kampuni ya Sameer Agriculture and Livestock (K) Ltd ambayo nayo hayakupatikana, na hata ujumbe uliotumwa kupitia anwani yao ya barua pepe info@sall.co.ke, bado haukwenda.
Kwa upande wa msemaji wa kampuni ya U-Fresh, ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake alipofikiwa na NIPASHE kupitia kwenye simu namba 0718771999 na 0789018088 iliyoko kwenye bidhaa zake, kuhusiana na kuuza bidhaa zisizokuwa na nembo ya TBS alisema:
“Ni kweli juice ulizonitajia zinatengenezwa na kampuni yangu ya U-fresh, lakini zina TBS,” alisema wakati bidhaa hizo hazina nembo ya shirika hilo la viwango.
Wakati NIPASHE ikiwa imeibua hali hiyo, baadhi ya wananchi wameonyesha kushtushwa na kitendo cha wao kununua na kutumia bidhaa za vyakula kutoka madukani ambazo hazina viwango vya ubora uliothibitishwa na TBS.
Monica Samora, ambaye ni mkazi wa Mbezi Beach alisema kwamba kama ni madhara basi atakuwa ni mmoja wa walioathirika.
“Mimi ni mzazi na wakati ninapoenda kununua bidhaa dukani au kwenye super market kwa mfano ni lazima ninunue zawadi kwa wanangu. Sasa ukiniambia kwa mfano vyakula kama chama, ambazo watoto wangu wanazipenda au biscuit hizi, unazonionyesha kuwa hazina ubora, nashindwa kuelewa,” alisema.
TBS ilithibitisha kwamba inatambua bidhaa hizo kuuzwa bila nembo na kwamba itazisaka na kuzikamata ili ziondolewe katika soko.
Mkurugenzi wa Viwango na Ubora wa TBS, Tumaini Mtitu, alisema tatizo hilo lipo na kwamba mara kadhaa wamekuwa wakipambana kuzisaka bidhaa ambazo zinauzwa bila ya kuwa na nembo ya ubora inayotolewa na Shirika hilo.
Akizungumza na NIPASHE, Ofisa Habari wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Gaudensia Simwanza, alisema suala la kuwapo bidhaa ambazo hazina nembo siyo la kwao, ni la TBS wenyewe.
Alisema wao kama TFDA, jukumu lao liko kwenye udhibiti wa vyakula na madawa, kwamba wanapaswa kuhakikisha kuwa, vyakula vilivyoko sokoni vina ubora unaofaa kwa mlaji na ndiyo maana vyakula vyote hupitia kwao kabla havijaingia sokoni.
“Viwe vimetengenezwa ndani au nje ya nchi vinapaswa kupitia kwetu, kabla ya kuingia sokoni.
TBS haihusiki na viwango vya ubora wa bidhaa za vyakula vinavyotoka nje, wao ni maalumu kwa ajili ya bidhaa za ndani, kwa lengo la kuvi-promote hasa,” alisema.
Alipoulizwa ikiwa vyakula vyote vilivyoko sokoni toka nje ya nchi vimepitia kwao, na kwamba vinafaa kwa matumizi ya mlaji alisema:
“Kwamba bidhaa zote za vyakula toka nje vilivyoko sokoni vimepitia kwetu, nitakuwa sisemi ukweli kutokana na ukweli kwamba, nyakati hizi ni za soko huria. Na ndiyo maana tunaendesha mazoezi ya ukaguzi mara kwa mara na kukamata bidhaa zisizofaa kwa mlaji.”
Aliwaasa wananchi kushirikiana na mamlaka yake, katika kutambua na kutoa taarifa zinazohusiana na bidhaa zilizoko sokoni, ambazo hazifai kwa matumizi ya mlaji, ili kuendelea kuzidhibiti.
Katika miaka ya hivi karibuni Tanzania imekuwa soko kubwa la bidhaa nyingi zisizokidhi ubora.
Hizi ni pamoja na vifaa vya ujenzi, umeme na elektroniki kama simu za mkononi, spea za magari kiasi cha kugeuka kama dampo.
Miaka michache iliyopita tulifanya msako wa bidhaa hizo, hasa vifaa vya umeme na elektroniki ambazo ziliteketezwa. Hali hata hivyo bado ni mbaya kwa upande wa bidhaa za vyakula.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment