Saturday 28 September 2013

Washtakiwa EPA jela miaka 13


Washtakiwa wa EPA, Bahati Mahenge (kulia), Manase Mwakale (katikati) wakiwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana, baada ya kuhukumiwa.Mahenge alihukumiwa kwenda jela miaka saba wakati Mwakale akihukumiwa miaka mitano. Picha na Venance Nestory 
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu kwenda jela jumla ya miaka 13, washtakiwa watatu katika kesi ya wizi wa Sh1.1 bilioni katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).
Akitoa hukumu hiyo jana kwa niaba ya wenzake, Jaji Sekela Mushi na Sam Rumanyika,Msajili Lameck Mlacha alisema mshtakiwa Bahati Mahenge atatumikia kifungo cha miaka saba jela.
Mshtakiwa Manase Makale atatumikia kifungo cha miaka mitano jela na mkewe ambaye ni mshtakiwa katika kesi hiyo, Edda Makale atatumikia kifungo cha mwaka mmoja na nusu.

Washtakiwa wawili kwenye kesi hiyo iliyosikilizwa kwa miaka mitano, Davis Kamungu na Godfrey Mushi waliachiwa huru baada ya mahakama kuwaona hawana hatia.
Mbali na kutoa hukumu hiyo, aliamuru mshtakiwa Bahati Mahenge na Manase Makale kurejesha kiasi cha Sh1,186,534,303.27 walichodaiwa kukiiba katika akaunti EPA,iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (BOT).
Akiendelea kusoma hukumu hiyo, Mlacha aliwaachia huru washtakiwa Davis Kamungu na Godfrey Mushi baada ya kuwaona hawana hatia kutokana na upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha pasipo kuacha shaka mashtaka dhidi yao. Kabla ya hukumu hiyo kutolewa, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro aliiambia mahakama kuwa upande wa mashtaka hauna rekodi za uhalifu za washtakiwa hao.
Kimaro aliiomba mahakama kutumia mamlaka yake chini ya kifungu cha 348(1) na cha 358(1) cha mwenendo wa mashauri ya jinai sura ya 20 kuwaamuru washtakiwa waliotiwa hatiani kurejesha fedha walizochukua na kuisababi+shia Serikali hasara.
“Mshtakiwa Mahenge, Manase na Edda wameonekana wanahatia, makosa waliyoyafanya ni mazito yameiingizia nchi yetu hasara kubwa, wapewe adhabu kali,” alieleza Wakili Kimaro mahakamani hapo.
Kwa upande wa mshtakiwa Mahenge aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa sababu ana watoto wanne, wazazi wake ni wazee wote wanamtegemea.
Alidai kuwa alikuwa akihudhuria kesi kwa miaka mitano sasa toka mwaka 2008 ni kama alikuwa akitumikia kifungo hivyo aliiomba mahakama ufikirie muda huo wakati ukitoa adhabu hiyo.
Manase Makale, yeye alidai kuwa ni mgonjwa anafamilia kubwa inayomtegemea na mshtakiwa Edda Makale ni mkewe hivyo kama wote watahukumiwa watoto wao watateseka.
Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Hakimu Lameck alisema katika shtaka la kwanza la kula njama washtakiwa Mahenge na Makale walionekana wana hatia na watatumikia kifungo cha miaka mitano jela.
Katika shtaka la pili la kushughushi Manase na Mahenge walionekana wana hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano jela, katika shtala la tatu lililokuwa likimkabili Mahenge pekee alihukumiwa kifungo cha miaka saba jela.
Shtaka la nne, Mahenge na Manase walihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela, shtaka la tano, Mahenge, Manase na Edda walihukumiwa kifungo cha miezi 18.
Huku katika shtaka la sita, Mahenge na Manase walihukumiwa kifungo cha miezi 18 jela, shtaka la saba linalomkabili Mahenge pekee alihukumiwa kifungo cha miaka saba jela.
CHANZO:MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...