Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki
Kambi ya Upinzani Bungeni imemshushia tuhuma nzito Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki (pichani), ikiwamo ya kushinikiza mradi upewe msaada wa Sh. milioni 10 kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kinyume cha taratibu.
Kwa mujibu wa kambi hiyo, Balozi Kagasheki, ama kwa kujua ana maslahi binafsi na kampuni hiyo ijulikanayo kama Catherine Foundation, ulipata msaada wa Sh. milioni 10 kutoka NCAA kama wajibu wake kwa jamii.
Kambi hiyo imedai kuwa msaada huo ulikiuka kanuni za msaada ambao unaelekeza kuwa kwa shughuli za kijamii usizidi Sh. milioni 2.
Madai hayo yalitolewa na Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Bunge mjini hapa jana.
Mchungaji Msigwa alidai kuwa Waziri Kagasheki alimshinikiza Kaimu Mkurugenzi wa NCAA, amwelekeze Mhasibu kuulipa Catherine Foundation, unaomilikiwa na Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Catherine Maige Sh. milioni 10 kwa ajili ya ununuzi wa madawati Juni 18, mwaka huu ikiwa ni kinyume na mapendekezo yake ya Desemba 12, mwaka 2012 kuwa Catherine Foundation usubiri mwaka wa fedha wa 2013/2014 kwa kuwa hakuna na fedha za kutosha.
“Kambi ya Upinzani inataka kujua, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo alitumia kigezo gani kuilipa Catherine Foundation Sh. milioni 10 za msaada wa ununuzi wa madawati tofauti na kiwango kilichowekwa cha Sh. milioni 2 ? alihoji " Mchungaji Msigwa.
Aidha, Mchungaji Msigwa alidai kumekuwapo na ukiukwaji wa uendeshaji wa Mamlaka hiyo unaofanywa ma watendaji wa wizara hiyo huku Waziri Kagasheki akifumbia macho.
Mathalani, alidai katika mgawanyo wa vitalu vya utalii, kampuni mbalimbali zilipewa vitalu hivyo kinyume cha mpango wa miaka mitano wa NCAA .
“Kambi rasmi ya upinzani inazo nyaraka zinazoonyesha kuwa kampuni za Leopard Tours Ltd, Maasai Sanctuaries zilipewa vitalu vya utalii vya Ndulu na Oloololo vilivyokuwa nje ya mpango wa ugawaji wa Mamlaka kama inavyotakiwa kisheria,” alisema Mchungaji Msigwa ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema).
Hali kadhalika, alisema ni jambo la kushangaza kuwa Waziri Kagasheki, aliiandikia kampuni ya Leopard Tours Ltd barua ya kuitaarifu kwamba ameielekeza Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro kuipa kampuni hiyo ekari tano kwa dola 30,000 za Marekani badala ya dola dola 60,000 kwa ekari 10 kwa mujibu wa kanuni za ugawaji vitalu.
Pia alisema kwa kitendo hicho, alivunja sheria kwa kufanya maamuzi moja kwa moja na kampuni ya Leopard Tours Ltd na kushusha viwango vilivyowekwa kisheria bila kutoa Tangazo la Serikali.
Aidha, alisema Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imeendelea kufanya kazi bila Bodi kinyume cha Sheria ya mamlaka hiyo ya mwaka 2002, kifungu namba 5.
Alifafanua kuwa kwa mujibu wa sheria hiyo, kifungu namba 17. Bodi ina wajibu wa kutoa kila mwaka wa fedha taarifa za mahesabu ya mapato na matumizi ya Mamlaka pamoja na mali na madeni ya Mamlaka.
Pia alisema Bodi ina wajibu wa kukabidhi kwa waziri ndani ya kipindi cha miezi sita baada ya ukaguzi wa mahesabu ya Mamlaka nakala za taarifa hizo ili zote kwa pamoja, ziwasilishwe kwenye Bunge.
“Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua waziri amewezaje kuwasilisha taarifa za mahesabu ya Mamlaka bungeni bila Bodi kuwapo,? Alizidi kuhoji Mchungani Msigwa.
Hata hivyo, Balozi Kagasheki alipohojiwa kwa njia ya simu na NIPASHE kuhusiana na madai kuwa alishinikiza Catherine Foundation ipewe msaada wa Sh. milioni 10, alisema haimuingii akilini hata kidogo kwa yeye kufanya hivyo.
Alisema upo mchakato wa kuomba msaada kutoka NCCA na yeye licha ya kwamba anafahamu kuwapo kwake lakini hana habari nao na wala hauingilii.
“Mimi ni mtu wa principles (kanuni), siwezi kushinikiza kitu kama hicho, ama kweli akutukanaye hakuchagulii tusi.
Namuomba atoe ushahidi kwa hilo. Ila najua ni mwendelezo wa mashambulizi dhidi yangu ambayo alianza tangu Bunge lililopita ambayo alifikia kutaka nijiuzulu,” alisema Balozi Kagasheki.
Kuhusu kwamba aliielekeza NCCA igawe kitalu cha uwindaji kwa kampuni ya Leopard Tours Ltd kwa dola 30,000 chenye ukubwa wa ekari tano, Balozi Kagesheki alisema tangu alipotoka waziri mtangulizi wake, hakuna zoezi la ugawaji wa vitalu lililofanyika.
Alifafanua kuwa anachokijua ni kwamba Leopard Tours iliomba eneo la nje ya Hifadhi la Ndutu na kupewa kilomita za mraba 29.7 na kutakiwa alipe dola 60,000 za Marekani.
Alisema kampuni hiyo ilikataa rufani kwake kupinga hilo na ndipo yeye akaiambia NCAA ipewe kilomita 30 za mraba kwa dola 30,000 kwa kuwa haikuwa halali kufanya hivyo.
“Mimi ni Waziri nipo hapa kuhakikisha kwamba haki inatendeka. Nitakuwa waziri wa ajabu kama sitasimamia haki,” alisisitiza Balozi Kagasheki.
Juu ya Bodi ya NCAA kuendelea kufanya kazi nje ya muda wake, Balozi Kagasheki alisema Bunge liliagiza Bodi hiyo ichunguzwe na Kamati iliyoongozwa na Jaji Mihayo, iliundwa na kufanya kazi hiyo.
Alisema kamati hiyo imetoa mapendekezo yake na hatua mbalimbali zinaendelea huku uundwaji wa bodi mpya ukiendelea na kuongeza: “Hatutaki tupate Bodi isiyo makini.”
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment