Monday, 7 October 2013

COKE STUDIO IIMARISHE VIPAJI

KWA sasa katika medani ya muziki hapa nchini na duniani kote kumekuwa na harakati zinazofanywa na wadau mbalimbali wa muziki ambapo wameamua kuwekeza katika fani hiyo.
Uwekezaji huo katika muziki upo kwa aina mbalimbali, wapo ambao wanawekeza kwa kuwasaidia wasanii kujiinua kimuziki na pia wapo ambao wanajipanga kuwekeza kwa kufungua miradi kadhaa ya kukuza muziki. Miradi hiyo ni kama vile ile ya kuwekeza studio au vifaa vingine vya muziki ambapo wasanii wanaendelezwa kisanaa.
Miradi kama vile Tusker Project Fame, Epiq Bongo Star Search au ile iliyokuwa Coca- Cola Pop Idol ni moja kati ya miradi ambayo kampuni kubwa zimewekeza au kudhamini kwa lengo la kusaidia sanaa. Miradi mingine inalenga kuinua asili ya muziki kwa kuanzisha nyimbo zenye vionjo vya muziki wa asili.
Mradi wa Coke Studio ni moja kati ya miradi ya kuendeleza muziki hapa nchini wenye lengo la kuendeleza muziki wa kisasa wenye asili ya Afrika. Coke Studio ni kipindi cha muziki ambacho kitakuwa kikirushwa kwenye runinga na kwa hapa nchini kwa kuanzisha kitahusisha wasanii kama vile Nasib Abdul, ‘Diamond’ na Judith Wambura, ‘Lady Jaydee’.
Hicho ni kipindi ambacho kitahusisha wasanii wenye miondoko tofautitofauti ya kisasa kitakuwa kikiitwa Coke Studio Afrika. Kipindi hicho kinahusisha wasanii kutoka Afrika Mashariki na wengine wa kutoka Afrika Magharibi na Kusini. Wasanii kutoka kona nyingine ya Afrika ni pamoja na Seif Keita kutoka nchini Mali, King Sunny Ade, Mi, Waje, Jimmy Jat na Bez kutoka Nigeria.


Kwa upande wa Afrika Mashariki wengine ni pamoja na Octopizzo, Miss Karun na Just a Band wakiwa wanatokea nchini Kenya na pia kuna Hip Hop Panstula pia kuna Lilian Mbabazi wa Uganda. Pia wapo akina Boddhi Satva pamoja na Tumi wa Afrika Kusini pamoja na kundi la Culture Music la kisiwani Zanzibar.
Kitaanza kurushwa kesho kuanzia saa tatu usiku katika runinga ya ITV ambapo kitaanza kuoneshwa kwa miezi miwili. Wasanii hao, Diamond na Lady Jaydee ni wasanii ambao walienda Kenya kwa ajili ya kushiriki katika kurekodi kipindi hicho. Baada ya kumalizika kwa msimu wa kwanza ndio itaanza rekodi ya msimu wa pili ambapo wasanii wengine watachaguliwa pia.
Umoja wa wasanii mbalimbali kama hao wakishiriki kwenye kipindi hicho watasaidia harakati za kupata muziki wa kisasa wenye asili ya Afrika. Pia kutakuwa na wasanii walioshirikishwa katika kipindi hicho ambapo kutakuwa na wasanii kama vile Bamboo wa Kenya, Sega na Dela pamoja na Kassongo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na pia Temi Dollface kutoka Nigeria.
Akizungumza na waandishi wa habari Meneja wa Bidhaa wa Coca-Cola Tanzania Maurice Njowoka anafafanua kuwa Coke Studio itakuwa ikioneshwa Kenya, Uganda, Tanzania na Nigeria. Anaongeza kuwa itaenda hewani kwa vipindi vinane vya dakika 45 kila kimoja huku kukiwa na saa mbili za vipindi maalum kwa mwaka mpya.
Anaongeza kuwa katika kila kipindi kutakuwa na masuala mbalimbali muhimu katika sanaa ambapo anatolea mfano wa ujengaji wa sauti za kipekee kutoka kwa wasanii. “Pia kutakuwa na fursa ya watazamaji kuona kile kitakachokuwa kikijiri nyuma ya pazia ambapo wataona namna kipindi kinavyotengezwa na mengine,” anasema Njowoka. “
"Kwani fursa kubwa sana kwa Tanzania kushirikishwa kwenye kipindi kama hiki kwa kuwa kuna nchi nyingi kama Tanzania ambazo zingependa kuwa na miradi kama hii lakini kwa sasa Tanzania ipo na wasanii wetu pia wamo,” anasema Njowoka.
Anaongeza kuwa hiyo ni fursa kubwa kwa wasanii wa hapa nchini kutangaza kazi zao za sanaa pamoja na kuonesha vipaji vyao katika nchi nyingine nyingi za Afrika. Anatolea mfano kwa nchi kama Pakistani ambao kipindi hicho kimekuwa na mafanikio makubwa huku kikikadiriwa kuwa na watazamaji milioni 77 kwenye YouTube peke yake.
Akizungumzia ushiriki wake katika kipindi hicho msanii Lady Jaydee anasema kuwa amekuwa akiimba na kujitangaza sehemu mbalimbali za ndani na nje ya Tanzania. Anasema kuwa anaona kuwa kipindi hicho kitasaidia kuinua harakati zake za kujitangaza zaidi nje ya nchi.
“Kupitia kipindi hiki sisi kama wasanii mbali na kukuza vipaji vyetu, kukutana na kufanya kazi pamoja na wasani wengine lakini pia ni wakati muafaka kusema kuwa ile ndoto yangu ya kujitangaza kimataifa zaidi inaenda kukamilika,” anasema Lady Jaydee. Kwa upande wake msanii Diamond Platnumz anasema kuwa akiwa kama balozi wa Coca Cola hiyo kwake ni muendelezo wa fursa ambazo amekuwa akizipata kupitia kampuni hiyo.
Kipindi hicho asili yake ni Brazil ambapo kimekuwa kikiitwa Estudio Coca - Cola ambacho kilirushwa kwa mara ya kwanza Machi 2007. Kikiwa kinaoneshwa hapa nchini mashabiki watakuwa na fursa ya kuona na pia kupakua (downloading) vitu mbalimbali kama Video huku pia wakiwa katika nafasi ya kushinda vitu mbalimbali.
CHANZO: Habari Leo

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...