Mwanamuziki maarufu nchini, Nguza Viking maarufu kama Babu Seya (kulia) na mwanawe Johnson Nguza maarufu kama Papii Kocha, wakisindikizwa na askari Magereza baada ya ombi lao la kutaka hukumu ya
Wakili anayewatetea wanamuziki Nguza Vicking maarufu kama 'Babu Seya' na mwanawe Papii Nguza wanaotumikia kifungo cha maisha kwa makosa ya kulawiti na kubaka, Mabere Marando ameiomba Mahakama ya Rufani Tanzania kuwaachia huru wateja wake kwa kile alichoeleza ushahidi uliotumika kuwatia hatiani kuwa na mapungufu ya kisheria.
Aidha, amedai kuwa ushahidi uliotolewa na baadhi ya mashahidi wa Jamhuri haukufuata masharti ya sheria ya kupokea ushahidi wa watoto wadogo.
Marando alitoa ombi hilo jana wakati akitoa hoja ya ombi la warufani Babu Seya na mwanawe Papii maarufu kama Papii Kocha mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Mwenyekiti Jaji Nathalia Kimaro, akisaidiana na Mbarouk Mbarouk na Salum Massati.
Alieleza kuwa lengo la kufikisha ombi hilo mahakamani ni kutaka kuonyesha jinsi mahakama iliyotoa hukumu ilivyokosea kutowaachia huru wateja wake na badala yake ilitumia ushahidi wa watoto ambao ulikuwa na mapungufu ya kisheria.
“Katika hukumu yenu ya Februari 11, mwaka 2010 mlikubali kwamba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilikosea katika kupokea ushahidi wa watoto wadogo ambao hakufuata masharti ya kupokea ushahidi huo japo uliungwa mkono na ushahidi mwingine katika kuwatia hatiani warufani…” alieleza Marando.
Alidai kuwa mbali na mapungufu hayo, pia upande wa Jamhuri haukuita mashahidi muhimu kwenye kesi hiyo ambao walitajwa na baadhi ya mashahidi akiwamo Mangi mwenye duka jirani na nyumba ya Babu Seya.
“Mangi angeitwa mahakamani angesema ukweli kinyume na ushahidi wa Jamhuri hivyo kwa kuwa waliona atawaharibia kesi yao wakaamua kumuacha kwa makusudi …
pia kuna kijana mwingine Zizeli aliyetajwa katika ushahidi kwamba alikuwa akikusanya watoto kwa ajili ya kuwapeleka kwa warufani, hajaitwa mahakamani kuthibitisha tuhuma hizo” alidai Marando wakati akitoa hoja za utetezi alizowasilisha kwa saa mbili.
Upande wa Jamhuri ulikuwa na jopo la mawakili watano, ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Jackson Mdaki akisaidiana na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Angaza Mwipopo, Imakulata Banzi, Joseph Pande na Wakili wa Serikali Abrimark Mabruki.
Akijibu hoja za utetezi, Mdaki alieleza kuwa ombi lililowasilishwa na upande wa utetezi halina mashiko ya kisheria kwa sababu kifungu kilichotumika ni cha mashauri ya madai na siyo ya jinai kama ilivyo kesi hiyo iliyopo mahakamani.
“Tunaomba mahakama iyatupilie mbali maombi haya kwani kukubali kuyasikiliza na kuyatolea maamuzi ni sawa na matumizi mabaya ya mahakama… maombi haya yamefunguliwa chini ya kifungu cha mashauri ya madai na siyo kesi za jinai tunaomba mahakama kuyatupilia mbali” alieleza Mdaki.
Jaji Kimario baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, alisema mahakama inakwenda kuyapitia na itayatolea maamuzi tarehe itakayopangwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment