Wednesday, 9 October 2013

Mgomo wa mabasi watikisa Dar, Mikoani

Baadhi ya wasafiri na wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, wakiangalia mabasi yaendayo bara yaliyokuwa yamezuiwa na wamiliki wake kusafiri kupinga magari hayo kupita kwenye mizani jijini Dar es Salaam jana.

Mgomo wa mabasi jana ulitikisa mikoa kadhaa nchini na kuwaathiri maelfu ya wasafiri waliokuwa wakisafiri kwenda mikoa mbalimbali na nje ya nchi.

Maelfu ya abiria walikwama kwa saa kadhaa katika Kituo cha Mabasi cha Ubungo (UBT) jijini Dar es Salaam kufuatia mgomo wa wamiliki wa mabasi waliokuwa wakishinikiza serikali kusikiliza kilio chao cha kutaka wasiwe wanaingia mizani.

Mgomo huo ulianza asubuhi na kusababisha taharuki kwa abiria huku madereva wakiamriwa na waajiri wao kutoyaondoa mabasi hayo kituoni.

Wamiliki hao waliitisha mgomo kupinga utaratibu wa magari hayo kupitia kwenye mizani kwa madai ya kucheleweshwa kwa kuwa hayapakii mizigo kama inavyodaiwa na serikali.

Dalili za kuwapo kwa mgomo huo zilianza kuonekana mapema alfajiri, baada ya abiria kufika na kuingia kwenye mabasi hasa yale yenye ratiba ya kuondoka saa 12:00, lakini ulipofika muda wa kuondoka, madereva hawakuyatoa baada ya kupokea maelekezo kutoka kwa waajiri wao.




Baada ya sakata hilo kuonekana kuwa kubwa, Polisi wa kituo hicho waliingilia kati na kuwalazimisha baadhi ya madereva ambao walikuwa ndani ya magari kuyaondoa, jambo lililosababisha wamiliki kuwaamrisha madereva hao kutoka nje na kuyaacha huku abiria wakiwa ndani.

Dereva wa basi la kampuni ya Sai Baba lenye namba za usajili  T 684 BCD linalofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Nairobi, alilazimika kutimua mbio na kutokomea kukwepa kuswekwa rumande baada ya kujikuta ameondoa gari lake kituoni bila kujua kama kulikuwa na mgomo.

Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohammed Mpinga, alifika kituoni hapo saa 12:00 asubuhi na kushuhudia hali halisi jambo lililomfanya kuzunguka kwenye mabasi kuwatafuta madereva ili waondoe magari yao, lakini hakuwaona.

Kamanda Mpinga kwa kushirikiana na Conrad Shio, Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) Kanda ya Mashariki, Leo Ngowi, Meneja wa Leseni wa  mamlaka hiyo, walilazimika kuwatafuta wamiliki wa magari hayo ili kuzungumza nao.

Kutoondoka kwa mabasi hayo, kuliwafanya abiria waamue kupiga kelele wakihoji sababu za kukatiwa tiketi huku wamiliki wa mabasi wakijua kuwa kutakuwapo na mgomo.

Zaituni Nassoro, ambaye alikuwa anasafiri kwenda Mombasa, Kenya, alisema kitendo kilichofanywa na wamiliki wa magari hayo siyo cha kiungwana.

Jacqueline Amos pamoja na Simon Mwakajinga, waliokuwa wakisafiri kuelekea wilayani Sumbawanga, walisema kuna haja ya kutunga sheria itakayowabana wamiliki wa mabasi hayo kutofanya mgomo kama wamewakatia abiria tiketi ili kuepusha usumbufu kama huo.

Baada ya vurugu hizo, Polisi walilazimika kuyaondoa kwa nguvu magari hayo huku gari la polisi likiwa mbele na mabasi yakiwa nyuma.

Baada ya mazungumzo na mvutano wa muda mrefu, pande hizo mbili zilikubaliana na magari yakaanza kutoka kituoni hapo ilipofika saa 2:45 kufuatia makubaliano kuwa magari hayo hayatapitia kwenye mizani na Polisi kuwahakikishia Taboa kwamba wameshatoa taarifa kwa maofisa wake walioko katika vituo mbalimbali.

“Tumekubaliana na Sumatra, Polisi na wamiliki wa mabasi kuwa magari yote kwa leo yasipime kwenye mizani ili kuunusuru mgomo huu na abiria wasikubali kukatiwa tiketi kabla hali hii haijakuwa sawa," alisema Kamanda Mpinga.

Kwa upande wake, Shio alisema mgomo huo siyo halali kwani kitendo cha kumkatia tiketi abiria na kugoma kumsafirisha ni kinyume cha sheria.

Naye  Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Martini Ntemo, alisema kuwa mpaka sasa wizara yake haijatoa tamko lolote zaidi ya lile lililotolewa na Waziri wa wizara hiyo, Dk. John Magufuli.

Wakati huo huo, wamiliki hao wa mabasi wametoa siku mbili kwa serikali kuyatekeleza madai yao vinginevyo watagoma tena.

Hayo yalisemwa na Mweka Hazina wa Taboa, Issa Nkya, baada ya kikao kilichowashirikisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Suleiman Kova na Sumatra.

Alisema Sadiki aliyapokea malalamiko yao na kuahidi kuyafikisha kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Jitihada za NIPASHE kumtafuta Mkuu wa Mkoa hazikuzaa matunda baada ya simu yake ya mkononi kuita bila ya majibu.

MJINI MOSHI
Mjini Moshi, idadi kubwa ya wasafiri waliokuwa wakisafiri kuelekea Dar es Salaam na mikoa mingine, walikwama na kusota kwa zaidi ya saa tano huku wengi wao wakilazimika kusitisha safari.

Pia ulanguzi wa tiketi kwa mabasi ya mikoani hasa yaendayo Dar es Salaam, ulifanyika tangu alfajiri kutokana na baadhi ya mawakala wa mabasi kuuza tiketi kinyemela kati ya Sh. 30,000 hadi 35,000 kwa mabasi madogo ya kukodi na hata baada ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro kuamuru mabasi yote yaliyopo katika kituo hicho kuanza safari kabla ya serikali kuyachukulia hatua.

NIPASHE lilishuhudia idadi kubwa ya abiria wakiwa na watoto wadogo wamezagaa katika kituo hicho huku kukiwa na mabasi madogo yanayotoka katika miji midogo na wilaya za mkoa huo yakiingiza wasafiri kituoni hapo na polisi nao wakipambana kuimarisha ulinzi kila kona ya Manispaa ya Moshi.

Wakati madereva wa mabasi hayo wakiwa wamesitisha safari na wengi kati yao wakiegesha mabasi nje ya kituo hicho, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kilimanjaro, Joseph Mwakabonga, alikuwa akihaha kunusuru mali za wasafiri na kuzungumza na madereva na kuwasihi kuanza safari kabla ya kuchukua hatua, hali iliyosaidia na na baadhi ya mabasi kuanza safari saa 5:00 asubuhi badala ya saa 12:00  asubuhi.

JIJINI ARUSHA
Jijini Arusha, mabasi yanayofanya safari zake katika mikoa ya Tanga na Dar es Salaam, yaligoma kuondoka kwa saa tatu na kusababisha msongamano mkubwa wa abiria.

Madereva waliojitambulisha kwa majina ya Khalifa Mallya, Swalehe Amri na John Mollel, walisema wanashangaa kuona wanalazimishwa kuondoa magari yao kituo cha mabasi.

“Tutaondoka hapa lakini hatujui tutawapeleka wapi abiria na safari yetu itakapokwamia ni hapo hapo... huku ni kutesa abiria, bora tungeacha kuwachukua hapa kituoni mpaka mgomo umalizike,” alisema Mollel.

Baadhi ya abiria Anna Asenga, Janeth John na John Samuel, walisema wanasikitishwa kuona hali hiyo kwa sababu walipotoka nyumbani walikuwa waondoke saa 12:00 asubuhi, lakini waliondoka saa 2:00 asubuhi na hawajui hatma yao huko mbele ya safari.

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas, akizungumza na madereva hao Kituo Kikuu cha Mabasi Arusha, aliwataka wasafirishe abiria kwa sababu kuvunja safari ya mtu aliyopanga siyo
busara.

Juzi serikali ilisema haitaondoa uamuzi wake wa kufuta msamaha wa tozo kwenye mizani kwa uzito wa magari uliozidi ndani ya asilimia tano ya ule unaokubaliwa kisheria licha ya wamiliki wa malori wanaosafirisha mizigo mikoani na nchi za nje, kusitisha kutoa huduma kuanzia juzi.

Imeandikwa na Enles Mbegalo na Samson Fridolin, Dar; Cynthia Mwilolezi, Arusha na Godfrey Mushi, Moshi. 
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...