Saturday 12 October 2013

Mkapa: Kutosoma vitabu ni kujiongezea janga la umaskini


Dar es Salaam. Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa amesema idadi kubwa ya Watanzania hawapendi kusoma vitabu hali ambayo inachangia umaskini kuanzia ngazi ya kaya mpaka taifa.
Kauli hiyo ameitoa jana wakati wa kuzindua Kampeni ya Usomaji wa Vitabu kwa Watanzania (Lets reads Tanzania) iliyoandaliwa na Umoja wa Vijana wanaopenda kuandika vitabu nchini.
Mkapa alisema usomaji wa vitabu unasaidia kuongeza uwezo wa kuchambua mambo mbalimbali zikiwamo changamoto za kimaisha, kujenga ufahamu na kuchochea kasi ya maendeleo ya mtu binafsi.
“Huo ni ukweli usiopingika kwamba, Watanzania hawapendi kusoma vitabu, na hiyo ni dalili mbaya kwa taifa linalohitaji kupiga hatua za kimaendeleo katika nyanja zote,” alisema Mkapa.
Aidha, aliongeza kuwa elimu ya darasani pekee haiwezi kuwa msaada wa kuwakomboa vijana kukabiliana na changamoto za kimaisha.
“Mimi nilipenda sana kusoma vitabu na kwa sasa ni mwandishi wa vitabu, wiki chache zijazo nitazindua kitabu changu kitakachozungumzia miaka 10 ya uongozi wangu,” alisema.
Mkapa alisema utamaduni wa kusoma vitabu huongeza ufahamu wa kujua mambo mengi.
“Nawashauri someni vitabu vya akina Shabani Robert, Chinua Achebe badala ya kushinda vijiweni tu,” alisema Mkapa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba alisema asilimia 44 ya Watanzania kwa sasa ni watoto, ambapo idadi kubwa wanaopatikana maeneo ya vijijini hawapati mazingira mazuri ya kusoma vitabu.
“Waliopo mjini pia hawana mazoea ya kusoma na badala yake wamekuwa wakitumia muda mwingi katika mitandao ya kijamii, tusipokuwa makini tutawapoteza vijana hao,” alisema Makamba.
Akitoa mapendekezo sahihi, Makamba alisema ni vyema Serikali na Jamii wakatengeneza mazingira ya kuwajengea uwezo wa kujisomea vitabu ili wapate uwezo mkubwa wa kukabiliana na changamoto za kimaisha.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...