Wednesday 30 October 2013

NILISHAURIWA KUMUUA HUYU, KISA? MLEMAVU


Mtoto mwenye ulemavu, Oini Meng’ariki akiwa nyumbani baada ya kutoka shuleni katika Kijiji cha Kivululu wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha.Picha na Filbert Rweyemamu 

Oini Meng’oriki ni mtoto aliyezaliwa Septemba 11,2009; ni miongoni mwa watoto waliozaliwa akiwa na ulemavu wa viungo,hana mikono na miguu yake ina ulemavu kiasi kwamba hawezi kutembea.
Ni kwamba miguu yake imepinda, kiasi kwamba hata kukanyaga chini ili atembee inakuwa ngumu.
Hata vidole vyake haviko sawa vilivyo vidole vya miguu vya watu walio wengi. Kwa ujumla ana tofauti ya namna miguu yake ilivyo ukilinganisha na watu walio wengi.
Hata hivyo ukionana nae utatamani kuendelea kuwa nae kutokana na kuonekana mwenye tabia njema, sura ya matumaini na kuonyesha furaha muda mwingi wa maisha yake.
Tabia yake ya furaha, imesabisha awe na marafiki wengi, licha ya udogo wake wa umri.
Oini ni mtoto wa kwanza kwa mama yake Eva Meng’oriki (21) akiwa ni mke wa tatu kwa mume wake Meng’oriki Sumeno mkazi wa Kijiji cha Kambala,Wami Dakawa Wilaya ya Mvomero, Morogoro katika jamii ya wafugaji wa Kimasai.

Eva anasema baada ya kujifungua na kuona mtoto aliyempata ana ulemavu alishtuka kwa vile hajawahi kutokewa.
“Kama mwanadamu mwingine yeyote nilishtuka, lakini baada niliona haya ni mambo ya kawaida, naamini ni mpango wa Mungu, hakuna la kufanya zaidi ya kumpenda na kuahidi kumtunza,” anasema.
Anaongeza kuwa “Naamini Mungu ni kila kitu katika maisha yetu yeye akiamua kitu fulani hakuna wa kukipinga,” anasema.
Anaongeza kuwa “Nisingeweza kumkufuru Mungu wala kumlaumu kwa lolote, kwani amenipatia mtoto ambaye ana ulemavu kwa mapenzi yake na anajua kwanini imekuwa hivi.
“Jambo la kushangaza ni kwamba baadhi ya wanawake niliokuwa nao hospitali ya Bwagala,Turiani baada ya kujifungua waliniambia nisimnyonyeshe ili afe kwa njaa.
“Nilisononeka sana kuambiwa kauli ile, nilichojifunza ni kwamba huenda kuna walemavu wengi wanauawa, kwani ni wanawake wengi waliokuwa wakinishauri nimuue, namshukuru Mungu kwamba sikuwahi kukubaliana na ushauri wao hata kidogo, sikutaka mwanangu afe, niliona kama ni mashetani wale waliokuwa wakinishauri huo unyama.
“Nimuue kwa kosa gani alilofanya, kwani yeye alipenda kuzaliwa hivi alivyo? Ni dhahiri nchini kuna haja ya kuendeshwa kwa elimu ya watu kuwa na roho nzuri kwani kama ingekuwa ni mwenye kushawishika haraka leo hii mtoto huyu asingekuwa hai,”anasema Eva.
Anasema hata baada ya kupingana na wale wanawake waliokuwa wakimshawishi amuue, bado wengine waliendelea kumsisitiza afanye hivyo kwa sababu eti kuwa na mtoto mlemavu ni kama mkosi katika familia.
“Ni jambo la ajabu sana, wanawake wanaonekana wenye roho nzuri, lakini ndiyo waliokuwa wakinishauri kuua mtu eti kisa ni mlemavu, hiyo siyo sawa. Ni lazima watu tuwe na roho nzuri, tuwe na huruma...mtu amezaliwa mlemavu, badala ya kumuonea huruma unafikiria kumuua, huu ni uonevu ambao lazima watu tuachane nao...ni lazima watu tuwe na haya, kwa sababu Duniani kwenyewe tunapita, hatuna haki ya kuua wala kufanyiana mabaya, Mungu ana sababu zake,” anasema.
“Kuna mwanamke ambaye alinifuata karibu nilifikiri anataka kuniambia mambo ya maana, kumbe ananifundisha namna ya kumuua mtoto ili kabla ya kutoka pale hospitali kuelekea nyumbani awe amekufa.
“Mojawapo ya mbinu za kumuua ni hiyo ya kumnyima kumnyonyesha au hata kumnyima pumzi, ili mradi tu afe haraka kabla watu wengi kuja na kujua kuhusu mimi kujifungua mtoto huyu mlemavu,” anasema.
Anasema kwa namna anavyoona ni kwamba kuna watoto wamekuwa wakiuawa hospitalini.
“Wamepata wapi ujasiri wa kusema nimuue mwanangu, nafikiri wapo watoto ambao wamekuwa wakiuawa pale tu wanapobainika wamezaliwa wakiwa na viungo tofauti,” anasema Eva, akionya wenye tabia hiyo kuachana nayo kwa sababu walemavu nao ni watu na wanayo haki ya kuishi.
Anashauri kwamba kwa jinsi alivyoona hali ya ushawishi wa watu hasa akina mama akiwa hospitali, ni vizuri Serikali kusimamia vizuri watoto wote wanaozaliwa.
Kwamba ikiwezekana baada ya mtoto kuzaliwa, wawe chini ya uangalizi wa Serikali ili kuona kama wako katika hali gani, kwamba kama itabainika mtoto ana ulemavu, Serikali itoe kauli na maelekezo makali kwa mzazi au wazazi wote wawili.
Eva anaamini kwamba kama angekuwa mtu mwenye kufanya kila anachoambiwa na watu, leo hii mtoto wake huyu asingekuwepo, angekwisha muua kwani waliomshawishi walikuwa tayari hata kumsaidia kufanya kwa vitendo kama angeomba msaada huo.
“Hawakuishia tu kutoa ushauri, ni kama walikuwa tayari kwa lolote ili mradi tu mwanangu asiwepo, lakini wanashindwa kujua kwamba unaweza kuzaliwa mzima na ukapata ulemavu. Ni vizuri tukaachana na roho mbaya za uuaji na utesaji walemavu.
Baada ya kukaa hospitali, Eva alifanikiwa kushinda ushawishi wote aliopewa. Safari ya kurudi nyumbani ikaanza, akiwa na matumaini kuwa huenda hali ya mambo ingekuwa safi kwa maana ya kuepukana na zile kelele za kumshawishi kuua alizokuwa akiambiwa kule hospitali.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...