Kibaha/Dar es Salaam. Mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha ITV, Ufoo Saro amejeruhiwa vibaya baada ya kupigwa risasi mbili jana alfajiri huko Kibamba, Dar es Salaam.
Katika tukio hilo linalodaiwa kufanywa na mzazi mwenzake, Anthery Mushi ambaye alijiua baadaye, pia anadaiwa kumuua mama yake Ufoo, Anastazia Saro.
Ufoo alipigwa risasi moja tumboni na kutokea kwenye mbavu na nyingine ilipita kifuani hadi kwenye ziwa lake la kulia na kutokea kwenye mkono wa kulia.
Baada ya tukio hilo, Ufoo alipelekwa katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako alifanyiwa upasuaji.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lililosababisha vifo hivyo na kumjeruhi mwandishi huyo.
Kova alimtaja Mushi, ambaye alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Saro akidai kuhusika na tukio hilo.
“Mushi alimpiga risasi za kifuani mama yake Ufoo, ambaye alifariki palepale. Pia alimpiga risasi mwandishi huyo na baadaye alijiua kwa kujipiga risasi chini ya kidevu, risasi ambayo ilifumua kwa kiasi kikubwa eneo la juu la kichwa chake.”
Kova aliwaambia waandishi wa habari waliokuwa katika Hospitali ya Muhimbili kuwa, vifo hivyo vimetokana na wivu wa mapenzi.
Mashuhuda wa tukio
Akizungumzia tukio hilo, mdogo wa mwandishi huyo, Goodluck Saro alisema dada yake Ufoo na shemeji yake Mushi walikwenda nyumbani kwa mama yao huko Kibamba saa 12.00 asubuhi na kwamba baada ya kufika huko walikuwa na mazungumzo na mama yao ambayo hata hivyo, hakuyafuatilia kwa kuwa alikuwa amelala.
Goodluck alisema, muda mfupi baadaye alisikia sauti ya mama yake, ikimwita; “Goodluck nakufa... Goodluck nakufa.”
Alisema alitoka chumbani na kwenda sebuleni ambako alimkuta Ufoo akiwa ameanguka chini huku akichuruzika damu.
“Ufoo aliponiona aliniagiza nirudi chumbani mara moja. Niliporudi chumbani, Mushi akaanza kupiga risasi ovyo,” alidai Goodluck.
Goodluck alisema alikuwa chumbani na ndugu zake Jonas Saro na Abel Innocent, ambao walilazimika kupanda darini ili kuokoa maisha yao.
Alidai kuwa baada ya Mushi kuona amewakosa ndugu zake Ufoo alikusanya nguo zote na kuziweka karibu na mtungi wa gesi, ambao aliupiga risasi na kusababisha kuwaka moto.
“Tukiwa darini tulizidiwa na moshi tukalazimika kupasua paa na kuruka nje ya nyumba,” alisema Goodluck.
Baada ya kutoka nje alisema walipiga simu polisi na ilipotimu takriban saa tatu asubuhi polisi mmoja alifika lakini baadaye waliongezeka na hivyo kupata ujasiri wa kuingia ndani ya nyumba.
Mtuhumiwa akutwa na tindikali, kamba na shoka
Goodluck alidai kwamba walimkuta shemeji yao akiwa amejiua huku akiwa ameketi kwenye kiti na kichwa chake kikiwa kimefumuka jambo ambalo alisema wanaamini kuwa alijipiga risasi.
Goodluck alisema baada ya ukaguzi, askari walimkuta akiwa na kitu kinachoaminika kuwa ni tindikali, shoka, mifuko ya plastiki, kompyuta ndogo, kamba, pingu na risasi nane.
“Tunahisi alikuwa na risasi kama 17 hivi kwani alitumia tisa hivi wakati wa tukio hilo na zikabaki nane,” alisema Goodluck.
Baadhi ya majirani walisema walisikia milio ya risasi na wakati wakiulizana kulikoni, alitokea mtoto anayeishi kwenye nyumba ya marehemu na kuwaomba msaada akisema kulikuwa na ugomvi.
“Tulipokwenda tulichungulia na kuona damu zimetapakaa chumba kizima, pembeni tuliuona mwili wa mama yake Ufoo Saro ukiwa umelala chini. Nyumba ilikuwa imejaa moshi mzito, tulipiga simu polisi kutoa taarifa,” alisema mmoja wa majirani, Bobroy Ngowi.
Licha ya kuwa katika maumivu makali, hadi polisi wanafika, Ufoo alikuwa ameshatoka katika eneo la tukio mwenyewe.
Ufoo aelezea mkasa mzima
Akizungumza kwa taabu wakati akiwa kwenye gari la wagonjwa kutoka Tumbi kuelekea Muhimbili, Ufoo alisema alijivuta kutoka nje na kutembea mwenyewe hadi barabarani.
Alisema baada ya madereva wa Boda Boda kumwona anavuja damu nyingi, walimpakia na kumpeleka Tumbi.
Hata hivyo, alipofika Tumbi, anasema hakuchukuliwa vipimo kutokana na kutokuwepo kwa mtaalamu wa x-ray ndipo ilipoamuliwa kuwa apelekwe Muhimbili.
Akiwa amefuatana na Mwandishi Wetu, Julieth Ngarabali Ufoo licha ya kuwa na maumivu makali, alisimulia kilichomsibu.
Ilikuwa baada ya kufika Kibaha mizani Ufoo alipomwita mwandishi wetu: “Julieth naomba uiname nikusimulie kitu... Unajua aliyefanya haya ni Baba Alvin (Mushi). Amempiga risasi mama na mimi mwenyewe.”
Baada ya kusema hivyo, alinyamaza na kuanza kububujikwa na machozi.
Baada ya kufika Kibamba alipata nguvu na kusimulia kuwa mama yake alikuwa amefariki katika tukio hilo... Huku akilia, alisema kuwa alipewa taarifa hizo na polisi.
“Masikini mtoto wangu Alvin sijui itakuwaje, baba yake amejiua, amemuua mama yangu na babu yake alishafariki... sijui atabakia na nani, maana sijui kama nitapona,” alisema huku akilia.
Ufoo ambaye alitoka katika chumba cha upasuaji saa 12 jioni, alisema atakapopata nafuu ataweka hadharani mkasa mzima uliosababisha mauti na majeraha hayo.
Mushi ni nani?
Mushi alikuwa mfanyakazi kitengo cha mawasiliano cha Umoja wa Mataifa huko Darfur, Sudan na alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Ufoo kwa zaidi ya miaka 10.
Pia aliwahi kufanya kazi ITV na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), akiwa mpigapicha wa televisheni.
Baada ya kuondoka kwenye fani ya habari alijiunga na Mahakama ya Kimataifa inayoshughulikia kesi za Rwanda (ICTR), kabla ya kwenda Sudan.
Ofisa wa Kitengo cha Habari cha Umoja wa Mataifa huko Darfur, Said Msonda alisema kuwa Mushi alikuwa amehamishwa kutoka kituo cha El-Jenina na kupelekwa kile cha Al-Fasha.
“Tulikuwa tumepanga kumwandalia tafrija ya kumuaga baada ya kurudi kutoka Tanzania na haya ndiyo yametokea,” alisema.
Kaka mkubwa wa marehemu, Silva Mushi alisema mdogo wake alikuwa Moshi kabla ya kuja Dar es Salaam.
“Nilikuwa sijawasiliana naye siku nyingi na nilikuwa sijawahi kusikia kama alikuwa na matatizo yoyote na Ufoo,” alisema.
Mazishi ya mama wa Ufoo
Msemaji wa familia ya kina Saro, Iddi Lema alisema kuwa mazishi ya mama yake Ufoo yamepangwa kufanyika Ijumaa katika Kijiji cha Mashari, Machame mkoani Kilimanjaro.
Lema alisema msafara wa kuelekea huko utaondoka Dar es Salaam Alhamisi na kwamba ndugu, jamaa na marafiki watakutana kesho saa 10.00 kwenye Ukumbi wa Urafiki kwa ajili ya kufanikisha taratibu hizo.
Imeandikwa na Julieth Ngarabali, Aidan Mhando, Fidelis Butahe, Pamela Chilongola na Sanjito Msafiri.
CHANZO: Mwananchi
No comments:
Post a Comment