Sunday, 20 October 2013

UKISAIDIWA SEMA ASANTE KISHA SAIDIA WENGINE


Leo ni siku ya kusema asante katika safu hii ya MOYO UNADUNDA. Nami kama ndiyo mchokoza mada ningependa kusema asante kwa Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuandika makala katika gazeti hili kwa miaka mitatu sasa. Ilikuwa mwezi kama huu 2010 makala zangu zilipoanza kuonekana katika gazeti hili. Nawashukuru wasomaji wangu ambao bila kuchoka wamekuwa wakiwasiliana na mimi kunipa maoni yao kuhusu makala mbalimbali ninazotoa kwa jamii.
Hilo limenipa MOYO wa kuendelea kuandika na imenisaidia kujijenga zaidi katika uandishi wangu. Ukweli katika kipindi cha wiki mbili ambapo gazeti lilikuwa limefungiwa nilijihisi upweke sana. Sasa mambo ni shwari na naendelea kupokea maoni ya wasomaji.
Nasema asante kwa uongozi wa Mwananchi kunipa nafasi ya kujidai katika gazeti lao. Nasema asante kwa wale wanaozipitia makala zangu kabla hazijachapishwa ili kuhakiki ubora wake. Nasema asante kwa wote hao kwa sababu najua ni kitendo cha kiungwana kusema asante kwa watu wote waliotoa mchango uliokuwezesha wewe kuwa katika hali uliyonayo.

Binadamu tuna mahitaji mbalimbali yanayotulazimisha wakati mwingine kuomba msaada kwa wenzetu. Si jambo la ajabu kuwa na shida, kwani hiyo ndiyo hali ya kibinadamu. Kuna watu walifiwa na wazazi/mzazi mmoja wapo wakiwa bado watoto wadogo na wakajitokeza watu kuwasaidia katika masomo mpaka wakamaliza vyuo vya juu.
Inakuwa ni busara kuwashukuru wale waliojitoa katika kuhakiksha kwamba unapata elimu hiyo. Wapo wale waliokwama kiuchumi katika maisha kiasi cha kukata tamaa, lakini wakajitokeza watu wa kuwasaidia kwa kuwaonyesha njia ya kutokea, kuwakopesha au kuwafadhili mitaji.
Hawa nao wanatakiwa kuonyeshwa uungwana kwa kusema asante. Wapo wengine ambao maisha yao yamegubikwa na matatizo yanayowasababishia msongo wa mawazo ambao unaweza ukawashawishi watu hao kutoa uhai wao, lakini anajitokeza mtu ambaye anatoa msaada wa kisaikolojia na kumfanya mhitaji huyo kuishi maisha ya kawaida.
Hakika mtu kama huyu asipomshukuru huyo aliyemkwamua kutoka katika hali hiyo ya msongo wa mawazo atakuwa ni wa ajabu. Ni lazima aseme asante. Ila asante tunazozitoa zingekuwa na maana zaidi kama anayeshukuru angefanya hivyo kwa kuwasaidia wengine ambao nao wana mahitaji.
Mtu aliyezoea kusema asante tena inayotoka moyoni anaweza asielewe kabisa kwa nini nimeileta mada hii. Hata hivyo, kwa wale ambao wamekumbana na watu ambao kwao kusema asante wanajihisi kama wametoa utu wao, wananielewa hiki ninachokitoa leo.
Ukweli kuna watu hawana hulka ya kushukuru kabisa na wengine wanakwenda mbele zaidi kwa kuwafanyia visa watu waliowafadhili. Kwa upande wangu mimi nafikiri hii inatokana na mawazo ya watu ya kufikiri kwamba msaada wanaopewa ni haki yao.
Mwenye jukumu la kukusomesha ni baba na mama yako. Anapojitokeza mtu mwingine nje ya hao inabidi umwangalie mara mbili mbili kwa utu aliouonyesha. Si haki yako bali ni kwa huruma yake ametenda hayo aliyoyatenda. Yeye anawajibika kwa familia yake.
Katika maisha yetu ya kawaida hakuna fedha isiyo na kazi. Mtu anapokufadhili ujue amejinyima mengi yeye na familia yake kwa jumla.
Yote haya kayafanya kwa ajili yako, kwa nini usiseme asante? Wapo wanaosikitisha zaidi, kwanza wanashindwa kutoa asante kwa watu wanaowafadhili na juu ya hayo wanawatafutia visa hao hao waliowafadhili.
Kisa! Sasa hawahitaji msaada tena. Mtu mwenye mawazo kama hayo lazima atakuwa na upeo mdogo sana wa kupambanua mambo. Ni sawa na mtu ambaye alikuwa na kiu sana na kwa bahati nzuri anakuta kisima chenye maji mazuri sana, lakini baada ya matumizi anaamua kuyachafua bila kujali kwamba wapo wengine wanaoyahitaji maji hayo. Wakati mwingine watu hao watakaoyahitaji hayo maji ni ndugu zake wa damu.
Ndivyo ilivyo kwa mtu anayembeza mtu aliyemfadhili. Akipata tatizo lingine na awezaye kulitatua ni huyo aliyeshindwa kumwambia asante na badala yake kumbeza atafanyaje? Je, watoto wake anawaweka katika hali gani? Kitendo alichokifanya kinamkwaza mfadhili, wakala wake au mtu mwingine yeyote mwenye ukaribu na huyo mfadhili kutoa msaada kwa wengine.
Wengine wanadiriki hata kutafuta makosa waliyofanyiwa wakati walipokuwa wanafadhiliwa. Hivyo utawasikia wakilalamikia huduma mbovu na mambo mengine chungu mzima.
Sishawishi mtu kumlipa yule aliyemsaidia lakini nazungumzia utu wa mtu katika kusaidia wengine. Pengine kule kushindwa kuwasaidia wengine kungekuwa ni somo kwa wahusika. Kwamba wewe unacho lakini mkono wako ni mzito kabisa kwa wenzio. Hiyo ingetosha kukuonyesha kuwa kumbe kutoa ni kazi nzito. Hivyo umheshimu yule akupaye.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...