Friday, 1 November 2013

ALAMA ZA UFAULU KIDATO CHA NNE, SITA ZASHUSHWA

Waziri ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
Dk.Shukuru Kawambwa


Wakati wanafunzi wa kidato cha nne wakitarajia kuanza mtihani wa taifa wa kumaliza elimu ya sekondari Jumatatu ijayo, serikali imetangaza rasmi mfumo mpya wa usahihishaji wa mitihani kwa kushusha alama za ufaulu.

Hatua hizo zinatafsiriwa kuwa ni juhudi za kupata mwarobaini wa kuendelea kuporomoka kwa viwango vya ufaulu, uamuzi ambao pia umefuta daraja la sifuri kuanzia mwakani.

Aidha, mfumo wa upangaji wa madaraja umebadilika kwa kushusha viwango vya alama. 

Hatua hiyo imechukuliwa umma ukiwa bado unahoji kilicho nyuma ya pazia juu ya matokeo ya aibu ya mwaka jana ya kidato cha nne baada ya asilimia 60 ya watahiniwa kupata daraja sifuri (kufeli).

Mabadiliko hayo na utaratibu wa kuimarisha mfumo huo wa ufaulu yataanza kutumika katika kupanga matokeo ya mtihani kwa kidato cha Nne na Sita kwa mwaka 2013/2014.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome, alisema uamuzi huo umetokana na maoni ya wadau wa elimu kuhusu upangaji wa viwango vya alama katika mitihani kwa Kidato cha Nne na Sita na kwamba utazingatia matumizi ya alama za tathmini ya mwanafunzi (CA) na kuamua kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi.


Alisema katika muundo wa kwanza wa upangaji matokeo alama na kupanga madaraja wa zamani utakuwa tofauti na wa sasa, kutokana na mabadiliko ya mfumo huo kutumika kwa muda mrefu.

Awali Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) lilitumia alama A, B, C, D na F huku alama A ikianzia maksi asilimia 81-100, B= 61-80, C=41-60, D= 21-40 na F 0-20.  Aidha kulikuwapo na madaraja ya l, ll, lll, lV na 0.

Kwa mujibu wa mabadiliko hayo, alama zitashuka ambako alama A itakuwa ni  (75-100) B+ 60-74, B 50-59, C 40-49, D 30-39, E 20-29 na F 0-19.

Profesa Mchome alisema alama A itahesabika kuwa ni ufaulu uliojipambanua, B+  ufaulu bora sana, B ufaulu mzuri sana, C ufaulu mzuri, D uhaulu hafifu, E ufaulu hafifu sana na F ufaulu usioridhisha.

Alisema kuanzia mwaka huu kiwango cha pointi za kupanga madaraja kimeshushwa. Daraja la kwanza litaanzia pointi 7 hadi 17, daraja la pili 18-24, daraja la tatu 25-31, daraja la nne 32-47 na daraja tano 48-49.

Muundo wa madaraja wa miaka ya nyuma ulikuwa pointi 7-17 kwa daraja la kwanza, 18-21 daraja la pili, 22-25 daraja la tatu, 26-33 daraja la nne na 34-35 daraja la sifuri.

Alisema kuanzia sasa matokeo ya tathmini ya mwanafunzi katika masimo yake ya darasani yatatumika kupanga kiwango cha ufaulu katika matokeo ya mtihani wa mwisho wa sekondari na kwamba yatachangia kwa asilimia 50 kwa Tanzania Bara.

Kwa upande wa Zanzibar watatumia asilimia 40 ya matokeo ya tathmini endelevu ya mwanafunzi huku mtihani wa mwisho ikiwa utachangia kwa asilimia 60.


Alisema mkakati huu ni moja ya mikakati katika kuleta tija wa ‘Matokeo Makubwa Sasa’(BRN), na kwamba muundo wa matokeo kwa shule za sekondari hapo baadaye utatolewa kwa wastani (GPA).

MITIHANI YASAMBAZWA VIZURI
Pia Profesa Mchome alisema kuwa maandalizi ya usafirishaji wa mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne utakaoanza Jumatatu ijayo kwenda mikoani unaendelea vizuri.

Alisema watahiniwa waliojiandikisha ni 427,906. Kati ya hao, watahiniwa wa shule ni 367,399 na wa kujitegemea ni 60,507.


Hata hivyo, hakueleza mabadiliko yaliyofanyika ya alama na madaraja kwa upande wa kidato cha Sita zaidi ya kusema tu kwamba wamefuta alama S (subsidiary). 
Alipoulizwa sababu ya kuifuta, alisema hakuna haja ya kuendelea kuitumia.

Alisema kutokana na mabadiliko hayo kwa sekondari, yatabadilisha mfumo mzima wa matokeo kwa vyuo vikuu ambao unaendelea kufanyiwa kazi.

Katika matokeo ya mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka jana, wanafunzi asilimia 60 walipata daraja la sifuri  huku asilimia 24 wakipata daraja la nne. Kwa maana hiyo, asilimia 84 ya wanafunzi waliofanya mtihani huo wasingeweza kuendelea na masomo ya kidato cha tano au yale yanayohitaji ufaulu mzuri.

Baada ya matokeo hayo ya aibu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliunda kamati kuchunguza matokeo hayo. Hata hivyo, kamati hiyo hadi sasa haijaweka hadharani matokeo ya uchunguzi.

Kamati hiyo iliundwa na wajumbe 15, chini ya mwenyekiti Prof. Mchome na Makamu wake alikuwa Bernadetha Mushashu (Mbunge wa Viti Maalumu – Kagera).

Wengine James Mbatia (Mbunge wa Kuteuliwa ambaye alikataa uteuzi), Abdul J. Marombwa (Mbunge wa Kibiti), Profesa Mwajabu Possi (Chuo Kikuu – UDSM), Honoratha Chitanda (CWT) na Daina Matemu (TAHOSSA) na Mahmoud Mringo (TAMONGSCO).

Wengine ni Rakhesh Rajani (Twaweza), Peter Maduki (CSSC), Nurdin Mohamed (Bakwata), Suleiman Hemed Khamis (Baraza la Wawakilishi), Abdalla Hemed Mohamed (Chuo Kikuu – Suza), Mabrouk Jabu Makame (Baraza la Elimu Z’bar na Kizito Lawa (Taasisi ya Kukuza Mitaala).

Wakati kamati hiyo ikiendelea na kazi yake, serikali ilitangaza kutafuta matokeo hayo ya aibu na kuiagiza Necta kupanga upya matokeo hayo katika alama na madaraja ambayo yaliwanusuru takribani wanafunzi 30,000 waliokuwa wamefeli.

Licha ya kupanga upya matokeo hayo, shule nyingi za serikali zilikosa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano kutokana wengi wao kukosa sifa.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...