Thursday, 7 November 2013

CHINA KUWACHUNGUZA RAIA WAKE WALIOKAMATWA NA MENO YA TEMBO


Balozi wa China nchini, Lu Youping

Serikali ya China kupitia ubalozi wake nchini umelaani vikali vitendo vya uhalifu vikiwamo vya biashara ya magendo ya meno ya tembo na kwamba imetuma maafisa wake nchini kuwachunguza raia wake wanaodaiwa kukamatwa na pembe hizo na ikibainika ni kweli watachukuliwa hatua kali.

Kutolewa kwa kauli hiyo kumekuja siku chache baada ya kukamatwa kwa raia watatu wa China nchini wakiwa na meno ya tembo takribani 706 kinyume cha sheria katika eneo la Mikocheni, Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.


Akizungumza na NIPASHE jana, Naibu Mshauri Mkuu, Kitengo cha Siasa, katika ubalozi wa China nchini, Li Xuhang, alisema sheria za kimataifa ikiwamo ile ya  ‘Vienna Convention’ ambayo nchi hiyo pia imeridhia kuhusu kesi kama hizo, mtu yeyote akikamatwa na biashara ya meno ya tembo kuanzia kilo sita kinyume cha sheria, anapaswa kupewa adhabu kali ikiwa ni pamoja na kuhukumiwa kifungo cha si chini ya miaka kumi gerezani.

Alisema serikali ya China kupitia ubalozi wake nchini umeshapeleka maafisa polisi watakaoungana na wa Tanzania kwa ajili ya kufanya uchunguzi zaidi kuhusiana na raia wake waliokamatwa na meno ya tembo na kwamba wakithibitika, watashirikiana na serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kupelekwa mahakamani.

Balozi wa China nchini, Lu Youping, kupitia taarifa yake, alisema kuwa serikali ya nchi hiyo, inapambana vikali  na kitendo chochote kikiwamo cha biashara ya magendo ya meno ya tembo pamoja na bidhaa zake na kwamba yeyote anayekwenda kinyume na sheria ya utunzaji wa wanayama pori anapaswa kuadhibiwa vikali.

“Ubalozi wa China nchini, umeshitushwa na habari ya raia hawa watatu wa China waliokamatwa na askari polisi wa Tanzania kwa tuhuma za kufanya magendo ya meno ya tembo. Sasa upande wa China unafanya uchunguzi kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania ili kupata hali halisi,” alisema Dk. Youping na kuongeza:

 “Balozi wa China pamoja na ubalozi wake nchini, tunalaani vikali kitendo hiki cha mauaji ya tembo na biashara ya magendo ya meno ya tembo, na kwa dhati tunaiunga mkono serikali ya Tanzania kupingana na suala hili. 

Sambamba na hilo, ubalozi huo umewaasa raia wa nchi hiyo wanaoishi au kufanyakazi na wale wanaoitembelea Tanzania, kufuata sheria  ili kutunza sura ya nchi hiyo na kuendeleza ushirikiano mzuri baina ya nchi hizo.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...