
“Tarehe 26 hadi 31 ya Oktoba nilikuwa kwenye mkutano huko Afrika Kusini na Jeshi la Polisi la nchi hiyo, lilitoa taarifa kuwa kuna ongezeko kubwa la viwanda vinavyotengeneza dawa za kulevya ndiyo maana vijana wengi wanatumika ama kupeleka kemikali au kusafirisha dawa hizo kwenda katika nchi nyingine,” Alfred Nzowa
Wakati watanzania wawili waliokamatwa na kilo 55 za dawa za kulevya huko Erhukuleni, Ghauteng, Afrika Kusini, wakipanda kizimbani leo, Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya,Alfred Nzowa, amesema, nchi hiyo sasa ni tishio.
Alisema Watanzania wengi wameingia katika biashara ya dawa za kulevya kwa sababu ya viwanda vya kutengeneza dawa hizo, vilivyoenea katika sehemu nyingi za nchi hiyo.
Kamishna Nzowa alisema hivi sasa nchi hiyo ina viwanda vya kutengeneza dawa za kulevya ndiyo maana hata Julai mwaka huu, Watanzania wawili, Agnes Gerald na Melisa Edward walikamatwa wakiwa na kemikali za kutengeneza dawa hizo, zifahamikazo kama Ephedrine.
Juzi, Watanzania wawili walikamatwa na kilo 55 za dawa za kulevya zenye thamani ya Sh11.7 bilioni katika Kitongoji cha Kempton Park, Ekurhuleni, Gauteng.
“Tarehe 26 hadi 31 Oktoba nilikuwa kwenye mkutano huko Afrika Kusini na Jeshi la Polisi la nchi hiyo, lilitoa taarifa kuwa kuna ongezeko kubwa la viwanda vinavyotengeneza dawa za kulevya ndiyo maana vijana wengi wanatumika ama kupeleka kemikali au kusafirisha dawa hizo kwenda katika nchi nyingine,” alisema Nzowa.
Alisema kwa sasa nchi hiyo inasifika kwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya Cocaine kupitia njia ya maji, ambayo imepata umaarufu kwani si rahisi kwa wasafirishaji kukamatwa.
“Tunachofanya ni kuhamasisha ulinzi na usalama mipakani, Afrika Kusini inapitisha na kuingiza dawa za kulevya kwa wingi, tofauti na wengi tunavyofikiria,” alisema.
Julai 5 mwaka huu, Watanzania wawili, Agness na Melissa walikamatwa na kilo 180 za kemikali zinazotumika kutengeneza dawa za kulevya aina ya Ephedrine. Hata hivyo waliachiwa huru baada ya Masogange kukutwa na hatia ya kusafirisha kemikali hizo na kupigwa faini ya Sh2.3 milioni.
Nzowa pia alisema polisi wa Afrika Kusini na wa Tanzania wanashirikiana katika kupiga vita dawa za kulevya katika nchi hizo mbili hasa baada ya Watanzania wengi kubainika kuwa wanasafirisha dawa hizo ndani na nje ya Afrika Kusini.
“Tunapokutana katika vikao vyetu wanatupa taarifa zote kuhusu hali ya dawa za kulevya, wana majina ya Watanzania wanaoshikiliwa huko na hata marubani wa Kitanzania waliokamatwa na dawa huko Afrika Kusini,” alisema
Nzowa alisema nchi ambazo zinatoa taarifa za ukamataji kwa wingi ndizo zinazofanya kazi yake vyema tofauti na nchi ambazo zipo kimya.
Alisema kitengo chake kwa sasa kinafanya kazi kubwa ya kukamata wasafirishaji na kudhibiti usafirishaji wa dawa za kulevya vita.
Mkuu huyo wa kitengo, alielezea matumaini yake kuwa kama wananchi watashirikiana na polisi, biashara na matumizi ya dawa za kulevya hapa nchini, inaweza kupungua kama si kukoma kabisa.
Biashara hiyo imekuwa ikiwahusisha watu mbalimbali na wakati fulani Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, aliwahi kusema kuwa Serikali inawafahamu baadhi ya watu wanaojihusisha na biashara hiyo lakini haina ushahidi wa kutosha kuwakamata na kuwashtaki.
No comments:
Post a Comment