Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe
Waziri
wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ametangaza rasmi kumalizika kwa
fungate kwa watendaji wa serikali mkoani Tanga ikiwamo Mamlaka ya
Bandari (TPA), Mamlaka ya Mapato (TRA) na Jeshi la Polisi, kutokana na
kuhusika moja kwa moja na mtandao wa magendo hasa upitishaji wa dawa za
kulevya na pembe za ndovu.
Hatua hiyo inafuatia kuwepo kwa bandari bubu 49 mkoani Tanga ambazo
zimekuwa zikihusika na upitishaji wa bidhaa kwa magendo ili kukwepa
kodi, zikiwamo dawa za kulevya, wahamajia haramu na pembe za ndovu.
Dk. Mwakyembe aliyasema hayo jana wakati akizungumza na watendaji wa
TPA, TRA, wafanyabiashara na wadau wanaotumia bandari ya Tanga muda
mfupi tu baada ya ziara ya ukaguzi katika wilaya ya Pangani na bandari
ya Tanga.
Alisema ili kuthibitisha kauli yake hiyo atawataja kwa majina wahusika
na vinara wa mtandao huo na kwamba kuanzia sasa anatangaza rasmi vita
baina yao.
“Tunawajua kwa majina msione tumekaa kimya tu na mitandao yenu
tunaijua…jeshi la Polisi wanasaidia kuwasindikiza, yaani Tanga imekuwa
ni kituo cha kupokea bidhaa haramu…sasa honeymoon (fungate), ndugu zangu
imekwisha,” alisisitiza Waziri huyo.
Dk. Mwakyembe alieleza kutoridhishwa kwake na utendaji kazi wa TRA
mkoani hapa na kusema kuwa ataliwakilisha kwa Waziri wa Fedha, Dk.
William Mgimwa ili hatua za haraka zichukuliwe.
Awali, akizungumza katika mkutano huo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA,
Kipande Madeni, aliwataka watendaji wa mamlaka hiyo mkoa wa Tanga
kuendela kujituma katika utekelezaji wao ikiwamo kufanya kazi kwa saa 24
kama wanavyofanya Dar es Salaam.
Naye Kaimu Meneja wa TPA Mkoa wa Tanga, Freddy Liundi, alisema kuwa
bandari hiyo inatarajia kupokea vifaa aina ya Baji vyenye uwezo wa
kupakua mzigo hadi wa tani 3,500 kwa kontena 196 zenye urefu wa futi 20
mwezi Disemba, mwaka huu.
SOURCE:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment