Friday 29 November 2013

KAPTENI MSTAAFU ROBERT: SITASAHAU NILIPOHUKUMIWA MAISHA JELA -SEHEMI YA 2


Rubani wa ndege aliyeonja kifo kwa ajali ya ndege na kifungo cha maisha, 
Rubani huyu ni Kapteni Mstaafu Rodrick Robert(69). Picha na Maktaba 
Mwandishi: Unakumbuka nini kwenye vita hivyo?
Rubani: Nakumbuka siku moja nilikuwa off (napumzika kidogo), nikaamua kunywa bia. Na ratiba ilikuwa ikionyesha nitakuwa kazini kesho yake. Lakini ghafla kiongozi wangu alinijia na kunitaka nirushe ndege. Mimi nilikataa katakata kwa sababu nilikuwa nimekunywa pombe. Niliwahi kumwendesha Nyerere.
Mwandishi: Je, ni kweli ulimwendesha Nyerere? Na kazi ya jeshi iliendelea hadi lini?
Rubani: Ni kweli baada ya vita vya Amini niliendelea kurusha ndege za jeshi na pia kufanya kazi ya kuendesha ndege ya Rais Nyerere. Mwaka 1983 Januari 7, nilikamatwa na wanajeshi wengine wengi kwa tuhuma za uhaini. Tulidaiwa tulitaka kumuua Rais Julius Nyerere. 
Nilikamatwa nikiwa eneo la Airwing Dar es Salaam. Tulikaa kizuizini hadi Julai mwaka 1983 Mahakama ilipotangaza kwamba hatukuwa na kesi ya kujibu. Lakini cha kushangaza mwaka 1985 watu tisa kati ya wale walioshikiliwa mara ya kwanza, tulikamatwa tena na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kutaka kumuua Rais Nyerere.
Mwandishi: Je, kiukweli mpango huo ulikuwapo?
Rubani. Aaa...ulikuwapo haukuwapo, ‘it was planned by high official (ulipangwa na baadhi ya maofisa za ngazi za juu)’, unajua baada ya vita vya Uganda nchi ilikuwa imefilisika. Haikuwa na unga, sabuni, sukari na hata nguo, karibu kila kitu hakikuwapo. Hivyo Watanzania wengi walikuwa wamechanganyikiwa na hali ile.
Mwandishi: Kwa maana hiyo mpango huo ungefanikiwa je bidhaa hizo zingeonekana?
Rubani: Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi aliiokoa nchi baada ya kuruhusu kila kitu kiingie nchini hata bila ya kutoza kodi. Mwinyi aliituliza nchi. Pia Serikali iligundua kwamba waliokamatwa walitaka mfumo wa vyama vingi vya siasa ili kuishtua CCM ambayo ilikuwa imejisahau na hivyo kuanzishwa kwa vyama vingi jambo ambalo lilitekelezwa baadaye.
Mwandishi: Matatizo yaliyokuwapo enzi hizo na sasa unatofautishaje?
Rubani:Kama nilivyosema, enzi za Nyerere nchi ilifilisika, Mzee Mwinyi aliiokoa nchi, Rais Mkapa akaweka msingi wa kukusanya kodi, hivi sasa sijui kinachoendelea kwa kuwa sisomi sana magazeti kwani sina fedha za kununua.
Mwandishi: Mama Robert ulifanikishaje safari yako kurudi Songea. ?
Mkewe: Mimi niliposikia anafungwa maisha nilipigwa na butwaa na simanzi kubwa. Hivyo sikuwa na nguvu, lakini cha ajabu, baada ya saa 12 kupita, mkuu wa kikosi aliniita na kunitaka niondoke kwenye nyumba ndani ya saa 24. Kumbuka wakati ule mimi nilikuwa nafundisha Chuo Cha Utumishi Magogoni Dar es Salaam, hivyo nilihitaji kupata nafasi ya kuomba uhamisho na kufunga mizigo. Lakini mambo ya jeshi ni amri na nilitolewa mizigo ili nisafirishwe kwa ndege ya Jeshi ambayo nayo iliharibika. Lakini kwa bahati ilipona kabla ya saa 12 kumalizika, nikatakiwa nitaje niende wapi.
Suala hilo lilinifanya nitaje Songea kwa vile nilikuwa na watoto sita na Robert na watoto walikuwa wakiwafahamu ndugu wa Songea.
Hivyo mizigo na watoto walisafiri kwa ndege mimi nikabaki Dar es Salaam nikiomba uhamisho wa kwenda kufundisha Shule ya Sekondari ya Songea Wasichana.
Kwa kweli ilikuwa fedheha kubwa. Serikali inampenda mfanyakazi mzuri, lakini huyohuyo akiteleza kidogo ni takataka. Ipo haja ya kubadilisha msimamo huo.
Mwandishi: Kwako rubani, je unalo neno kwa Serikali?
Rubani:Aaaa , tangu nifike huku sijapata na wala sina senti ya Serikali. Wapo wenzangu waliosema eti Serikali inafikiria kutupatia chochote, lakini mpaka sasa sijasikia lolote.
Mwandishi: Kwa sasa afya yako ikoje na unajishughulisha na nini?
Rubani. Afya yangu nashukuru Mungu naendelea vyema, mambo mengine Mungu anasaidia.
Kapteni Mstaafu Rodrick Robert anasema ni suala la msingi kwa watu kuwa na moyo wa kulitumikia taifa kwani ndio msingi wa kuhakikisha tunakuwa na taifa lenye maendeleo makubwa.
“Jambo la msingi ambalo napenda kusisitiza ni moja tu kwamba kwa kila kitu ambacho mtu anafanya, anapaswa kuweka mbele maslahi ya taifa kwanza,” anasisitiza akiwaasa Watanzania kujenga tabia ya kuheshimu mila na tamaduni za taifa, pia kujali maadili ya uongozi.
Aidha anawashauri vijana kufanya kazi kwa bidii ili kuharakisha maendeleo nchini, kwani vijana ndio tegemeo kubwa kwa taifa na ulimwengu kwa ujumla kwa vile wana nguvu za kutosha.
MWISHO
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...