“Nilifika na baba hapa alinichukua toka Mwanza akaniambia ananileta kwa shangazi anayeishi hapa kuja kusoma” anasema Cosmas.
Hebu tafakari, kijana wa miaka 12 ambaye hajawahi kufika jijini Dar es Salaam, anafika Ubungo kwa mara ya kwanza akiwa na baba yake, na ghafla wanapotezana.
Hii ilimtokea kijana, Cosmas Steven, 13 ambaye alifika hapa jijini mwezi Januari akitokea Mwanza yeye pamoja na baba yake. Baada tu ya kufika katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo, Cosmas alipotezana na baba yake.
“Nilifika na baba hapa alinichukua toka Mwanza akaniambia ananileta kwa shangazi anayeishi hapa kuja kusoma” anasema Cosmas
Kwa bahati mbaya, Cosmas hakuweza kumpata baba yake na matokeo yake, aliishia kuishi katika mitaa ya jiji la Dar es Salaam ambapo kwa sasa anaishi kwa kuuza chupa tupu za maji na kucheza kamari.
Cosmas ambaye ameishia darasa la sita anasema: “Natamani kurudi nyumbani na kumuona baba yangu lakini sielewi namna ya kumpata, nnachojua ni kuwa anaitwa Steven John”
Cosmas pamoja na watoto wengine wa mitaani katika eneo hili wanaishi maisha yasiyo na utofauti na wanyama. Wanaoga katika Mto wa Msimbazi nyakati za usiku wakati watu wote wamelala.
Wanalala katika vibaraza vya maduka katikati ya jiji ambapo hata hivyo hutakiwa kuchangia gharama ya malazi ya shilingi 200 hadi 300 kwa usiku mmoja.
Chanzo chao kikuu cha mapato ni kuuza chupa tupu zinazozagaa kwa wenye viwanda na kampuni ambazo zinanunua chupa hizo kwa kilo na kucheza kamari au kuombaomba pembezoni mwa barabara.
Hata hivyo, fedha hizo wakati mwingine huenda zisiwe riziki kwao kwani usiku wanapolala vibaka au watoto wa mitaani wenye nguvu zaidi yao, huwanyang’anya kwa nguvu fedha hizo.
Haya ndiyo maisha ya watoto wa mitaani ambapo si Cosmas pekee bali lipo kundi kubwa la vijana wanaoishi mitaani Tanzania nzima.
Tovuti ya Humanium Help the Children(HHC) inaeleza kuwa katika Jiji la Dar es Salaam pekee kuna watoto 3,000 hadi 5,000 ambao wanaishi mitaani.
Pia tovuti hiyo inaeleza kuwa watoto hao wengi wao wana umri wa kuanzia miaka mitano hadi 18 ambapo asilimia 80 kati yao ni wanaume wenye umri wa miaka saba hadi 14.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment