Mtoto wa miaka saba amejikuta akibeba majukumu makubwa ya kumlea bibi yake, Martha John (64) aliyepooza kwa kumtafutia chakula na kumuogesha, eneo la Yombo Kilakala jijini Dar es Salaam.
Wawili hao wanaishi peke yao huku bibi huyo akiwa ni mtu wakunyanyuliwa ndani na kutolewa nje kwa msaada wa majirani.
Mwandishi wa gazeti hili alimkuta mtoto huyo mwenye umri mdogo akimuogesha bibi yake na kumvalisha nguo.
Martha anasema kuwa anajisikia vibaya kulelewa na mjukuu wake ambaye angepaswa kuwa shuleni lakini kwa kuwa hana mtu mwingine wa kumsaidia, jukumu hilo linabebwa na mjukuu wake.
Alisema ugonjwa umemfanya ashindwe kufanya shughuli za kumpa kipato ambacho kingemwezesha kumpeleka mjukuu wake shule.
Mjukuu wake amekuwa akimpikia chakula ambacho hukiomba kwa majirani na kanisa la Mtakatifu Karoli Lwanga lililopo eneo la Yombo Dovya, ambalo pia humpa msaada wa nguo.
Alisema kuwa bado anaishi katika maisha magumu kwani wakati mwingine hukosa fedha za kununuliwa dawa na mahitaji mengine muhimu.
Kutokana na hali yake, wakati anapotolewa nje inapofika usiku wakati mwingine anakosa mtu wa kumrudisha ndani.
Alisema wakati mwingine inamlazimu asote kuingia na kutoka ndani anapokosa mtu wa kumsaidia.
Pamoja na tatizo la ugonjwa, yeye na mjukuu wake wanaishi katika mazingira magumu ya kukosa chakula, chandarua, fedha za kununua dawa na kodi ya pango ya nyumba.
Aidha anasema kuwa, pamoja na kujaliwa kuzaa watoto 12, kati yao wawili walifariki na waliobaki hawana kazi hali inayomfanya aendelee kuishi katika mazingira magumu.
Pia anaomba msaada ili mjukuu wake aweze kupatiwa elimu kwani wazazi wa mtoto huyo hawana uwezo na jukumu hilo kaachiwa amsomeshe licha ya kwamba hajiwezi.
Ameomba wasamaria wema kumsaidia mahitaji yake kwani yupo kwenye hali ngumu ya kimaisha kutokana na magonjwa yanayomkabili.
Gazeti hili lilizungumza na mtoto huyo ambaye alieleza kuwa huwa anatamani kwenda shule kama watoto wenzake, lakini tatizo ni kwamba bibi yake anaumwa na hana fedha za kumsomesha.
Alisema huwa anamsaidia bibi yake kumuogesha pale wanapokosekana majirani, kupika, kuchota maji na kumfulia.
SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment