TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Watanzania
waishio nje Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete amesema wajibu mkuu wa Watanzania wanaoishi nje ya
nchi ni kuisemea vizuri, kuihangaikia na kuitetea nchi badala
ya kushinda kwenye mablogu wakiiponda, kuibeza na kulalamika.
Aidha,
Rais Kikwete amesema kuwa kuishi kwa Watanzania nje ya nchi kutaonekana
jambo la maana zaidi ikiwa watatumia rasilimali na fursa wanazozipata
ugenini kusaidia kubadilisha hali na maisha ya ndugu zao waliobakia
Tanzania.
Rais Kikwete pia amewaonya Watanzania hao wasije kuchanganyikiwa na kujichanganya wenyewe kwa
kuiga tamaduni za kigeni kupita kiasi.
Rais
Kikwete alikuwa anazungumza na Watanzania waishio nchini Poland usiku
wa jana, Alhamisi, Novemba 21, 2013, kwenye Hoteli ya Bristol mjini
Warsaw ambako alifikia wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku nne katika
Poland.
Aliwaambia Watanzania hao na familia zao: “Matumaini na matarajio yetu sisi tuliobakia nyumbani ni kwamba mtaisemea vizuri nchi yetu, mtaitetea nchi yenu, mtaihangaikia nchi na kuleta faida nyumbani. Ni jambo haliingii akilini kuwa baadhi yenu mnaweza kuishi hapa na kazi yenu ikawa ni kushinda kwenye mablogu mkilaumu nchi yenu wenyewe. Nchi mbaya,
viongozi hawafai..mnapata faida gani. Mnazo nchi ngapi?”
Aliongeza Rais Kikwete: “Kuhangaikia
nchi yetu ni wajibu wenu ambao hamwezi kuukwepa. Matumaini yetu ni kwamba asukuma mbele maslahi ya nchi yenu, mtatetea ustawi wa nchi yenu na ndugu zenu. Fursa zilizoko hapa mnazijua wenyewe, sisi hatuzijui. Nyie ndio mnaishi hapa, sisi tuko mbali na hatuwezi sisi kutegemewa na kutarajiwa tufanye mambo ya hapa ambayo hatuyajui.”
Alisisitiza Rais Kikwete: “Mbona kazi za ma-Ngo’s mnazifanya vizuri bila kusukumwa ama kushawishiwa lakini kazi za kusaidia ndugu zenu hamfanyi? Kama hata hamwezi kusaidia ndugu zenu mnachangia nini nchi yenu?”
Rais
amesema kuwa kwa Watanzania waishio nje kuonekana wanajali na kutetea
nchi yao kutasaidia kujenga hoja ya msingi kuhusu umuhimu wa kuanzishwa
kwa uraia pacha (dual citizenship) ambao Watanzania waishio nje
wanaulilia. “Mnaweza kuhalalisha hoja ya uraia pacha kwa kuwa watu wenye
faida kwa nchi.”
Kuhusu ombi lao la uraia pacha, Rais
Kikwete amesema kuwa ni wajibu wa Watanzania waishio nje kuongeza kasi
ya kuchangia mjadala kuhusu suala hilo ili likubaliwe kuingizwa kwenye
Katiba Mpya.
“Rasimu ya kwanza ya Katiba ililikataa jambo hilo kwa sababu hili ni jambo lisilokuwa na ushabiki na upenzi mwingi nyumbani. Ujumbe wangu kwenu ni jipangeni vizuri kutetea hoja yenu hii. Saidieni mjadala wa jambo hilo badala ya
kushinda kwenye mablogu mkijadili siasa na hivyo kusahau yenye maslahi kwenu.”
Kuhusu kuiga tamaduni za nchi nyingine na kusahau za nyumbani, Rais Kikwete aliwaambia kuwa inaelekea kuwa baadhi wachache wanaoishi nje ya nchi, wamejichanganya na kuchanganyikiwa kiasi cha kusahau mambo ya kwao.
Rais
Kikwete alitoa kauli hiyo baada ya mmoja wa Watanzania kudai kuwa suala
zima la mahari limepitwa na wakati na kuwa kutoa mahari ni sawa ni
kuwauza watoto wa kike.
Rais ambaye alionyesha kushangazwa na
kauli hiyo, alijibu: “Msiige mambo ya kigeni kiasi cha kuanza kuchanganyikiwa.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
22 Novemba, 2013
No comments:
Post a Comment