Saturday, 9 November 2013

Wachina meno ya tembo kizimbani


Raia watatu wa China wakifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana.



Wachina watatu wanaokabiliwa na shtaka la kukutwa na meno ya tembo vipande 706 yenye thamani ya Sh. bilioni 5.4, wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.


Washtakiwa hao ni Huang Gin (50), Xu Fujie (22) na Chen Jinzhan (31), walifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mfawidhi wa mahakama hiyo, Isaya Arufani kujibu tuhuma hizo.

Kabla ya kusomewa mashtaka hayo, wakili anayewatetea Edward Chuwa aliiambia mahakama kuwa, wateja wake hawajui lugha ya Kiswahili wala Kiingereza, lakini baada yamajadiliano ndugu wa mmoja wa washtakiwa hao aliyekuwa mahakamani hapo, aliapishwa ili aweze kutafsiri kinachoendelea.


Baada ya kuapishwa ndugu huyo, kesi hiyo ilianza ambapo Wakili wa Serikali Mwandamizi Faraja Nchimbi, alisoma jalada la kesi hiyo na kudai kuwa, washtakiwa kwa pamoja walikamatwa Novemba 2, mwaka huu katika Mtaa wa Kifaru Mikocheni wakiwa na nyara hizo.

Alidai kuwa, washtakiwa hao walikutwa na vipande 706 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilogramu 1880.

Wakili huyo alidai kuwa, washtakiwa hao walikutwa na vipande hivyo vyenye thamani ya sh. 5,435,865,000 wakimiliki bila kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Hakimu anayeshikiliza kesi hiyo alisema kuwa, kama wana maombi ya dhamana yapelekwe Mahakama Kuu ambapo Wakili wa washtakiwa, Chuwa aliiambia mahakama kuwa atafanya hivyo.

Upelelezi wa shtaka hilo unaendelea na kesi hiyo itakuja tena kwa kutajwa mahakamani hapo Novemba 21, mwaka huu. 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...